The Chant of Savant

Monday 18 February 2013

Je wataka kuukata kirahisi?


Mambo kwa vyama, NGOs na dini
Nina mpango kamambe wa kuukata bila kukatika. Nina mpango wa kupeta kiulaini. Nina mpango wa kuanzisha ima chama au shirika kama siyo kampuni ya kuuza neno la Mungu ili niukate. Kama nitaanzisha chama, basi bi mkubwa shurti aanzishe NGO ili aweze kula sambamba nami. Au siyo?
Nimepata sayansi hii ya kuukata baada ya kuona jamaa yangu Agussie Lyatongolwa kipindi fulani alipokuwa hajisikii vizuri. You know what? Pale Manzese nimewahi kuingia kwenye ofisi ya chama chake na kumkuta mkewe amekalia kiti chake akitoa maagizo utadhani ndiye alikuwa mkiti. Niliipenda sayansi hii ambayo kwa kitaalamu huitwa family business in the name of people’s business.
Nguli mwingine aliyenifungua macho ni Ben Bill Mkapu—usimchanganye na Mkapa---ambaye alipopata ulaji rahisi ambao wengine huuita urais alimruhusu bi mkubwa wake aitwaye Anna Tamaa kuanzisha NGO ya Fursa kwa wote wenye madaraka. Nguli mwingine aliyenivutia ni Jake M Kiquete ambaye naye alimruhusu bi mkubwa kuanzisha NGO ya Maulaji ya Wake za wakubwa.
Kama nguli wote hawa wamefanya kitu hiki kwanini nami nisitie timu ili mie na nyumba yangu tuondokane na ukapa?
Kwa upande wa kuanzisha kampuni sorry shirika la dini, nilivutiwa na magwiji kama Zaky Ka-Tortoise, Gettie Rwakatarehe, Silver Gamanyua, Luchekelo,Mtumwa Mwingila, Chris Mwakasenge na wengine wengi ambao wametokea kuwa mabilionea simply because wana sanaa za kuwakamua kondoo wa Bwana. Upo mshirika? Mambo kwa politiki kama siyo kwa Yesu ati. Kuna haja gani ya kuanzisha mkapuni wa biashara ya kidunia na kusumbuliwa na TRA wakati kuna ulaji laini na wa dezo? Kwa vile mie si mtasha wala mmanga, jamaa wa TRA hawatanipa misamaha ya kodi. Lakini nikiwazukia na neno la God wataingia mkenge na kunipa misamaha ya kodi ili niwe bilionea haraka. Hapa hata mlipa kodi hatanistukia wala kulaumu kwa vile nampa huduma yangu ya kutenda miujiza na kumfanya awe ‘bilionea’.
Hakika, huu nao ni muujiza! Unawakamua maskini na kuondoka na utajiri wakati wao wakiendelea kungoja miujiza. Unaanzisha vituo vyako vya radio na runinga kama siyo magazeti. Najua. Wanoko wataona kama naota ndoto za mchana wasijue nimeishafanya utafiti wa kina na kugundua kuwa baadhi ya jamaa wametumia kampuni za kiroho hata kuingia kwenye kampuni za uroho hasa kisiasa. Muulize Gettie Rwaka uheshimiwa wake ameunyakaje kama siyo kupata tafu toka kwenye kuuza neno la God. Usishangae siku moja kusikia mtume Nkwazi anakuja kutoa huduma ya kiroho kwa uroho mtakakitu sorry roho mtakatifu chini ya makanisa kama Church of the Creator for Mankind (CCM) au Church of Unified Faith (CUF) kama siyo Tabernacle of Almighty for International Fraternity of All (TAIFA). Kama ni biashara ya dini lazima nitoke na kitu kama Unchallengeable Lord’s Appointed Jamboree of Immortals. (ULAJI).
Kwa vile mimi nina utaalamu wa uchakachuaji, propaganda na sanaa, lazima nianzishe chama ili kuhakikisha nakomba mshiko wa kaya nzima. Lazima hapa nisimame kidete na kung’ang’ana kuhakikisha ukoo wangu na marafiki zangu tunaibuka kuwa mabilionea wa kutisha katika kaya hii. Ili kuwanasa walevi lazima, nihubiri neema na pepo hata kama wahubiriwa wataendelea kuishi kwenye nakma na moto. Who cares kama nitapa changu nao wakabaki na umaskini wao? Huu nao ni muujiza wa miujiza kuona watu wanapewa maneno ya kitapeli na kutoa pesa huku wakiamini kuwa wanafanya kazi ya Bwana. Hapa hakuna cha kazi ya bwana wala bibi zaidi ya bwana na bibi wanaowaingiza mjini.
Kauli mbiu yangu itakuwa, well we can make you richer than everybody under the sun. Najua. Walevi wanavyopenda na kuabudia kimbombo na kupenda vya dezo na kuishi kwa matumaini, wataukwaa mkenge. Lazima niwatwishe mkenge. Kwani mimi ni wa kwanza kuwabamiza mkenge? Mbona imekuwa kawaida ya wajanja kuwaingiza mkenge kila baada ya miaka mitano? Hapa kosa langu liko wapi iwapo natumia vipaji vyangu kuukata na kula kuku kwa mrija hata kama waliwa wanakula shida na karaha? Kama hamjui, huu ndiyo unaitwa ujasiriamali. Unaijasiria mali by all means available and possible kama Machavelli wa enzi za akina Lorenzo de Medici chini ya utawala wa familia uliojulikana kama Famiglia de Medici. Kwa taarifa yako, familia ya Medici ndiyo ya kwanza duniani kuwa tajiri. Najua wengi kwa sasa wanawaabudia akina Carlos Slim Helu, Bill Gates na rafiki yangu na mshirika wangu Warren Buffet. Hawa ni cha mtoto ukilinganisha na akina Medici. Anyways, hayo tuyaache.
Sijui chama changu nikiite CCM yaani Chama Cha Maulaji au CUF yaani Chuma Ule na Furahi? Hili nitaliamua baadaye.
Sijui NGO ya bi mkubwa tuiite WAMA yaani Wanyonge na Mafanikio? Anyways, tutaamua baadaye.
Leo tunaghura na mambo ya methali. Sijui kama siku hizi bado zinafundishwa pamoja na vitendawili tega na tegua urongo njoo utamu kolea. Ilm yenyewe imenyongwa na wenye jeuri ya kupeleka vigemezi vyao Majuu. Who cares? Usishangae wembamba wa reli, angalia mabehewa ilobeba. Je wainyaka ile isemayo msitu ni ule ule ila nyani wengine? Hivyo, usione wingi wa bangi na gongo ukadhani sina mipango bab kubwa na bambam. Naweza kufanikiwa. Who knows kama wengine, tena mafwala, wamepeta kwanini mimi mjanja nisipete mwanawetu? Ukitapeliwa mara nyingi utajua kuwa umetapeliwa baada ya kutapeliwa. Ole wake ajae kwetu. Hana tofauti na aendaye kwa waganga wa jadi au kienyeji au wanasiasa. Tahadhali. Hii ni kwa wenye akili tu. Again, you’ve to kiss many frogs before getting Mr Charming.
Zikomo kwa mbiri mose wa lero. Tafsiri? Siku ajirejea bwana mkubwa mtapewa.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Februari 16, 2013.

No comments: