Saturday, 25 June 2016

Dk Makufuli lazima uwatumbue akina Nkapa na wenzake


            Juzi nilinusurika kujinyotoa roho. Si pale nilipokwenda kwenye kongamano na Kigoda cha Mwl Nchonga. Nikiwa nimepiga pamba zangu bila bangi na gongo nimejipendezea tu si kidhabu mmoja aitwaye Big Ben Nkapa akanichefua nusu ninyanyuke na kufanya kitu mbaya kama si kumheshimu marehemu Mchongo (Bwana God Amuwekee Patamu) stori ingekuwa nyingine. Wakati sisi tukilewa mma, wajivuni wanalewa madaraka na kujisahau wakidhani tumesahau uchafu wao. Bila chembe ya aibu wala utu wanatuomba msamaha.  Sisi hatuombi msamaha kuwasulubu na kuwatumbua.
Kuna kipindi nilishindwa kujizui kusikiliza porojo na upuuzi kiasi cha kutaka kumkichaka Ben kama yule jamaa wa kwa Saddam aliyefanya shambulizi la kiatu. Ilibidi nijizuie; kwa vile hiyo si jadi ya walevi ambao jadi yao ni kufanya kweli bila kujali nini kitatokea. Anyway, shetani na Ben washindwe.
 Leo nataka namtumia kidhabu huyu na wajivuni na wezi wenzake; waache kututia madole vinginevyo tunaweza kuamua kama mbwai mbwai. Wanadhani tumesahau walivyochomoa njuluku na mimali yetu? Tuliwaminyia; sasa wanatutia madole kana kwamba hatunayo ya kuwatia? Hivi Ben anadhani tumesahau yeye na marafiki na kaya yake walivyokwapua Kiwila? Anadhani walevi wameishasahau au kusamehe alivyopiga mnada Banki Biyashara aliyotupa kihasara kwa makaburu wenzake?
Kama Big Ben ana kumbukumbu ndogo au hana kabisa, asidhani walevi ni wasahaulifu na mabunga kiasi hicho. We still vividly remember how he robbed us. He must stop kvelling. Samahani. Nimechukia hadi kikameruni kinanitoka bila kujua wala kuhiari.
Sijui kwanini Ben hataki kukubali kuwa hana power tena na tukimbana Dk Kanywaji anaweza kutumbuliwa wakati wowote? Sasa ajue; nitahamasisha walevi na michupa yao kuingia mitaani kuhakikisha Ben, Njaa Kaya na mzee Ruxa wanashikwa na kutupwa lupango ili wachunguzwe.
Hivi huyu anadhani walevi wameishasahau HEPA yake na Njaa Kaya? Pamoja na ulevi wetu, bado tunajua kuwa HEPA iliasisiwa na Nkapa, Mangulangula, Njaa Kaya na Pita Noni ili kushinda kwenye uchakachuaji. Tunajua walioshirikiana na Net Problems Group iliyopewa kuua Tanisco waliletwa na makampuni ya shemeji za Ben baada ya nkewe bi Anna Tamaa kumzidi kete. Yethu, unafanya mchezo na mbesha! Rua, Ben tafadhali usinifanye niape kwa majina ya miungi wakali wakamnyotoa roho hata kabla hajakanyaga Keko au Ukonga.
Kwanini Ben hataki kukumbuka kuwa hata mijengo yetu aliyojitwalia yeye na wenzake bado tunaitaka na kuikumbuka? Ngoja Dk Kanywaji apate rungu la pili amtumbulie mbali. Lazima mijengo yetu irejeshwe na Ben na wenzake watumbuliwe tena kavu kavu. Utaachaje watu waliotumia akili uchwara kuibia kaya? Utaachaje wavivu wa kufikiri waibie kaya halafu waendelee kuwakonga walevi  nawe udai unapambana kwa ajili ya kuwaletea maisha bora na kubadili kaya?
Kwanini Ben anasahau kuwa walevi walitaka asulubiwe muda mrefu ila Njaa Kaya akamkingia kifua akiwa Sweden ambako nami nilikuwa nimealikwa kutoa mhadhara juu ya faida ulevi wa usawa ambapo wanawake na warume hunywa pamoja bila kupigana wala kukwaruzana.
Hivi kwanini Ben anusurike wakati washirika zake kama Dan son of Jonah na Pesambilimbili Mrambaramba walishapatikana na hatia kwa makosa waliyotenda wakiongozwa na Ben huyu huyu? Hakuna sehemu alituboa walevi kama kutuasa tuchape kazi kwa bidii wao waibe na kula kwa bidii. Eti li jiBen lilisema tusiulize kaya imetutendea nini bali tumeitendea nini! Lenyewe–zaidi ya kuiibia kaya–liliifanyia nini? Ama kweli nyani haoni nonihino lake. We ngoja walevi waendelee kuchukia uone tutakavyofanya kweli pakawa hapakaliki. Basi kama Ben anadhani walevi wamemsahau au wanamuogopa, anajidanganya. Rejesha mijengo yetu badala ya kuleta rongorongo uchwara. Mwizi ni mwizi hata aitwe mheshimiwa.
Mbali na Ben kutusisitiza tuchape mzigo yeye ahomole atakavyo, aliwashambulia waandishi wa umbea kuwa hawajui kufanya uchambuzi. Aliongeza kuwa wanalalamika badala ya kushauri. Umshauri nani wakati ukifanya hivyo, gendaeka linakwambia u mvivu wa kufikiri? Ungelishaurije jitu lenye kujitiatia na kujua kila kitu japo sasa limeisha na kuishiwa? Ben alinasema eti watu hawajui kufanya analysis kana kwamba yeye anajua. Huo ugwiji wa analysis wa Ben uko wapi iwapo kila alichofanya ni hovyo? Hata alivyoongea hakuonyesha chembe ya utafiti wala uchambuzi anaotaka wengine waujue. Unawezaje kusema walevi wote hawajui kuongea kana kwamba umeongea nao wote halafu uitwe pumba zako uchambuzi? There’s no sacregious sin in research like generalization that Ben made. Ohooo! Nisameheni. Kila ninapochemka kikameruni kinamwagika chenyewe.
Kama Ben hatafunga domo lake, atanifanya niingie mtaani na kwenda moja kwa moja Magogoni kuhahakikisha anatumbuliwa tena chap chap na kavu kavu. Apange jinsi ya kurejesha njuluku zetu, mijengo yetu, Kiwila na kunyea debe badala ya kuleta ngebe. Kwa taarifa yake, hata nkewe tunachunguza ili atumbuliwe. Hata ntangulizi wake na aliyenrithi wote tutawatumbua tu. Sijui nani anawapa kiburi wajivuni hawa hadi wakajilisha pepo wakati wana kongwa shingoni mwao? Shame on them all! Rejesheni njuluku na mali mlizotuibia badala ya kututisha na kutuhubiri upuuzi wa kuomba misamaha ya kisanii na kimagamba wakati nyinyi ni majipu na magamba yanayotucheka na kutuzomea kimoyomoyo.
Kwa vile nimechonga sana, nahisi kiu kiasi cha kuhitaji msokoto na kachupa ka gongo lau nipoze hasira nisijekwenda kufanyia gendaeka kitu mbaya.
Chanzo: Nipashe Jumamosi.

No comments: