The Chant of Savant

Wednesday 7 November 2012

TAKUKURU na wabunge walipovuana nguo!

JAMAA wa taarabu walipoimba “Mtu Mzima Hovyo” sikujua kuwa kumbe walimaanisha! Mwenzenu juzi nilipata burdani na kutoa burdani kijiweni.
Baada ya kushuhudia wahishimiwa wa Mjengoni na njemba za Takokuru wakivuana nguo tena hadharani, niliamua kuchukua kigoma changu na kujimwaga mitaani kucheza ndundiko.
Wakati sherehe zangu za kuvuana nguo hazijatua si nikasikia kuwa vijana wa Takokuru wamemnyaka mhishimiwa Zungu ambaye hata hivyo siyo zungu kitu bali uvumishi wa waswahili. Wapi na wapi chotara wakimakonde na kiarabu akawa zungu? Hata hivyo, wanaojua mchezo wa kulindana na kugeuzana majuha walijua hawa vijana wangekemewa na mambo kuisha! Unacheza na Chama Cha Mafisi siyo? Mgosi Machungi haachi kusema tiishasema kuwa mbwa hamng’ata aiyemfuga. Hayo tuyaache.
You know what? Baada ya ile Taasisi ya Kupamba na Kupokea Rushua (Takokuru) kusema wahishimiwa ni wala rushwa si nao walikuja juu na kuigeuzia kibao ikaishia kuwa kama jibwa jizi! Kamwene Pita Msigwa ndiye aliongoza mashambulizi kwa Takokuru aliosema ni wala rushua Kaya nzima hakuna. Wanakula rushua kuliko hata Endelea Chenga na Dokita Iddiliisha Rashid.
Msigwa alisema kuwa mijamaa ya Takokuru ina utajiri kama Bill Gate. Nasikia dingi wao Eddie Washea ana njuluku kuliko hata mzee Warren G Buffet yule mshikaji wa kwenye kijiwe chetu cha Nebraska kule kwa Joji Kichaka. Huyu jamaa tulisoma wote chuo ingawa yeye hakumaliza. Hayo tuyaache.
Baada ya wahisimiwa wala rushua kuwavaa wala rushua wenzao wa kampuni ya kutetea na kukusanya rushwa Takokuru, mwenzenu nilifarijika nikijisemea kuwa sasa nimewapata. Nilicheka sana kuona huu wendawazimu na ujuha wa kitaasisi ambapo madingi waliamua kutoana nguo na kubaki watupu.
Kumbe ndiyo maana jamaa wanapigania uheshimiwa kwa kila namna ili wapate njuluku za rushua! Sasa nimeelewa. Kama sikosei, kama Bunch of Thieves (BoT) itakuwa imesheheni watoto au ndugu wa vigogo. Kwani hamkusikia kuwa hata mahospitali yote ya Dar yanasimamiwa na watoto wa vigogo waliotajwa kuwa Amani Milima ya Kighoma, Janati Joji Alihama, Asha Omare Mahitaa, Hawa Rashidu Kawa na Gwa nini Ikate ile Kamba? Hapa bado daktari Salama Kikwekwe ingawa ni mtaalamu wa njino.
Turejee kwenye uhuni wa Takokuru na wahishimiwa. Mie zamani nilidhani kuwa Takokuru hawali rushua.
Lakini baada ya kupata data kuwa jamaa hawa ni matajiri wa kutupwa nilistuka na kubadili imani yangu juu yao.
Hata hivyo, tujiulize. Hata wakiamua kama walivyokwishaamua kula rushua nani atawakamata wakati wakamataji ni wenyewe?
Hii mzee mzima ilinikumbusha kisa cha wazee wa mabao wanaomilkin ngwara ngwara bin dala dala. Magari yao hayapigwi bao. Nani atayapiga bao wakati wapigaji mabao ni wao? yaani baada ya kufichuka ufisadi huu wa wakubwa na mbwa wao nilitamani mwalimu Mchonga afufuke na kuwa rais wa kaya ili awakamate hawa jamaa na kutaifisha mali zao na kuwapeleka lupango.
Lakini kwa sasa nani atampeleka lupango nani wakati wote ni mijizi yarabi? Nakumbuka mgosi Machungi na Mipawa waliwahi kudai kuwa wahishimiwa wetu wanawakilisha matumbo yao na nyumba zao ndogo. Mimi nilibisha. Sasa nimeamini walichomaanisha magwiji hawa wa uzamizi wenye PhD za kijiwe tena bila kughushi.
Hakuna kitu kilinishtua kama Takokuru kunyamazia tuhuma nzito kama hizi. Nilidhani angalau wangejibu hata kwa majibu mepesi. Badala yake waliuchuna wakijua kuwa walevi ni wepesi wa kusahau. Na kweli wamesahau. Laiti nguvu na akili inayotumiwa kwenye upuuzi kama upinzani na chuki za kiimani vingeelekezwa kwa majambazi hawa, basi kaya yetu ingekomboka vilivyo tena haraka.
Ajabu hata mkuu wao aliyesema ana orodha ya wala rushua wote, majambazi na wauza unga aliminya wakati jamaa wa Takokuru wako chini ya afisi yake!
Hata hivyo simshangai kutokana na jinsi yeye na watu wake wanavyohomola sawa na Takokuru yake na wahishimiwa. Muulize ili ahadi ya kurekebisha ile mikataba ya kichukuaji ya uwekezaji imefia wapi?
Si amehomola na kuacha jamaa waendelee kutugeuza shamba la bibi.
Naanza kujenga hitimisho kuwa haki kwenye kijiwe chetu iko sokoni ikiuzwa na kila kibaka kwa amtakaye na bei atakayo.
Je, namna hii tusipochenjiana tusiokuwa kwenye gemu si tutaisha jamani?
Walevi mko wapi au bado mnaendelea kushikilia matumaini?
Shauri yenu mtaendelea kuliwa na wawekezaji na makuadi wao waliotamalaki kila kona. Mie simo! Haliwi mtu.
Nani atamla mvuta bangi na mlevi ambaye yuko tayari kujinyotoa roho hata bila kuudhiwa? kwa walevi walio laini wakiimbiwa nyimbo ngojera na sanaa za amani, hakika mtaliwa sana.
Hata hivyo, siyo mbaya. Mmezoea kuliwa endeleeni kuliwa tu. Kweli kaya yetu sasa imegeuka ya kulana. Walimu wanakula wanafunzi wao. Wachungaji wanakula waumini; madaktari wagonjwa; wanasiasa wapiga Kura.
Nasikia kuna makabila hata wababa wanakula vibinti vyao! Ni kulana mtindo mmoja.
Polisi wanawala wahalifu, wenye nyumba wapangaji wao bila kusahau madalali. Ama kweli kaya ya kuliwa ni ya kuliwa. Mnaipeleka wapi kaya yetu?
Kwa vile jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani, je, ni wangapi watatumia udhaifu huu kuendelea kuwala wenzao? Upuuzi ni pale jogoo wanapokunya ndani wasiguswe lakini vifaranga wakithubutu wanatishiwa kifo?
Kwani hatuyaoni ambapo wakubwa wanakula kila aina ya rushwa na kuachiwa ilhali wale wadogo wakipatilizwa? Je walevi mtaliwa hadi lini? Siachi kujiuliza.
Kama wahishimiwa tena watunga sharia wanakula rushua kweli watatunga sharia za kuzuia na kupambana na rushua au kuilinda na kuipamba kama yalivyo matendo ya Takokuru? Hakika hii ni kaya ya mafisi na mafisadi!
Naona Zungu anakuja ngoja nikamuulize alivyoua hii soo.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 6, 2012.

No comments: