Tuesday, 26 August 2014

Kijiwe kwenda kufunga bunge la Katiba

 Baaada ya wasaka tonge wakubwa na wadogo kujifanya kuwa hawana uwezo wa kusitisha Bunge Maalum la Katiba (BMK) lakini bado wakawa na mshipa wa kutuibia kwa kujilipa laki tatu kwa siku kwa kuharibu kila kitu, Kijiwe kimedhamiria kuwakomboa wachovu kwa kulifunga bunge husika. Nani anataka bunge-duka la wasaka tonge na wachumia tumbo kujitajirishana huku tukiendelea kusikinishwa?
Leo ni Msomi Mkatatamaa analianzisha. Anavuta kombe lake la tangawizi na kubwia kidogo na kuzoza, “Waheshimiwa, hali ilivyo ni kwamba tunaendelea kuibiwa na wasaka tonge na wachumia tumbo kwa kisingizio cha kuandika Katiba Mpya ambayo si mpya kitu bali mizengwe ya Chama Cha Mafisadi (CCM). Je mna mawazo gani kuhusiana na kuzuia wizi huu wa mchana uliofichwa kwenye mchakato?”
Mijjinga anadaikia hoja na kusema, “Yaani vipande thelathini vinaangamiza Kaya yetu kirahisi hivi! Je tutamlaumu nani iwapo tuna uwezo wa kuzuia jinai hii kwa kushinikiza kigwena hiki cha ulaji na wizi wa njuluku zetu kisitishwe mara moja?”
“Tiende Dodomya tikawatie adabu na kuwadai uchache wetu wanaopeana wakijua fika wanafanya utoto na Katiba haitapatikana. Haiwezekani tiendeee kuwa mashahidi wa maangamizi yetu. Je mnasemaje wakubwa?”
Mipawa anadakia na kusema, “Mlisikia ya Njaa Kaya kujifanya kuwa hana uwezo wa kuvunja hili buge la ubuge ubuge wa laki tatu zinazoangamisha kaya yetu?"
Kapende anajibu bila kungoja Mipawa aendelee kudema, “Ujinga mtupu. Kwanini aweze kuliunda ashindwe kulivunja kama si sanaa na rongorongo? Who’s fooling who hither guys?”
Mpemba aliyekuwa ndiyo anamaliza kuweka tasbihi yake mfukoni anakatua mic, “Kama hawezi livunja basi atuache sie tumsaidie kulivunja kwa vile ndiyo wahanga wa wizi huu wa nchana. Kama anamaanisha asemacho wallahi lazima tulivunje na asitutumie ndata kutubwenga kwa vile hana ubavu nalo lakini sisi tunao. Nshachoka na mchecheto wao waniouita nchakato. Nchakato gani  wa kutuibia?”
Mheshimiwa Bwege, akiwa anamaliza kipisi chake cha sigara kali, anauma mic, “Hivi haya mabilioni wanayohonga kuvuruga mchakato na kupitia upuuzi wao yangesomesha vijana au kutibia wagonjwa wangapi? Huu ulafi na roho mbaya vinamsaidia nani kama siyo kuongeza mzigo kwa mlipa kodi maskini wanayemhujumu na kumuibia kila siku?”
“Kaka unaongelea kusomesha na kutibia wakati walafi haya hayawahangaishi! Wasomeshe nani wakati vitegemezi vyao  hata vya mahawara zao vinasoma ughaibuni huku nao wakibitiwa na hata kuangalia afya zao huko huko? Hakuna anayejali kaya wala wanakaya bali tumbo lake na tamaa zake walaani hawa.” Anajibu Mijjinga huku akibonyeza kisimu chake kusoma sms aliyotumiwa na kidosho wake.
Msomi akiwa anakuna kichwa ili kutoa mapwenti anakula mic tena, “Jamani hakuna kitu kinanitia kichefu chefu kama huu usanii unaoitwa mchakato. Huu si mchakato bali mchakamchaka wa kutuibia njuluku zetu.  Ukitaka kujua jinsi huu mchakato ulivyo mchecheto kama alivyosema Ami hebu angalia wanavyomsakama jaji Waryuba. Heathy minds discuss issues while sick one discuss personality. Badala ya kujadili rasimu ya Waryuba, wameshikilia kumsingizia na kumtukana utadhani alijiteua.”
Anakunywa tangawizi yake na kuendelea, “Hakuna sehemu jamaa ameonyesha uhovyo na uchovu kama hapa. Unaunda tume tena bila kulazimishwa halafu unaigeuka na kuanza kuikashfu na kuisingizia? Ukisikia kuishiwa na ukilaza ndiyo hivi. Kama hana haja ya kuandika katiba mpya basi avunje genge lake ili wakati muafaka utapowadia iandikwe hata kama ni baada yay eye kutimka mwana kutimka akatokomee kwenye kaburi la sahau.”
Maneno ya Msomi hayajamfurahisha bi Sofi Lion aka Kanungaembe. Kwa usongo anakatua mic, “Mie nasema Katiba Mpya itaandikwa. Sema nyie hamna shukrani wala subira. Badala ya kumpongeza mkuu kwa kuwapa fursa ya kuandika Katiba Mpya mnamuandama kwa mitusi. Je mitusi yenu ndiyo itaandika Katiba?”
Kabla ya Sofi kuendelea, mshikaji wake Kanji anakatua mic, “Sofi ambia yeye ijue. Kuu naunda chakato ya Katiba. Kwanini vatu nakuwa gumu kuelewa simple things like these.”
Mbwa Mwitu aliyekuwa akinong’ona jambo na mzee Maneno anakula mic, “Kanji unamdanganya nani? Kwani hiyo Katiba ni mali ya kuu au mali ya lalahoi yote? Sofi anasema tumpongeze. Loo! Tumpongeze kwa ujinga na kutuhujumu siyo au anataka tumpe tuzo ya kuhujumu Katiba?”
Mgosi Machungi hangoji Mbwamwitu amalizie, “Kaka imeongea kitu muhimu sana. Hatiwezi kumpongeza kwa ujinga na hujuma kama hii ya kutiibia njuuku. Kama akitaka pongezi aende huko kwenye genge lake wanakopongezana kwa kia upuuzi au awambie waniigeia wampe nyingine.”
Mpemba anakamua tena, “Mie naona tuache kulalamika ati. Twende kule Dodomya kama alivosema Ngosi tukaukate nzizi wa fitina ati.sijui mwasemaje?”
Msomi anamjibu Ami haraka haraka, “Hapa kaka umenena. Tuache kulalamika. Badala yake twende kule tukawatie adabu. Maana hii pesa wanayozawadiana kupitisha ujinga ni mali yetu na si yao. Na hata hiyo Katiba ni mali yetu. Tangu lini punda akahofia kutua mzigo?”
Ukiondoa Sofi na Kanji, Kijiwe kizima kinaazimia kwenda Dodomya kufunga bunge ili kuokoa njuluku za umma.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 27, 2014.

No comments: