Saturday, 18 June 2016

Magufuli tumbua hata vilaza wazito

William Lukuvi cropped.pngDiodorus Kamala (12746453754) (cropped).jpgRIO DE JANEIRO - JUNE 13: The Humanidade Event on June 13, 2012 in Rio de Janeiro ,Brazil - stock photoMary Nagu.jpgImage result of saada mkuya
          Akiweka jiwe la msingi la maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli alisikika akilaumu kitendo cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kudahili watu wasio na sifa ambao aliwaita vilaza akimaanisha wasio na uwezo mkubwa kiakili.
            Katika hotuba yake ya takriban saa nzima, Magufuli aliimwagia sifa lukuki UDSM akisema kuwa imedahili vipanga akimaanisha watu wenye akili zinazochemka ingawa hili nalo linatia shaka hasa ikizingatiwa kuwa madudu na rushwa na upendeleo vimo katika idara nyingi na karibia kila sehemu nchini. Sijui kama kweli waliodahiliwa na kujiunga na UDSM ni vipanga watupu.
            Magufuli alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Una D, D unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa serikali, ni aibu ya ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani.” Magufuli alionyeshwa kukasirishwa na kashfa hii; na kusisitiza kuwa asingeweza kuvumilia madudu kama haya.
            Aliongeza, “Lakini wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D, D manaake wengine ni divisheni 4, kuchukua digrii, wapo wanafunzi wengine wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wapo wanafunzi wengine walio na diploma wamekosa mikopo.” Huu ni ushahidi kuwa kuna watu wenye sifa hawakuwezeshwa kujiunga na vyuo vikuu wakati wasio na sifa wakiwezeshwa. Ndiyo maana tunasema; hatujui kama UDSM haina vilaza hata kama si wengi kama waliogunduliwa UDOM.
            Baada ya kufichuka kashfa hii, tunapaswa tujiulize maswali magumu kidogo na kuyapatia majibu sahihi tena kwa wakati. Je hapa vilaza ni wale waliohonga wakadahiliwa na kufanikiwa kuingia chuoni au wale waliowadahili ilhali wakijua kufanya hivyo–licha ya kuua elimu–ni kinyume cha sheria na tararibu hata akili ya kawaida common sense? Je hawa wote si vilaza japo kwenye maeneo tofauti? Waliosajili ni vilaza wasiojua aina ya watu waliopaswa kuwadahili na kuwaruhusu kujiunga na chuo. Je kuna vyuo vingapi vyenye kujaza vilaza ili kujipatia fedha badala ya kutoa elimu nchini? Je tatizo ni vyuo au mfumo mzima wa elimu nchini? Je kwanini wameadhibiwa wadahiliwa bila kuwahusisha wenzao waliowadahili. Waingereza husema; it take two to tango yaani hii ni ngoma ya wawili. Iweje waliosababisha kashfa hii wasiwe korokoroni wakingojea kupewa haki yao? Je ni vilaza wangapi wameishajipatia shahada kinyume cha sheria? Je serikali ina mpango gani kuwabaini na kuwachukulia hatua mojawapo ikiwamo kutotambua shahada zao au kuwalazimisha warudie masomo kwa gharama zao?
            Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu na kusema ukweli kama ambavyo–mara nyingi –rais Magufuli amesisitiza, Tanzania ina vilaza karibu kila idara na nyanja. Wapo kwenye mahakama, bunge, wakuu wa wilaya na mikoa, kwenye baraza la mawaziri; na wamo hata kwenye ofisi ya rais. Mfano wa karibuni ni kwa mtuhumiwa mmojawapo wa kughushi sifa za kitaaluma aliyefichuliwa na mwanaharakati Keinerugaba Msemakweli. Huyu si mwingine ni waziri William Lukuvi aliyetajwa sambamba na mawaziri na wazito wengine wa wakati ule. Waliotajwa na Msemakweli ni pamoja na Deodorus Kamala, Emanuel Nchimbi, Mary Nagu, Makongoro Mahanga, Victor Mwambalaswa, na Raphael Chegeni. Pia wapo mawaziri na vigogo wa zamani ambao CVs zao zinaonyesha shaka. Hawa ni aliyekuwa waziri wa fedha Saada Mkuya, naibu wake Adam Malima na aliyekuwa meya wa jiji la Dar Es Salaam Didace Massaburi. Malima na Mkuyu–kwa mujibu wa CVs zao–walipata shahada za pili bila kuwa na shahada za kwanza.
            Hakuna kitu kilishangaza wengi kama wawili hawa kupewa wizara nyeti ambayo matokeo yake ni majipu kama vile Escrow. Hata waliowateua nao wanatia shaka bila shaka.
            Msemakweli hakutaja tu bali aliandika kitabu alichokiita Mafisadi wa Elimu Tanzania. Baada ya Msemakweli kurusha kombora lake, Tume ya Vyuo vikuu, Tanzania Commission of Universities (TCU) iliwataka wahusika kufika mbele yake na kujitetea. Hadi sasa wananchi walio wengi hawajui kilichoendelea. Kwani si wahusika wala serikali waliokuwa tayari kueleza ukweli na uongo ni upi kiasi cha kuacha madai ya Msemakweli yakisimama kama ukweli usiopingika. Alipotoa shutuma hizi, wapo waliotishia kumshitaki wasifanye hivyo. Je hii maana yake ni nini? Ni kwamba waligwaya ima kutokana na madai ya Msemakweli kuwa ukweli mtupu au kuogopa kumwaga mtama kwenye kuku wengi kiasi cha kuumbuliwa zaidi. Hili hakika nalo ni jipu linalopaswa kutumbuliwa haraka huku watuhumiwa wakiwajibishwa kwa kutoza faini na kurejesha mapato yote waliyopata kwa kutumia sifa za kughushi. Kwa wale waliomo serikalini, wanapaswa kufukuzwa mara moja huku walioko bungeni wakifungashiwa virago haraka pia.
            Haiingii akilini kuwaadhibu wanafunzi tena vijana wadogo waliosukumwa na shida na uwepo wa mazingira kutenda kosa walilotenda huku serikali ikiwaacha mafisadi wakubwa wa elimu kama alivyowaita Msemakweli. Huku ni kutekeleza sheria kibaguzi na kuifanya iwatumikie wenye nacho wakati ikiwapatiliza wasio nacho.
            Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli awatumbue vilaza wazito ili kuondoa dhana ya upendeleo na kulindana. Maana kama atatumbua wanafunzi waliogundulika juzi wakati kuna vigogo waliojipatia vyeo na marupurupu bila kustahili, ataonekana kama anaendeleza mchezo ule ule uliokaribia kukiua Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa “Huyu ni Mwenzetu.” 
Chanzo: Mwanahalisi.

No comments: