Tuesday, 19 August 2014

Hizi tuzo zingine kwa Rais Kikwete hapana

HABARI iliyosambazwa kwa vyombo vya habari ni kwamba Rais Jakaya Kikwete amepewa tuzo nyingine ya The Icon of Democracy. Ni icon au agony of democracy? Ajabu!
Pamoja na wahusika kujisifu, ukichunguza sana unagundua kuwa nyuma ya tuzo hii kuna Wanigeria. Kulikoni? Je, kuna matapeli wanaomzunguka Kikwete na kusuka apewe upuuzi huu ili baadaye wahusika waje kumtumia baadaye kwa kumtoa upepo au kutafuta fursa na kuchukua kwa njia za uwekezaji uchwara kama ilivyokuwa kwenye tuzo nyingine ya kutia shaka ya The Most Impactful Leader of Africa iliyotolewa na Jarida lenye uhusiano na Wanigeria?
Kama Kikwete ni most impactful leader of Africa wale ambao ni truly most impactful watawekwa fungu gani? Je, huu si utapeli wa mchana? Maana tunaambiwa yupo Mwandishi wa habari ambaye pia ni pastor Elvis Ndubuisi Iruh kwenye tuzo ya sasa sawa na African Leadership Magazine ambalo makao yake makuu ni 13 Mambilla street, Off Aso Drive, Asokoro.P. O. Box 9824 Garki – Abuja, Nigeria.
Je, wahusika wanajua tabia ya Rais Kikwete ya kupenda sifa na kuthamini sana waandishi wa nje kuliko wa ndani? Je, Kikwete na walioridhia kupokea tuzo hii wanajua sifa za waliotoa tuzo husika?
Je, mamlaka zetu, badala ya kupokea na kuwapatia tuzo, zinafanya utafiti na kujiridhisha kuwa wanaotoa hizo tuzo wanafaa kufanya hivyo? Maana, ukiangalia kinachoitwa tuzo na walioitoa unapata walakini.
Hata jina la gazeti lenyewe shaka tupu ukiachia mbali mwenye kulimilki. Je, kwanini wapokeaji hawakujiuliza maswali muhimu kuhusiana na tuzo husika au ni kwa vile wanavishwa kilemba cha ukoko?
Je, kweli Kikwete ni Icon of Democracy (kielelezo cha demokrasia) au kinyume chake yaani Agony of Democracy?  Hawa hawajafanya utafiti. Kama wameufanya, wamemhadaa.
Pia, kutofanya utafiti ni ushahidi wa ukosefu wa uelewa wa wahusika. Ni bahati mbaya, hata wanaopokea wanatenda kosa hilo hilo. Si kila king’aacho ni dhahabu. Haiwezekani mtu aliyevuruga mchakato wa katiba mpya ukiachia mbali kutuhumiwa kuingia madaraka kwa fedha iliyonyakuliwa kwenye benki ya umma (EPA) asikanushe, akawa icon of democracy. Vinginevyo neno icon limepoteza maana kama si kumtapeli ili wahusika waje wamtumie baadaye.
Hata ukiangalia tuzo ya The most impactful leader haina maana kwa mtu ambaye impact yake kwa uongozi na kutokaa ofisini akitumia muda mwingi ughaibuni kwa shughuli ambazo zingeweza kufanywa na waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Rais Kikwete anawezaje kuwa icon of democracy wakati serikali yake inasifika kwa kutumia polisi kuwapiga hata kuwaua wapinzani na waandishi wa habari na watetezi wa haki za makundi.
Rejea mauaji ya watu watano kule Arusha kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mnamo Januari 2011, utesaji wa Dk. Steven Ulimboka hapo Juni 26, 2012 na kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda hapo Machi 5, 2013, kutaja kwa uchache bila kuongelea mauaji ya rejereja na mara kwa mara ya polisi ya watu wasio na hatia katika sehemu mbalimbali nchini.
Kwanini hawa kama si matapeli wa kawaida wa kinigeria, hawakuzingatia yote haya? Tuzo za Kikwete ni kashfa kwa Watanzania hasa wahanga wa utawala mbovu.
Rais Kikwete hawezi kuwa the most impactful leader au icon of democracy kwa madudu yote haya. Hapa hujaongelea ufisadi, uzembe, matumizi mabaya ya fedha za umma na kutotimiza ahadi alizotoa kwenye uchaguzi wa kidemokrasia. Hujaongelea uchakachuaji wa kura uliomwingiza madarakani kwa kipindi cha pili. Hujaongelea mbinu chafu zilizotumiwa na kundi lao la mtandao kuwachafua wenzake kwenye uchaguzi wa 2005 na matumizi mabaya ya fedha na vyombo vya habari.
Cha mno ni kutambua kuwa wanaompa nishani Rais Kikwete, licha ya kuwa matapeli wa Kinigeria, wanajua fika kuwa wanachofanya ni kutumia upenyo huo  kuficha utapeli wao unaolenga kumtumia kwa sasa au baadaye kujipatia nafasi kukamata rasilimali zetu.
Hebu jiulize, yuko wapi yule profesa kidhabu aliyeandika kitabu cha Kikwete kabla ya kugundulika kuwa kumbe ni kilaza anayedesa kazi za wenzake? Je, ilikuwaje washauri wa Kikwete hawakungundua kuwa mtu kama huyu mwenye usomi wa kutia shaka hakufaa kuandika kitabu cha Rais?
Hata hivyo, utamlaumu nani wakati Rais mwenyewe anasifika kwa kuwakingia na kuwateua watu waliotuhumiwa kughushi sifa za kitaaluma kama wale waliotamalaki kwenye baraza lake la mawaziri na wengine ubalozini?
Je, tumegeuka taifa la kitapeli au taifa la kutapeliwa kirahisi hata kwa kusifiwa uongo na upuuzi? Je, waliomshauri Kikwete kupokea tuzo hizi wanangoja nini ofisini iwapo itabainika watoa tuzo hizo si watu wa kuaminika?
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 20, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Makubwa haya Lakini Prof Lipumba alisema JK ni dhaifu kwani walisoma wote huo kikuu cha DSM
CCM ni mafisadi huchagua viongozi dhaifu ili waandelee kupeta sitoshangaa mgombea Urais toka CCM mwakani ni chagua la Mifisadi

NN Mhango said...

Anon usemayo ni kweli haswa ikizingatiwa kuwa Kikwete atabaki kwenye historia ya taifa letu kama rais bomu tuliyewahi kuwa naye. Mzururaji, mbabaishaji, msanii, mfujaji na asiyekuwa tayari kujifunza. Huyu jamaa ni balaa kwa taifa letu. Tuombe Mungu amalize ngwe yake na kutokomea huko aendako.