Wednesday, 13 August 2014

ACT itakufa kabla ya kuzaliwa?

Mbowe, Slaa, Lissu Lema na wenzake watajwa na Zitto kuwa wahafidhina, wabadhirifu na watukuzao siasa za maji taka
SINA ugomvi na kuanzisha chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) ambacho watani wake wanakiita (Alliance of Conspirators and Traitors) ambacho ni matokeo ya mnyukano wa uongozi kwenye chama kikuu cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
ACT-Tanzania ilitokana na kumvua uongozi ndani ya chama mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye sasa amekimbilia mahakamani kuzuia asivuliwe uanachama kama walivyofanyiwa wenzake Samson Mwigamba na Dk. Mkumbo Kitila.
Huwa najiuliza: Kabwe angekuwa amefukuzwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) angekuwa bado na jeuri ya kuendelea na ubunge eti kwa vile mahakama imeingilia kati? Sitaki kuingilia uhuru wa mahakama.
Hebu tuangalie athari za kuanzishwa ACT kiasi cha kupigiwa upatu na baadhi ya vyombo vya habari. Je, ACT itafua dafu au kuishia kuwa mbio za sakafuni? Je, tunavyo vyama vingapi vilivyoanzishwa kwenye mazingira sawa na yaliyosababisha kuanzishwa ACT vikashamiri?
Hata hivyo, shinikizo la kuanzishwa chama kipya kikilenga kuumeza na kuudhoofisha upinzani si la kwanza, hivyo hatutegemei lilete madhara yoyote makubwa.
Je, wanaofadhili ACT ni nani hawa wenye ubavu wa kuunda chama ndani ya muda mfupi wakitegemea kufanya miujiza kama sio CCM kutaka kuvuruga na kuhujumu upinzani ili iendelee kuwa madarakani kinyume cha sheria?
Tumesikia anatajwa Edward Lowassa, ingawa imekanushwa kwa mbali kwamba ndiye yuko nyuma ya kuifadhili ACT ili kukidhoofisha CHADEMA, aweze kushinda kirahisi iwapo atapenya ndani ya CCM.
Je, ACT itafua dafu au watakula fedha za CCM na Lowassa tu? Kiko wapi Chama Cha Jamii (CCJ) kilichosababisha uvumi na kihoro kuwa kingewachukua vigogo toka CCM?
Kwanini CCM imeigiza siasa za kimabutu yaani uhuni wa jambazi na imla wa zamani wa Democratic Republic of Congo wa kutumia mapandikizi na vibaraka wake kuanzisha utitiri wa vyama kumwezesha kushinda?
Hii ndiyo demokrasia ya kweli ambayo CCM imekuwa ikijitapa kuwa ilianzisha wakati ikiihujumu kwa mbinu chafu mbali mbali kila uchao? Ni bahati mbaya kuwa hata hawa wanaoshabikia vyama nyemelezi, kama wao si nyemelezi basi uwezo wao wa kufikiri ni wa kutia shaka.
Tumesoma kwenye vyombo vya habari kuwa wapo waliokwishajiandaa kuhama vyama vyao ili kumfuata Kabwe. Kama kuna wanoamfuata mtu basi wamenoa kama si kutafuta gea ya kurejea kwao CCM lau wapewe mabaki ya vyeo kama walivyofanyiwa wenzao wakaishia kupotea kisiasa.
Wako wapi akina Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Walid Kaborou, Njeru Kasaka na wengine wengi waliosifika kwenye medani ya siasa? Wako wapi hawa? Walimalizwa na wakapotea na kusahaulika.  Yeyote aliye tayari kutumiwa si wa kuaminiwa na hata na anayemtumia.
Ukimshawishi mtu kumhujumu mwenzake akakubali basi ukishamtumia humdharau mtu yule. Hata nawe atakuhujumu tu. Ni suala la muda tu. Huwezi kumwamini tena. Maana kama anaweza kumdhulumu mwenzake atashindwaje kukudhulumu wewe?
Ndiyo maana wengi waliorejea CCM walipotezwa kisiasa wakabaki kuhaha na kutapatapa wakijutia uamuzi wao. Wasiopenda kujifunza watarudia kosa hili. Mlikwisha kuambiwa CCM ina wenyewe. Wanajuana, wanajulikana na wanajijua.
Wapo waliohama vyama kwa vile walikuwa maarufu wakidhani kuwa “umaarufu” wao ungewasaidia kupata madaraka. Walisahau.  Umaarufu wao ulitokana na kuwa vyamani wanamokimbia sasa.
Mwanandoa hana umaarufu akiwa mtalaka. Akitalikiwa anagundua hili. Wako wapi akina Augustine Mrema? Je, ni wangapi walimfuata wakaishia kugeukana na kufukuzana? Kwanini watu hawajifunzi kuwa ukishajifunga umemaliza. Ukivunja mkataba unapwaya na huo umaarufu wa ndotoni unayeyuka kiasi cha kupotea kama hao tuliowataja. Hivyo, upinzani hauna haja ya kuwa na hofu tokana na kuhama kwa washirikina wanaoabudia watu badala ya sera.
Ufuasi unaokifaa chama ni wa kufuata sera si mtu. Hakuna anayeweza kuzidi chama. Chama kinchozidiwa mtu awe mwenyekiti au mwanzilishi wake kitakufa kifo cha mende.
Hata marehemu baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere, pamoja na ugwiji na uzito wake, hakukizidi chama chake. Leo nani huyu anayeweza kupinga kanuni hii ya maumbile kisiasa? Hata hivyo, haishangazi ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu umekaribia na CCM inatumia mapandikizi na makuwadi wa kisiasa kuhujumu upinzani.
Waondoke tena haraka waone watakavyoanguka. Upinzani hauwezi kuendeshwa kwa ibada za binadamu. ACT itakufa kifo cha mende kama CCJ muda si mrefu. Ni bahati mbaya, hata huyo Kabwe anayeonekana kuwa mhimili wa ACT anasahau kuwa binadamu ni wale wale.
Wanaweza kumpa anachotaka. Lakini ajue muda si mrefu historia itajirudia. Ukiishi kwa upanga utakufa kwa upanga. Kama wasaka tonge wenzake watampa uongozi ni kwa muda ili wamtumie. Baada ya mawimbi ya kisiasa kuanza kuwapiga na hali ikatulia huku washitiri wao wakikitoa, naye atageukwa na wale ambao hakutegemea kama alivyowageuka aliowageuka bila kutegemewa.
Hii ni kanuni ya kawaida ya maisha. Huwezi ukawa mwizi usiibiwe. Isitoshe, Kabwe bado ni mchanga kisiasa. Umaarufu bandia unaomhangaisha ndio utakaommaliza.  Laiti angejiuliza ni kwanini magwiji kama Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta hawakuihama CCM zaidi ya kuwaponza akina Fred Mpendazoe waliowatanguliza kama Kabwe alivyowatanguliza akina Mwigamba na Dk. Kitila.
Walijua wakifanya hivyo watakwisha kisiasa. Hivyo, waliamua kupambana ndani kwa ndani. Hiki ndicho wanachofanya akina Edward Lowassa, Fredrick Sumaye na wengine walioonyesha kuutaka uongozi lakini wakashindwa kujiondoa kwenye chama chao hata kama ni bomu. Timing ni muhimu katika siasa. Timing ya ACT haionyeshi utaalamu wowote kimkakati.
Tumalize kwa nukuu tatu.Study the past if you would define the future.”  Confucius na “Never interrupt your enemy when he is making a mistake.” Napoleon, na“A wise man gets more use from his enemies than a fool from his friends.”  Baltasar Graci├ín, The Art of Worldly Wisdom.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 13, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Njaa mbaya sana
wanasiasa wa Bongo kama wachezaji mpira , hufuata maslahi, tujiulize kama wewe mpenzi wa simba hata ikifungwa miaka 200 bado utakuwa mpenzi wa Simba, lakini ukiwa mchezaji unahama kwenye maslahi
wote Njaa wao si wakombozi wa wanyonge
FUNGUKENI WATANZANIA
INASHANGAZA CHAMA HIKI KUPEWA USAJILI CHAPU CHAPU ILI KIUWE UPINZANI LAKINI 2015 WAPIGA KURA TU VIJANA TUMESOMA TUDANGANYIKI KWA PILAU,FULANA,WALA VITENGE TUNATAKA MAGEUZI BONGO TUMECHOKA TUMECHOKA NA KURA 2015 HAZIIBIKI NGO

NN Mhango said...

Anon usemayo kweli tupu. Je tutaendekeza njaa hadi lini wakati huwa haiishi?