Juzi mzee mwenzenu nilinusurika kutiwa nari na jamaa zangu nilipokuwa kule Ntwara. Si nilishinda Nanguruwe na kulala Nang’ombe. Baada ya kuuchapa
ulabu kama sina akili nzuri niliamua kwenda zangu Msimbati kushuhudia ilipo neema inayoleta balaa kwa kaya. Sikuamini nilichoona hasa nilipofika zangu Masasi. Si nilikuta chingas wamelewa hadi kuamua kufanya kweli baada ya kuona Lisirikali linataka kuwaletea za kuleta! Chinekeee! Jamaa si walichukia kama simba aliyekoswakoswa risasi. Hawakusikia cha muadhini wala mchota maji. Waliamua kieleweke kwa kufanya kweli tena kweli kweli.
Japo kaya yetu haina asili ya kuchomana, kasheshe la hivi majuzi kule Masaasi si nchezo. Gesi asili imevuruga asili. Nani alijua kuwa mijengo na mimali ya waishiwa, sorry, wahishimiwa ingetiwa nari? Imetokea.
Mlevi, kama ada, hakosi kubwabwaja visanga kama hivi vikijiri. Siku zote wazito walidhani kuwa wenye mikiki na makeke ni wao tu. Walikosea so to speak. Waliwachukulia walevi kuwa makondoo waliopigwa na ulabu kiasi cha kutoweza kufanya makeke na mikiki. Ndiyo maana mkulu na kimwana wake waliposikia akina njomba na shem zake wakiapa kwa miungu yote ya mbingu na ardhi kuwa gesi asili haiachi asili yake na kupelekwa Kinyeezi waliamua kusepa kwa pipa kwenda kwa Sepu wa Fifa, kubembea na kutanua majuu. Wenzie wako serious ye’ afanya machezo! Ashindwe nini kwenda kutumia wakati gesi itakayoingiza mshiko wa nguvu imeishagunduliwa? Angeogopa nini iwapo kila kero inapotokea wanafungulia Fanya Fyoko Uone (FFU)? Anayo simpo solution: kwenye kero ya gesi tumia geshi. Ukisikia utawala uliotukuka kwa utukutu na utukufu ndiyo huu. Maana, humtia adabu kila anayejifanya hamnazo ili wakubwa waendelee kutanua na kutimiza mipango yao bila kupingwa wala kuulizwa. Hivi wanaotaka gesi iishie Ntwara hawajui kuwa ikibaki kule, makuadi, wawekezaji na wachukuaji watasusa kwenda kule kutokana na kutokuwapo na miundo na mbinu za kuifyonza na kuifaidi gesi?
Kwa vile hii si mara yao ya kwanza kutumia zana hii hatari inayonenepeshwa na kodi za walevi, walipojitia kuleta fyoko, matabibu si walizimwa kama kibatari wakati ule mkuu na kidosho wake wakiwa zao Jomeika na Brazilia wakining’inia na kubembea? Mara hii mmesahau jinsi Dk. Stivi Ulimboka alivyotiwa adabu kiasi cha kunusurika kunyotoka roho? Wako wapi matibabu waliojitiatia kiherehere cha kutaka waongezewe mshiko? Nani angekubali upuuzi huu wa kutaka mshiko mkubwa bila ukubwa wakati ni wa wakubwa wenye matanuzi makubwa? Hakuna anayeruhusiwa kufaidi mshiko wa kaya isipokuwa mkulu na wenzake. Kama wewe si mwenzao ulie na kusaga meno kwa sana tu. Ukileta kujua jua unashushiwa kipigo cha mwizi na geshi letu linalosifika kwa kuramba shaba walevi wasio na hatia.
Huwa napenda geshi letu lililivyo na nidhamu ya ajabu. Lenyewe huwa halina cha kuangalia sura ya mtu wala nyani bali kufanya kiroboti roboti kumsulubu yeyote litakaloambiwa. Hii mijamaa ina nidhamu kwelikweli. Unajua kuwa niliona baadhi ya njemba ziliyokuwa zikitembeza mkong’oto zikiwa na buti zinazokwenda upande? Nilipopita hata kwenye lines zao niliona vituko God knows. Vijumba vichafu na vya kubabana. Ajabu ya maajabu ya nidhamu ya ajabu ni kwamba mijamaa haikuwa na haja ya kuangalia hali zao mbaya bali kuwafanyia walevi wanaoleta kiherehere cha kudai gesi isitoke Ntwara. Huwa nawashangaa walevi wawe wa gongo bangi na hata madaraka. Mfanyiwe nini ili mtumie akili? Sijasema mnatumia massaburi kama wanaowatembezea nkong’oto. La. Mnatumia vichwa ila vya panzi. Mnapaswa kuamua kweli kweli na siyo kujaribu. Msinikumbushe kisa cha maticha walipodinda na kujifanya hawajui kitu kudai eti wataacha kupiga chaki. Nambiiiiie! Wameishiwa wapi kama si kunywea?
Wote wanaotaka kuvunja amani na utulivu ‘wetu’ wanapaswa kuelewa kuwa hii kaya ina wenyewe na wenyewe ni wenye maulaji. Kama huna maulaji unataka ulaji wa nini? Kwanini kusumbua kwa kutishia maulaji ya watu? Mara hii mmesahau miradi kamambe yenye kukomboa kaya kama EPA, Richmonduli, Meremetuka UDA, Sukitaa, Mwanakaya Gold, IPiTL na madudu mengine aliyotuneemesha?
Najua kinachowasumbua watu wengi ni ujinga. Hivi hamjui kuwa gesi mnayogombea haiwezi kuwa-processed Ntwara? Wataalamu wanasema kuwa hali ya hewa ya Ntwara hairuhusu gesi kuweza kuwaka kwa vile kuna vigagula wengi wanaotishia igeuke maji ili wote tupate hasara? Kitaalamu hali hii tunaiita impasse. Kuepuka impasse na madhara yake huwa tunashauri wahusika watumie mbinu iitwayo divide and eat. Yaani unawagawanya walevi kwenye makundi hasimu nawe unaendelea kufanya vitu vyako. Kwa mfano, unaweza kuwaambia kuwa kitendo cha kutaka gesi isiondoke Ntwara licha ya kugawa kaya, ni tishio kwa usalama wa kaya. Hivyo, huwezi kuvumilia kitu kama hiki. Wakiuliza unawezaje kuvumilia madudu kama EPA, Richmonduli na mengine unasema kuwa walioko nyuma yake ni wachache. Hivyo, mnaweza kukaa pamoja na kuyamaliza kiutuuzima. Hamkusikia mkulu akisema kuwa aliwabana jamaa wa Kagoda na EPA wengine eti wakarejesha njuluku walizokuwa wamekwapua? Huu ndiyo utawala uliotukuka unaojali sheria na kulinda njuluku za umma kwa kusuluhisha kero kizimamoto. Isitoshe, wajanja wa hayo madudu hawahitaji FFU kuwatuliza kama hawa wanuka njaa. Pia, waliofanya madudu hawachomi nyumba wala gari la mtu. Wao huchoma gesi kwenda kuwekeza kule Ususio sorry Uswizi. Hawa wana tija kwa taifa maana wakati wa kuusaka ukuu wanachangia mishiko mikubwa ya kuwezesha wenye kuutaka ulaji kuwapa walalanjaa takrima nao wakatoa kura ya kula na mchezo unaishia pale kwa amani na utulivu. Au vipi?
Tumalizie kwa kuonyesha ni kwanini jibu la mgogo wa gesi ni geshi. Geshi licha ya kuwapa watu kibano, linaleta nidhamu inayowavutia wawekezaji kwenda kule kuwekeza na kuchukua gesi. Hivyo, inabidi watu wa Ntwara waelimishwe kuwa hakuna mwenye nia mbaya na gesi yao bali ni kutaka kuwaridhisha wawekezaji ambao kikanuni hawapaswi kuudhiwa au kupingwa. Maana ukiwaudhi wanasusa kuwekeza kuanzia ten percent hata mambo mengine.
Kwa leo nimejitahidi kutotumia lugha ya kitaalamu. Kwa vile naona mchuma wa FFU unatia timu, acha niishie kabla sijamtia mtu ma-karate nikafungwa bure. Imetoka hiyo!
Chanzo: Nipashe Jumamosi  Februari 9, 2013.