Wednesday, 20 August 2014

Tunapofundishwa Kiswahili na wasiokijua


          Hakuna ubishi. Kiswahili chimbuko lake ni Tanzania ingawa hali ilivyo, Tanzania itaanza kufundishiwa Kiswahili tena kibovu tokana na kuvuruga mfumo wake wa elimu. Tanzania, kama taifa, tumeanza kupoteza umakini kwa kiwango kikubwa. Wengi walitegemea tungenufaika na kuwa wenye lugha ya Kiswahili. Lakini wapi. Badala yake wanaonufaika na lugha hii adhimu inayopanuka kwa kasi barani Afrika na ulimwengu mzima si wengine bali wanafunzi wetu. Ukiachia mbali uzembe tulioonyesha kwenye nyanja za uongozi hata elimu na kujitambua, tumeonyesha aina nyingine ya uzembe ambapo tunapwakia kila kinachokuja kwetu bila kufikiri wala kuhoji.
Nani alitegemea kuwa Tanzania ingefundishwa au kuridhia kutumia Kiswahili kibovu au cha kupotoshwa? Hili kwa sasa ni dhahiri na halina ubishi na wala hakuna anayekereka nalo kiasi cha kuchukua hatua mujarabu.
Leo tutataoa mifano michache ya kuonyesha jinsi nchi ambayo ndiyo chimbuko la Kiswahili inavyofundishwa na wanafunzi wake tena maneno yaliyokosewa. Leo tutaongelea baadhi ya maneno tunayotumia vibaya kana kwamba hatuna maneno sahihi kwa dhana husika.
Hivi karibuni maneno ufisadi, fisadi na mafisadi yamesikika sana. Yamekuwa kile kwa kiingereza huitwa buzzwords yaani maneno yanayotumika sana kiasi cha kuwa kama fasheni. Kila unaposoma au kusikiliza vipindi redioni utasikia mafisadi, ufisadi au fisadi yakitumika kwa makosa kumaanisha kile kinachopaswa kuwa wahujumu, uhujumu na mhujumu kama tutatumia Kiswahili sahihi.
Ingawa neno fisadi ni la Kiswahili, halimaanishi wakosefu wa maadili kiuchumi bali kimahusiano. Na kama likitumika kumaanisha ukosefu wa maadili humaanisha watapanyaji na si wezi wanaoiba na kuficha au kutumia kwa anasa na matumizi mengine yasiyo utapanyaji. Fisadi kwa Kiswahili sahihi humaanisha mtu mchonganishi au mfujaji lakini si mwizi. Mtu wa karibu na fisadi ni mfitini anayeweza kufitini na kufitinisha watu sawa na fisadi ambaye ni mtu mwovu mwenye kufisidi na kugombanisha watu hasa wenye uhusiano mzuri akisikumwa na roho mbaya au wivu au kijicho. Ukiangalia maana halisi ya fisadi, unashangaa kugundua ni kwanini wahujumu hata wala rushwa wakaitwa mafisadi. Je wanamfisidi nani wakati wanachofanya ni kuhujumu au kumwibia fulani?
Ukiachia mbali neno fisadi, kuna dhana nyingine inakosewa sana. Dhana hiini kuhusiana na ajira. Kiswahili sahihi tunasema fulani ameajiriwa. Wenzetu ambao Kiswahili si lugha yao wanasema fulani kaandikwa kazi. Haileti maana zaidi ya kulazimisha dhana nzima. Hata ukiangalia historia ya ajira ya mswahili, utakuta kuajiriana mara nyingi kulihusisha vibarua mashambani ambako kila muajiriwa alipewa ngwe yake na kuifanya. Ajira hii haikuhitaji wala haikuwa na kuandikana hasa ikichukuliwa kuwa yalikuwa maridhiano na makubaliano ya watu wanaofahamiana na wengi wao wasiojua kusoma na kuandika. Sasa hii kumwandika mtu kazi imetoka wapi? Wenye kufahamu wanaweza kutuelimisha lau tujue na kujadili zaidi dhana hii tuone matumizi yake sahihi.
Dhana ya ajira haiishii kwenye kuandikwa bali inakwenda hadi kuleta dhana nyingine ambayo ni kufutwa kazi. Kwa vile aliyeajiriwa, kwa mujibu wa Kiswahili cha wenzetu ameandikwa basi kuachishwa kazi kwao ni kufutwa kazi. Kwa mswahili haswa mwenye kuimanya na kuitumia vizuri lugha ya Kiswahili mtu anaposita au kusitishwa kazi ima awe amestaafishwa au kuachishwa au kufukuzwa kazi. Hakuna cha kufutwa wala kuandikwa bali kuajiriwa na kufukuzwa kazi au kuachishwa ajira. Hii ni mifano tu. Yapo maneno mengi ambayo ima yanatumika kimakosa au yametengezwa na wenzetu kwa vile sisi hatuwezi. Mfano ni maneno kama runinga, rununu, na rukono yakimaanisha televisheni na simu ya kiganjani mtawalia. Je sisi hatuwezi kutengeza yetu mfano badala ya kutumia runinga tukasema kabapicha yaani kabati ya picha au pichambali? Ni mfano tu.
Pamoja na Kiswahili kuwa na historia ndefu na mfumo mzuri, bado waswahili wale wale wenye asili ya lugha yenyewe wamegeuka wazembe kiasi cha kufundishwa lugha potofu wakati walipaswa kutoa muongozo wa nini ni sahihi na nini si sahihi.
Je ni kwanini Tanzania imefikia hatua mbaya ya kufundishwa Kiswahili kwa mfano na Kenya? Japo jibu la swali hili ni refu sana, kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa chanzo kizuri ni kuvurugwa na kuuawa kwa mfumo wetu wa elimu ambao unazalisha ima wasomi wasioiva kiasi cha kufikiri na kudurusu na kuandika mambo au wasiojua dhima nzima ya jukumu lao kama wasomi. Kutokana na hali hii ambayo imechangiwa na uhujumu kulhali katika kila nyanza, wasomi wamegeuzwa watu wa kufukuzia pesa hata kama ni kwa kutelekeza taaluma zao au kuziuza kwa yeyote ambaye anaweza kuzitumia atakavyo. Ndiyo maana tuna maprofesa wengi wanasiasa kuliko wana taaluma.
Baya zaidi, maprofesa au madaktari hawa tunategemea wawe wameelimika, wanapopewa nyadhifa huvurunda karibu kila kitu. Leo tutatoa mfano kwa profesa mmoja aliyewahi kuwa waziri wa elimu akaivuruga. Huyu si mwingine ni Jumanne Maghembe ambaye chini ya uongozi wake elimu yetu ilizidi kuporomoka hadi alipokuja mwingine daktari Shukuru Kawambwa akaimalizia kabisa. Huu ni baadhi ya ushahidi kuwa baadhi ya wasomi wetu ni kama hawakuelimika.
Imefikia mahali Tanzania tunaingiza vitabu feki na visivyofikia kiwango kwenye mitaala yetu kwa vile waliovitunga wamepiga ‘dili’ na wakubwa wanaoamua nini kufindishwe na nini kisifundishwe. Mfano mwingine wa haraka ni pale ambapo taifa linakuwa na ukame wa vitabu vilivyotungwa kisomi na kisanii.  Badala ya wahusika kuangalia ubora wa kitabu wanaangalia namna ya kuingiza vile vinavyoweza kuwapitia chai yao. Je namna hii tutafika ambapo tumefikia kufundishwa Kiswahili potofu na kibovu na wanaopaswa kuja kujifunza toka kwetu?  Basi tubadilike kabla hatujawa wakimbizi na wafungwa wa kila kitu kwenye taifa letu hasa ikizingatiwa kuwa nyanja karibu zote zimehujumiwa.
Chanzo: Dira 

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hii ningependa wengi wasoma maa waTanzania tumejifunga, hatujafunguka yaani kwetu kila kitu tunakubaliana tu ...tutakipoteza kiswahili chetu hivi hivi....

NN Mhango said...

Da Yacinta usemayo ni kweli tupu. Tumejifungia bila kujua jinsi ya kufunguka tokana na uongozi mbovu na wa kinyemelezi. Wameua elimu kwa vile wanasomesha watoto wao nje. Wameua afya kwa vile wanaangalia afya zao hata kutibiwa nje. Wamesahau kuwa bila ya jamii iliyoelimika tutaendelea kuachwa nyuma nao wakiwa miongoni mwa waathirika wa hujuma yao.

Anonymous said...

Tatizo la Tanzania viongozi kuannzia rais wanaouna ujiko kuongea kigeereza tean cha kusuwa suwa
rais wa norway , ujerumani, ufaransa
wote huongea kwa lugha zao kwani ndo walipa kodi lazima wajue live kiongozi kangoea nini
cha kushangaza kiswahili kinafundishwa dunia nzima uliza walimu wanatoka wapi , Ghana, kenya,
toba toba

NN Mhango said...

Anon umenena. Tatizo la walio wengi ni kutojiamini na kudhani kuwa kujua kiingereza ndiyo kusoma,ajabu wengi hata hawakijui vizuri.