Saturday, 16 August 2014

Kidato cha sita ni ushindi au ushinde?


 
          Japo habari za watahiniwa wa kidato cha sita mwaka wa elimu 2013/14 kushinda kwa asilimia 95.98 zimefurahisha wengi, zinaacha maswali mengi kuliko majibu.  Haijawahi kutokea nchini kiwango kama hiki cha ushindi kufikiwa. Inashangaza ni kwanani wanafunzi wamefanya vizuri wakati hali ya elimu ikiwa hoi nchini? Nini kiliongezeka kuboresha elimu kiasi cha kustahili ushindi huu mnono? Je kuna namna hasa ikizingatiwa madudu yaliyofanywa mwaka jana kiasi cha kidato cha nne karibia wote kufutiwa matokeo na kuanzisha madaraja mapya yaliyoonyesha kuwa suluhu kisiasa lakini si kitaaluma? Ni muujiza gani umefanyika kufikia kiwango hiki? Muulizeni waziri husika Shukuru Kawambwa kafanya miujiza gani kutoka kwenye kufeli ghafla bin vu kwenda kwenye kushinda kwa kiwango kikubwa hivi. Kumbuka.  Mwakani kuna uchaguzi mkuu. Hivyo, siasa haichezi mbali kiasi cha kuweza kufanyika uchakachuaji na ushenzi mwingine ili watawala waonekane wanafanya mambo waliyoahidi wakati ni bomu tu. Bila maelezo ya kwanini watahiniwa wa kidato cha sita mwaka 2013/2014 washinde kiasi hicho ambacho hakijawahji kutokea tujue hakuna namna.
Mwaka 2011 matokeo ya kidato cha sita yalionyesha kuwa  kiwango cha ufaulu kiliongozeka kwa  nukta 36  tu kutoka 87.24 mwaka 2010 jana hadi 87.58 mwaka 2011. Kwa lugha rahisi ni kwamba ufaulu kati ya mwaka 2010 na 2011 uliongezeka chini ya asilimia moja. Hili ni jambo la kawaida na linaweza kupewa maelezo ya kina likakubalika bila kuzua shaka kama ilivyo kwa matokeo ya mwaka huu.
Mwaka 2009 kiwango cha ufaulu kiliongezekwa kwa aslimia 1.65 ikilinganishwa na mwaka 2008. Ni rahisi kufuatilia mtiririko wa ufaulu wa matokeo kila mwaka. Hata ukifuatilia ufaulu kuanzia mwaka 2000 hadi 2012 utagundua kuwa ufaulu haujawahi kuchumpa kama ilivyotokea mwaka huu bila maelezo.
Ifahamike kuwa kuhoji matokeo haya hakumaanishi kuwa watahiniwa hawawezi kushinda. Hasha. Lazima kuwa na sababu ya kufanya hivyo. Haiwezekani kuchumpa toka asilimia 87.85 za mwaka jana hadi asilimia 95.98 mwaka huu bila kuwa na namna au uboreshaji wa elimu au mchezo mchafu wa kupanga matokeo ili kukidhi matakwa ya watu au chama fulani kisiasa. Lazima hapa yatolewe maelezo ya kina na yanaoingia akilini kitaalamu. Vinginevyo ushindi huu unaweza kuwa kiini macho cha kuwafanya wahusika wanaosifika kuua elimu yetu waonekane wanachapa kazi wakati si kweli. Maana, asilimia 8.13iliyoongezeka haiwezi kukosa maelezo kitaalamu. Kama hakuna maelezo na ushindi tajwa haupo. Kwani bila maelezo ya kitaalamu basi kutakuwa na mambo yanayofichwa kutokana na ukweli kuwa yataakisi mchezo mchafu au kuchezea mfumo wa usahihishaji hata upangaji madaraja. Ongezeko la asilimia nane na ushei si mchezo na haliwezi kukubalika bila maelezo ya kitaalamu na yanayoingia akilini. Hivyo, badala ya kushangilia ushindi huu wa kutia shaka tuhoji nini kimefanyika ili kitusaidie kuepuka kushindwa kila mwaka. Bila hivyo, haya matokeo na ni kuchezewa mahepe. Je kinachoitwa ufaulu wa juu kipo au ni mahepe? Waziri kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Susan Lyimo (CHADEMA) anatoa jibu akisema, “Hapo kinachooneka goli limepanuliwa ili magoli yaingie zaidi kwani kati ya mwaka jana na mwaka huu kitu gani kimefanyika. Ukaguzi wa walimu na wanafunzi haufanyiki, ufaulu unaongezekaje?”
Nijuacho ni kwamba kama hatutahoji na kupata majibu, wanasiasa wetu wataanza kujipiga vifua wakigeuza ushindi huu wa mashaka kuwa sera yao kwenye uchaguzi ujao. Watafanya hivyo wakijua fika kuwa ni uongo ila kwa vile wana haja ya kushinda kwa njia yoyote hawatajali kuwaambia wananchi uongo wa mchana kweupe. Tunamtaka waziri husika atoe taarifa ya ufanisi huu wa kimbunga ambao si kawaida na kama umewezekana lazima kuwepo sababu na maelezo ya kitaaluma.
Kitu kingine kinachoweza kutustua ni ile hali ya shule zisotegemewa kushinda zaidi ya zile zilizotegemewa. Hata hizi zilizotegemewa ambazo nyingi ni za binafsi zinapaswa kuchunguzwa kuona ni nini wanafanya hadi kufikia ushindi huu. Lazima tujiulize ni kwanini shule binafsi zinashinda kuliko shule za umma ili tuweze kuboresha shule hizi zinazotafuna kodi nyingi ya umma ukiachia mbali kuwa tegemeo la wengi wasio nacho.  Hali hii ya ushindi wa shule binafsi inatukumbusha shule moja ya binafsi iliyofungiwa jijini Dar es salaam iliyokuwa inasifika kwa kuongoza kwenye mtihani. Baada ya kufanya uchunguzi iligunduliwa kuwa ilikuwa inawapa majibu watoto ili washinde sana na kukuza soko lake. Je mchezo huu umeisha? Je ni shule ngapi zinazotafuta soko kwa njia zozote ziwe chafu au safi? Je mfumo wetu wa hovyo wa elimu usio na ukaguzi wa kutosha, unaoruhusu wahusika serikali kuwa na shule zao binafsi unalikwepa hili?
Huwezi kupanda majani ukavuna chai. Hivyo, ushindi huu ulioonekana kushangiliwa sana na vyombo vya habari haujakamilika bila maelezo. Tumewekeza nini na kiasi gani kwenye elimu tangu mwaka jana hadi tustahili ushindi huu?
Tumalizie kwa kutoa mwito kwa wadau wa elimu kuchunguza ufaulu huu usio na maelezo. Hatutegemei kuambiwa kuwa mfumo ulioanzishwa hivi karibuni wa Big Results Now ndiyo sababu ya muujiza huu. Haiwezekani mfumo ulioanzishwa juzi utoe matunda haraka hivi vinginevyo uwe umeanzishwa kufunika vitu kama hivi visivyo na maelezo ya kina.
Chanzo: Dira Agosti 2014.

2 comments:

Anonymous said...

mtapasisha sana kwa ajili ya uchaguzi mwakani
lakini Mbatia alisema kweli
na nimtu mkweli tangu enzi za baba yake Nape Korea walipingana
Mbatia anajua mengi bongo akifunguka
watakuwa hapatoshi bongo
lakini wabongo waoga angaliani usa now

NN Mhango said...

Anon usemayo yana mashiko. Je wapiga kura wataendelea kukiamini chama angamizi wakati wao ni wahanga? Tieni akilini.