The Chant of Savant

Wednesday 5 February 2014

Je ni mwanzo wa mwisho wa Zitto Kabwe?


YAMEISHAANDIKWA mengi kuhusiana na hatima ya kisiasa ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), Zitto Kabwe.
Kitu kimoja tu hakijaandikwa. Nacho ni kuandika tanzia yake kisiasa.
Ukiangalia uzito wa hali ya mpapariko na mparaganyiko aliyomo Kabwe, unashawishika kuandika tanzia. Hata hivyo, siandiki hii tanzia. Wengine watafanya hivyo.
Leo nitaongelea mgogoro wa CHADEMA. Rejea kile kilichoitwa Waraka wa Kuhujumu Chama wa Kitila – Zitto – Mwigamba. Sitaki kudurusu kesi iliyoko mahakamani kama ilivyofunguliwa na Kabwe kwa vile naheshimu mahakama sana.
Ninachoweza kusema ni kwamba ubunge wa Kabwe kwa sasa unatokana na mahakama na si chama chake. Hivyo, punde si punde, Kabwe atakuwa historia ndani ya CHADEMA na sasa nyingine kwenye duru za kisiasa nchini, vinginevyo itokee miujiza.
Wengi wanahoji Kabwe atakwenda wapi baada ya kutimuliwa toka CHADEMA? Nadhani Ansbert Ngurumo alitoa jibu la swali hili kwenye safu yake ya Maswali Magumu ya tarehe 12 Januari.
Sitaki nirudie alichoandika Ngurumo. Ila naweza kusema kuwa darasa lake la walipo wale wanasiasa machachari, tena wengine toka CHADEMA hiyo hiyo wakiwa na vyeo vikubwa kuliko vya Kabwe, ni jibu tosha kwa Kabwe ambaye linapaswa kumfikirisha ili ajiandae kisaikolojia kwa pigo na anguko hili la ghafla.
Kwanini nasema Kabwe au Mkumbo waandike tanzia yao kisiasa?
Kwanza, kukiri kwa Mkumbo Kitila ndiyo ushahidi utakaotumika kumfukuza Kabwe uanachama.
Kwa kukubali kuwa waliandika waraka uliokuwa na lengo la kuhujumu chama, watatu hawa walifanya kile ambacho Wahindi huita ‘suttee’ ambapo mara nyingi wanawake waliochoka na maisha hujichoma moto.
Pili, kile kitendo cha Mkumbo kusema waraka wao haukuwa kosa, lakini akaomba msamaha, ni ushahidi wa kutapatapa ambao ulisaidia CHADEMA kumtimua uanachama. Na hawawezi kusema walionewa. Walifungwa kwa maneno yao wenyewe.
Tatu, kama wenzake Kabwe wamevuliwa uanachama kwa kosa lile lile atanusurika vipi?
Nne, hakuna kitu kiliwavua nguo wahusika na kuwaonyesha kama wababaishaji kama kitendo cha kutaka kujiuzulu ili waondoke kwa heshima.
Wengi walihoji: Kama walichotenda si kosa walitaka kujiuzulu kwa sababu gani?
Tano, wapo waliodhani kuwa Kabwe na wenzake “wangemwaga mtama” kwa maana ya kufichua maovu ya CHADEMA. Bahati nzuri, japo nia ya namna hii ilikuwapo, hapakuwapo na “mtama” wa kumwaga ikizingatiwa kuwa CHADEMA wanafanya mambo yao wazi wazi kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Kwa ngoa na usongo alivyonavyo Kabwe, kama kungekuwa na maovu yoyote yaliyotendwa na chama au viongozi wake, bila shaka asingeyataja tu bali angeyaimba kama shairi ili angalau kujifariji baada ya kupata lililompata.
Waswahili walisema: Ivumayo haidumu (hasa inapovumishwa pale isipostahiki kuvuma). Emma Bombeck katika kitabu chake “At Wit’s End”, aliwahi kusema; “Don’t confuse fame with success – usichanganye umaarufu na mafanikio.”
Naye Oprah Winfrey amewahi kusema; “If you come to fame not understanding who you are, it will define who you are – Kama ukiwa maarufu bila kujijua umaarufu utakuumbua.”
Nadhani hili ndilo linawasumbua wengi wanaokabiliwa na hali kama ya Kabwe. Hufiki mbali. Kutojitambua ni sehemu ya utoto ambao si kuvaa nepi bali kutenda kitoto, hata atendaye hivyo awe mtu mzima vipi.
Kabwe kweli alivuma kutokana na sababu mbaya tu. Au tuseme ajali ya kisiasa. Alivuma pale alipojitokeza kuwa mpambanaji mzuri na mtetezi wa haki za wananchi. Baada ya sifa kuingia kichwani, alifikia mahali kusema eti angetaja majina ya vigogo walioficha pesa ughaibuni. Baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kumvua nguo, Kabwe aliishia kunywea kwa aibu ya kuongopa na kuzua. Hadi kesho tunauliza: Yako wapi majina ya majambazi na mafisadi walioficha pesa yetu nje?
Kitu kingine kilichommaliza Kabwe ni ile hali ya kudai kuwa asingegombea ubunge kwa mara ya pili. Badala yake angwenda kufanya kazi anayopenda ya kufundisha chuoni.
Msimu wa uchaguzi ulipowadia, Kabwe aligombea huku akisahau aliyokuwa ameahidi. Kwa wapiga kura hili lilikuwa pigo kubwa. Nadhani hata CHADEMA waliliona hili na kulihofu. Wenye busara walihofu na kuhoji hili.
Yanini kupayuka wakati unaweza kujiondokea kimya kimya au kutangaza kutorejea siasa wakati wa mchakato wa kutafuta wagombea? Kupenda sifa kwingine kwaweza kuwa kitanzi kwa mhusika.
Pigo jingine kwa Kabwe ni ile hali ya kushutumiwa kuwa anatumiwa na CCM na asikanushe na kutoa majibu mujarabu. Wapo wanaoona kama ni ukweli. Maana ungekuwa uongo Kabwe, bingwa wa kuongea, asingekaa kimya.
Ukiunganisha na uvumi kuwa Kabwe atarejea kwao CCM, unaona ukweli japo kwa wanaojua mizengwe ya CCM, akifanya kosa akajirejesha kule, watamtema kama ganda la mua.
Kwa waliosikia nukuu za Januari Makamba kuwa kiongozi wa nchi awe ni mtu mwenye kujua kutunza familia yake, walishajua kuwa Kabwe hawezi kukatiza pale ikizingatiwa kuwa neno mke au mtoto bado ni msamiati mgumu tu japo nasikia ana mtoto.
Alioa lini? Watamchunguza kuanzia dada zake hadi mama yake ili wamchafue. Huu ni ushahidi kuwa huko CCM nako hakubaliki. Wameishamtumia. Hawamuhitaji tena ili asiwachafue. Kama amewasaliti wenzake, atashindwa nini kuwasaliti waliomtumia, tena kwa kumlipa jambo ambalo hajakanusha?
Licha ya ushiriki wa Kabwe kwenye kuandaa waraka husika, hakuna kilichomuumbua kama kudai kuwa hakuwa na taarifa za mpango huu mzima.
Alichodai Kabwe ilikuwa sawa na kumficha msichana unayetaka kumuoa uchumba halafu bado ukasema una mpango wa kumuoa.
Ushahidi wa kimazingira ni kwamba Kabwe alijua na kuratibu kila kitu. Kuna wanaoona kama hapa kilichokuwa kikifanyika ni kutumiana yaani wawili kumtumia Kabwe naye kuwatumia.
Hata hivyo, tuseme CHADEMA imekuwa na subira kupita kiasi, hasa kwa Kabwe na siasa zake tatanishi. Nadhani kwa uamuzi waliochukua dhidi ya Mkumbo na Mwigamba na hatimaye Kabwe utakuwa somo kwa wengine kuwa kumbe CHADEMA inaweza kung’ata, tena kwa makali zaidi.
Tumalizie kwa kumpa Kabwe nasaha fupi ya Kilatini; Consilio, quod respuitur, nullum subest auxilium – asiyekubali kushauriwa hawezi kusaidiwa.

Hivyo kaka, Acta est fabula, plaudit – mchezo kwishnei kwa lugha ya watoto wa mjini. Huo ni ushauri huenda unaweza kukusaidia kama utakubali kushauriwa.
Chanzo: Tanzania Daima Feb. , 5, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

NN Mhnago naomba faragha....nipatie email yako

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
email yangu ni nkwazigatsha@yahoo.com