Sunday, 10 February 2013

Bunge lisivumilie wabunge wahuni


Taarifa za hivi karibuni kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walichapana kiasi cha kuumizana, kudhalilisha, kutishiana hata kuwekana ndani si jambo linalopaswa kufumbiwa macho au kushughulikiwa kisiasa na kishikaji.

Ingawa tofauti ya binadamu, hata kukwaruzana, ni jambo la kawaida, kukwaruzana huku kunapohusisha wanaodhaniwa kuwa ni waheshimiwa wabunge wanaopaswa kuonyesha picha ya uongozi na uadilifu, hugeuka kuwa jambo jingine. Katika tasnia ya habari kuna dhana maarufu kuwa mbwa akimng’ata binadamu si habari. Ila binadamu akimng’ata binadamu ni habari kubwa.

Taarifa ambazo hazijakanushwa ni kwamba katika tafrani la Dodoma ambalo lilihusisha vyama viwili lilizuka tokana na kugombea mlingoti. Wengi tuliposoma habari hii tulistuka na kusikitika hasa pale wahusika wakuu walipokuwa waheshimiwa wabunge. Je hawa ni waheshimiwa au waishiwa?

Wabunge wazima wanagombea mlingoti? Waheshimiwa wazima wanafanya vitu visivyo vya heshima. Je huku si kuishiwa? Kimsingi, wabunge kama wawakilishi na viongozi wa wananchi wanapaswa kuwa kioo cha jamii. Lakini kwa kilichojiri Dodoma kinaonyesha wahusika kuwa si kioo cha jamii tena bali kilio cha jamii. Inasikitisha zaidi kuona sasa baadhi ya wabunge wanaanza kuota sugu kwenye kufanya uhuni na ubabe tena dhidi ya wananchi wanaodai kuwawakilisha. Wabunge wanaotuhumiwa kuhusika kwenye vurugu hizi ni Aden Rage (CCM-Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (CCM-Tarime), Seleman Jafo (CCM-Kisarawe), Said Mtanda (CCM-Mchinga) na Mary Chatanda (CCM-Viti Maalumu).

Mfano, Rage amejipatia umaarufu kutokana na kile wazungu huita wrong reasons.Ni Rage huyu huyu alipanda jukwaani bila aibu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kule Igunga akiwa na bastola kiunoni hapo Septemba 2011 kana kwamba tulikuwa Somalia ambako jambo kama hili ni kawaida kutokana na taifa hili kuwa kile kinachoitwa Failed state. Tanzania si failed state wala haijawahi kukaribia hapo pamoja na udhaifu wake hasa ufisadi na utawala mbovu. Ajabu ya maajabu, pamoja na Rage kutenda jinai hii, si chama wala serikali waliomkaripia achia mbali kumfikisha mbele ya vyombo vya dola. Je tunajenga taswira gani kama siyo kuanzisha uhuni na ubabe wa kimfumo?

Kwa vile Rage na wenzake ‘wako’ juu ya sheria kutokana chama chao walichokuwa wakikipigania kuwa madarakani, amenogewa na kukubuhu kiasi cha kuwashawishi wenzake kufanya uhuni ambao ni aibu kwao na hata bunge kwa ujumla.

Nilitegemea kusikia karipio la bunge baada ya wabunge kufanya uhuni. Nani amkaripie wote iwapo wahusika mfano, spika na naibu wake wanasifika kwa ubabe na uburuzaji? Rejea spika Anna Makinda alivyoua hoja ya mbunge wa Arusha, Godbless Lema alipodai waziri mkuu ni mwongo hapo Machi 11, 2011. Rejea juzi tu naibu spika Job Ndugai alivyoleta vurugu wakati mbunge wa Ubungo, John Mnyika akiwasilisha hoja binafsi kiasi cha kusababisha wabunge wa upinzani kumtolea uvivu na kususa kikao cha bunge.

Pamoja na vyombo vya habari kuripoti jinsi wabunge waliyoshiriki vurugu kikamilifu, naibu spika wa bunge Ndugai alikaririwa akijaribu kuwatetea tofauti na hali halisi. Alisema, “Pale kama wasingekuwapo wabunge hali ingekuwa mbaya sana na yule kijana angeumizwa, kwani uwapo wao ulisaidia katika kuamua ugomvi ule,”

Je wananchi ni wapumbavu waliodai kuwa wabunge walikuwa vinara wa vurugu? Je kati ya Ndugai aliyesikia na wananchi walioshuhudia zile vurugu tumwamini nani?

Je huku si kuishiwa kwa CCM? Je inakuwaje mwenyekiti wa CCM ambaye ni rais wa nchi anakubali watu wachache wadhalilishe serikali yake na chama chake?

Ni ajabu kuwa Rage hajakomaa kisiasa kiasi cha kuona aibu anayosababishia taifa na chama chake. Je tatizo hapa ni nini? Je Rage ni nani katika nchi yetu kujifanyia atakavyo bila kushughulikiwa kisheria? Je kwa rekodi hii bado Rage anapaswa kuendelea kuwa mbunge na kumilki silaha wakati hana uwezo wa kujizuia? Je mamlaka husika wanangoja Rage aue ndipo yachukue hatua? Hakika dalili za mvua ni mawingu. Rage na wabunge wa namna yake wasipodhibitiwa mapema watatugharimu kama taifa.

Kuna haja ya kuwaelimisha watu aina ya Rage kufahamu kwamba kuwa katika chama tawala siyo kuwa na leseni ya kutawala katika kila kitu. Ingawa ni mapema kutoa hukumu, taarifa za awali zinaonyesha kuwa CHADEMA walipandisha bendera yao kwanza ndipo CCM wakaamua ishushwe ili wapandishe yao. Je hapa kuna utawala bora na unaofuata sheria na kujali usawa na haki za binadamu iwapo wahuni wachache wanaweza kutumia hali ya kuwa chama tawala kuwanyima haki wengine kuonyesha hisia zao? Maneno ya Jella Mambo katibu wa CHADEMA wilaya ya Dodoma yanatosha kuonyesha ubabe wa CCM. Alikaririwa akisema, “Kwanza, wamechukua bendera yetu.

Halafu tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna agizo la Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati wa Bunge.” Ajabu hata polisi waliotoa agizo hili hawajatoa maelezo ni kwanini wanavumilia jinai hii! Je kuchukua bendera ambayo ni mali ya CHADEMA si wizi uliopaswa kufunguliwa kesi mahakamani? Lakini nani afanye hivyo wakati waliotenda jinai hii ni wafuasi na viongozi wa chama tawala? Je namna hii hatuleti vurugu inayoweza kulizamisha taifa letu iwapo wanaoonewa watasema ‘sasa basi’?

Hali inaanza kuwa mbaya hasa unapokuwa na wabunge ambao hawana mpaka na wapiga debe pale Mwenge Stendi. Je hawa waliwezaje kupenya vigezo vya uadilifu hadi wakapendekezwa au kuteuliwa kuwa wabunge? Je hii ndiyo sera ya kulindana au kupatikana ubunge kutokana na rushwa? Maana, si rahisi kuelezea namna ya wabunge wa hovyo wa hivi walivyoweza kupenya na kuchaguliwa bila kujenga shaka juu ya mfumo uliowapitisha. Kuna haya ya mamlaka husika na watanzania kwa ujumla kutowavumilia wabunge na maafisa wengine wenye mamlaka waliyopewa na umma kutowavumilia watu wahuni.

Chanzo: Dira Feb.,11,2013.

No comments: