Friday, 15 August 2014

Hawa ni wabunge au wabuge?

          Taarifa kuwa wabunge wamekuwa wakiombaomba fedha kwenye mashirika kukidhi shida mbali mbali binafsi na za kisiasa zinawafanya waonekane kama wabuge badala ya wabunge. Kwanini mbunge ategemee kuomba wakati ana jimbo kubwa ambalo lina raslimali nyingi kuanzia watu hadi maliasili? Je nao wameathiriwa na mdudu wa kuombaomba kama serikali yao?
Aliyefichua uombaomba wa wabunge si mwingine bali mwenzao Tundu Lissu aliyekaririwa akiliambia bunge, “Sifa hizi zina sababu yake. Kuna nyaraka na barua zinazoonyesha wabunge mbalimbali waliochukua fedha za mifuko hii kwa sababu mbalimbali.” Baada ya Lissu kulipua bomu hili alishambuliwa na wahusika hata kwa matusi ya nguoni badala ya kupinga madai aliyotoa.
Lissu aliongeza, “Unaweza ukajiuliza maswali mengi. Wizara inaomba fedha katika mfuko wa jamii ili kununua kompyuta na vifaa vingine vya ofisi wakati ina bajeti ya ununuaji wa vifaa hivyo.
Inatisha. Wabunge waliotuhumiwa kuombaomba toka kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao waliusifia kwenye michango yao bungeni kama kulipa fadhili.
 Waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi).
Hapa tunaongelea wabunge wanaoomba pesa kwenye mashirika. Je ni wangapi wanaomba pesa kwa wawekezaji kiasi cha wawekezaji kugeuka miungu kama ilivyotokea kule Mara ambapo mgodi wa dhahabu unaendelea kuwaumiza wananchi wa kule bila serikali kuchukua hatua?
Hivi waziri anapogeuka ombaomba unategemea atatenda haki pale anapojikuta akipambana na shirika linalomfadhili? Jibu analo Lissu aliyekaririwa akisema, Hali hii inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia Serikali na taasisi zake.” Haya mashirika si wajinga. Wanatoa fedha kwa wabunge wakitegemea kuwatumia. Maana hakuna cha bure duniani tunapongea kiuchumi. Ukitaka kuona huu ukweli hebu jiulize: Inakuwaje shirika kama NSSF kutoa pesa kwa wanasiasa wakati wanaochangia mfuko huo wakizungushwa kupata mafao na michango yao kama hakuna biashara nyuma ya pazia? Kuonyesha baadhi ya wabunge wetu walivyogeuka wabuge, mmojawapo, Machangu alikaririwa akijitetea kwa kutoa majibu ya kibugebuge aliposema, “Ni muongo kabisa (Lissu) yeye inamhusu nini hiyo?”  Huyu hata kama ameingia kwa tiketi ya kupendelewa hafai. Anauliza eti yanamhusu nini Lissu wakati akishuhudia heshima ya bunge ikishuka tokana na upogo na uroho? Yanamhusuje wakati kazi yake kama mbunge wa upinzani ni kuisaidia serikali kurejea kwenye mstari? Huyu kweli ni mbunge au mbuge asiyejua hata mambo mepesi kama haya wala wajibu wake?
Mwingine aliyethibitisha waheshimiwa hawa walivyogeuka wabuge ni Lusinde aliyekaririwa akisema, “Fedha hizo tumeshapata na pia tuliomba nyingine katika Kiwanda cha Saruji cha Wazo bado hatujapata.” Mbunge kama huyu anayetegemea kufadhiliwa na kiwanda kama Wazo Hill anaweza kusimamia haki za wananchi wa maeneo hayo wanalalamikia kiwanda husika kuchukua maeneo yao ya ardhi au kuchafua mazingira wakati alishalishwa ubuge?
Trumegeuka taifa la hovyo sana. Taifa la ajabu la maombaomba wakati mali tunayo ila tumeikalia. Rais anakesha kwenye ndege akienda ughaibuni kuomba huku akishindwa kurejesha fedha zilizofichwa Uswizi. Waziri naye anaomba bila kumsahau mbunge. Je namna hii tutafika? Tunakuwa kama hayawani kuomba kile ambacho tuna uwezo wa kuzalisha kama tutaamua kutumia akili sawa sawa!
Ni bahati mbaya sana kuwa baadhi ya watuhumiwa wamejitahidi kugeuza tuhuma za uombaomba kuwa za kisiasa wakati kimsingi ni za kimaadili. Huu ni ushahidi kuwa madili yamechukua nafasi ya maadili kiasi cha wabunge wetu kugeuka wapiga madili badala ya kusimamia maadili ambayo kimsingi, ndiyo yangewawezesha kuwanufaisha wale waliowachagua. Hatuwezi kufika kwa mfumo huu wa kila mtu kujihudumia kwa njia safi na chafu. Hatuwezi hata kidogo. Tukiweza tutaangamia kama jamii na taifa kutokana na upogo na uroho wa baadhi yetu wanaotaka kuhalalisha haramu. Uombaomba si kitu kizuri hata kama kinafanywa na watu wenye madaraka makubwa kama rais wabunge na mawaziri. Kinachopaswa kufanyika si kuupenda bali kupambana nao kwa njia ya kujitegemea na kupambana na ufisadi na sera za kibabaishaji.
Ombaomba ni ombaomba hata akivaa suti au kuitwa mheshimiwa au rais na makorokoro mengine. Uomba omba ni udhalilishaji na ukorokocho.
Leo hatusemi mengi. Badala ya wabunge wetu kujigeuza wabuge na kuchukia kila anayewakosoa au kupinga udhalili huu wa kujitakia, wabadilike na kuwa wabunifu kwenye majimbo yao kiasi cha kuweza kujijengea heshima. Kuomba hakuwezi kutatua matatizo ya wahusika zaidi ya kuwadhalilisha na kuwafanya watumwa wa wale wanaowafadhili. Kimsingi, wabunge wetu wachukie na kuepuka kuwa wabuge yaani wapenda udoho udoho au vitu visivyolingana na hadhi yao.
Chanzo: Dira Agosti 2014.

No comments: