Na kama si kuheshimu sheria, n’shawanyofoa watu roho au kuwazaba wengine
mabao hasa ndata na ‘lisirikali’ wanaovumilia upuuzi huu.
Juzi kule Buseresere, ‘walimnyotoa’ roho Mchungaji wa watu. Kisa?
Wanagombea kuchinja! Wenzetu wakisikia vitu hivi, on top of mauaji ya albino,
wanashindwa kututofautisha na hayawani hasa fisi na mbwamwitu.
Wenzetu wanashindana kwenda anga za juu, sisi kuchinjana na kupigana
risasi! How come karne ya 21 watu wanyotoana roho wakigombea kuchinja njiwa na
kuku?
Mna-‘boa’ na kutia aibu. Badilikeni, pepo si ya wauaji, wavivu wa kufikiri
wala wababaishaji. Utasikia jitu linasema (eti) dini yake ni bora kuliko
nyingine.
Una dini wewe au uduni wa udini? Wenye dini wakiitwa nawe uje! Loooh!
Hiloo! Huwa siachi kujiuliza hata kama kilevi. How come watu wanagombea dini
wakijificha kwenye udini wakati hata dini zenyewe hawazijui?
Mwenzenu nimesoma ‘matabu’ yote ya dini kuanzia, Mahabharata, Bhavagand
Gita, Shastra, Upanishad, Sri Guru Granth Sahib na Dasam Granth hadi Tao Te
Ching ya Lao Tzu.
Vitabu hivi na vile vitakatifu vya biblia na koran, vinafanana kwa jambo
moja-usimtendee mwenzio usivyotaka kutendwa.
Wa-‘ingilishi’ wanaiita hiyo kuwa, golden rule. Sisi walevi tunaiitwa
diamond rule. Ingawa vitabu vyote vilijitahidi kila kimoja kuvutia upande
wake.
Hakuna nilichokipenda kama Tao Te Ching hasa falsafa yake ya Wu wei yaani
kufuata mkondo badala ya kulazimisha mambo.
Sisi walevi tunafuata mkondo, ndio maana tukisha-‘utwika’ tunasukwa sukwa
kwenda kila upande bila kupinga. Hii ndio maana ya Wu Wei. Huna haja ya
kulazimisha mambo.
Dini ziko wazi. Hata mlevi akikupayukia usimpige risasi. Hata kama kasisi
atakutoza uchache kwa njia ya ‘swadaka’ huna haja ya kumchukia.
Hamna haja ya kuhangaishwa na kuhukumiana. Siku ya siku Bwana Mkubwa
atakata mzizi wa fitina kwa kuhukumu. Je, mkihukumu leo, siku hiyo yeye atafanya
nini?
Kwa walevi wanaoleta ujinga ujinga wa udini na uduni, wanapoteza muda wao.
Watawanyaka na kufichwa, halafu waanze kulalamika na kutishana. Wenzio
wanagombea ‘migesi’ na ‘mifweza’, ninyi mnagombea kuchinja hadi kuchinjana!
Mmechelewa kweli kweli!
Hakuna kazi ngumu na hatari kwa sasa kama kuwa mwandishi wa umbea, Padri au
Mchungaji. Ukijikuta kwenye kazi hizo jua wataku-mwangosi kama siyo
kuku-mushi.
Watashindwaje iwapo kuna mashehena kama lile liitwalo Irunga, yanahubiri
mauaji na maangamizi na ‘lisirikali’ linawavumilia?
Ukiuliza kunani? Siri kali kama kawaida! ‘Mijitu’ imekosa akili hata ya
kusoma amri ya sita yaani, usiue! Sijaona sehemu imeandikwa usilewe wala
usichinje kuku wako hadi achinje so and so.
Tunamdanganya nani? Ajabu hata watu wakubwa wamejiingiza kwenye upuuzi huu!
Kama mmechemsha muiteni mzee Ruksa awasaidie kwa kutoa ruksa kama kawaida yake
ili kila mtu ajifanyie atakavyo.
Ukila mbwa ruksa, ukinywa gongo ruksa, ukivuta bangi ruksa, ukiibia umma
ruksa, ukiwa mkristo ruksa, ukiwa muislam ruksa ila hakuna ruksa ya kuchukiana
na kuuana. Simpo!
Kwa mlevi, huu ni ulevi tena mbaya unaoitwa uduni uliojificha nyuma ya
udini. Hivi hawa wanaouana kwa misingi ya udini hawajui kuwa hili si jibu la
uduni wala udini wao?
Badala ya mpambane na mafisi na mafisadi, mnaanza kuchukukia na kumalizana
tena walevi wenyewe maskini. Kule Buseresere si walimnyofoa roho mchungaji wa
kondoo wa Bwana, baada ya kuacha kuchunga na kufanya kazi ya kuchinja.
Chinja chinja na chunga chunga wapi na wapi? Huu nao ni uduni. Badala ya
mgombee nani amefuga, nyie mwagombea nani achinje. Nauliza kilevi.
Hivi ng’ombe anayefugwa na mzinzi mwizi hata muuaji siyo haramu hata
kumchinja, achilia mbali kumla? Hivi kwenye vibanda vyenu vya kupanga,
mnakopandishiwa kodi kila uchao wanaowanyonya wanajali dini zenu?
Je, walanguzi wa bidhaa, umeme, simu, vyakula na kila kitu wanajali dini
zenu? Umaskini, ujinga, magonjwa, uhuni, uduni hata ujini hauna dini.
Lazima niwaonye. Msije mkazidisha ‘mibangi’ yenu na kupanga kuvamia mabaa,
mkidhani kitaeleweka. Tutamnyofoa mtu roho bila kujali anaamini katika
nini.
Maana ukiona walevi wanaanza kuchoma makanisa ujue kesho watachoma mabaa.
Sisi tumeishajiandaa na ‘michupa’ yetu. Tutawaponda ponda na kuwafutilia mbali.
Kwani mbwai ni mbwai!
Kuchomeana mali au kunyofoana roho ni uhuni usiopaswa kuvumiliwa.
Inashangaza ndata wanapewa ruksa to shoot to kill wanapoandamana
wapingaji.
Ila wahuni na wabangaizaji wanaojificha kwenye udini wakifanya mauaji au
uhuni unasikia tuvumilie. Jamani tuvumilie hadi lini iwapo haki hatuioni? Bila
kuwakamata hawa wahuni na kuwatupa lupango watatusumbua sana na kutuzuia
kutumbua kwa raha zetu.
Lazima walevi tunywe tutakavyo hata kama wengine hawapendi. Lazima watu
waende kwenye ibada zao hata kama mna shaka nazo. Wajua? Kama watu wangekuwa
wamepiga shule kama mimi wala wasingechukiana wala kunyofoana roho.
Mnapigania na kuchukiana kutokana na ujuha na ujinga wenu. Hivi huyo Mungu
mnayepigania mwamjua yukoje? Mnayajua mafundisho yake? Mna lenu jambo!
Kwa taarifa yenu msimchanganye Mungu kwa ‘mibangi’ na kasumba zenu. Kama
wenzenu ni wabaya kiasi hicho, jiulize aliyewaumba nani?
Hata kiti moto kaumba yeye. Hata mwana wa Adam alibadilisha maji kuwa ulabu
ili watu wafaidi na kuchangamka. Sasa makosa yako wapi kwa mlaji na
muumbaji?
Anyway, sitaki nimwage falsafa ambayo ni nadra katika anga hizi. Kwa wale
waliosoma Para-philosophy wanaelewa ninachokiimanisha.
Ukiachia mbali uduni, uhuni na udini, kuna tatizo na ujini. Majini hupenda
sana damu. Mnamwagana damu kumlisha nani kama siyo jini aitwaye udini, uduni na
uhuni?
Na nawaonyeni, ingawa mimi si mtabiri kama yule habithi shehe Yaya,
natabiri jini huyu atawasumbua msipoacha utaahira na ubwege wenu.
Damu ya Mwangosi, Kachela, Mushi na wengine wengi inapasa kutosha.
Mchinjeni jini huyu kama siyo kumchoma moto badala ya kumalizana nyinyi kwa
nyinyi. Hatosheki huyo.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Februari 23, 2013.
No comments:
Post a Comment