Sunday, 26 June 2016

Je Gwajima anatumwa au anajituma?


            Katika kutapatapa ima kujiweka karibu na rais John Pombe Magufuli au kuficha maovu yake, askofu bandia na wa kujipachia Josephat Gwajima amelikoroga asijue jinsi ya kulinywa. Kwa waliosikiliza matusi, kashfa, uchochezi na maudhi yaliyomwagwa na anayejiita askofu Josephat Gwajima unashangaa kwanini nchi yetu inawavumilia viongozi wa kiroho waroho wa mali na madaraka wasioheshimu hata vyeo vyao. Unashangaa, kwa mtu kama Gwajima asiyejua jinsi ya kutumia kichwa na ulimi wake anachohubiri. Je ni kwa faida ya nani na kwanini na ili iweje? Je kuna kinachomsukuma Gwajima kusema anayosema? Si bure; k una namna. Gwajima anasikika kwenye mahubiri yake ambayo yako kwenye mtandao akisema vitu ambavyo haviingii akilini hasa pale anapojifanya mtetezi na msemaji wa rais John Pombe Magufuli. Je ametumwa au amejituma na ili iweje? Je Gwajima anadhani anaweza kumtapeli Magufuli ambaye sifa zake zinamtosha kiasi cha kutohitaji mtetezi? Hata kama Magufuli angehitaji mtetezi, si mtetezi na utetezi uchwara kama alivyobainisha Gwajima. Je Gwajima amesahau kuwa Magufuli na washauri na wasaidizi wake wanamjua alivyokuwa kipenzi cha Edward Lowassa, mgombea wa Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambaye anamsaliti na kutaka kujitenga naye? Kama amemsaliti Lowassa, Gwajima anaweza kumsaliti yeyote kama alivyofanya kwa Mungu wake ambaye amekuwa akimuuza badala ya kumtangaza. Je Gwajima anadhani watanzania ni wasahaulifu kama yeye? Kwanini asikubali kuwa alikosea na kuendelea na msimamo wake? Kama anaijua siasa vizuri basi avue joho na aanzishe au kujiunga na chama ili ajulikane yuko upande gani badala ya kutumia madhabahu kufanya uhuni.
Gwajima alitoa madai kuwa vyanzo vyake vya ‘kiufufuo’ vimemtaarifu kuwa kuna watu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana mpango wa kumhujumu na kumzuia Magufuli asiwe mwenyekiti wa CCM kwa hofu ya kutumbuliwa. Ya CCM yanamhusu nini wakati yeye si mwanasiasa? Nadhani vyanzo vya Gwajima si vya ufufuo bali ufu unaomsumbua kiasi cha kuhubiri uongo, uchochezi na kashfa bila sababu zozote za msingi. Bila shaka serikali haitamwacha hivi hivi. Gwajima alikwenda mbali akiwatuhumu marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kwa mambo mbali mbali amabyo hakuyatolea ushahidi. Alitaka wachunguzwe. Nadhani ni wakati muafaka kwa Gwajima kuchunguzwa alivyopata ukwasi wa kutisha kiasi cha kumilki helkopta. Je alifanya biashara gani halali au haramu tena kwa muda mfupi hivi? Gwajima alidai kuwa kuna genge la watu linalotaka kumzuia Magufuli asiwe mwenyekiti wa CCM.  Ni bahati mbaya kuwa Gwajima–katika kujikomba kwake–alishindwa kutoa ushahidi kwa kutaja majina ya waliopo nyuma ya hujuma hii. Magufulil awe au asiwe mwenyekiti wa CCM inamhusu nini Gwajima? Kwanini mambo ya Ngoswe asimuachie Ngoswe mwenyewe?
Gwajima licha ya kuonyesha ubabaishaji, kigeugeu na unafiki eti anasikika akilaani ufisadi kuanzia ujangili, mita za mafuta, kupitisha makontena bila kulipiwa na mengine mengi. Je Gwajima alikuwa wapi? Kwanini hakuyasema haya wakati yakitendeka hadi angojee ujio wa Magufuli? Mbona hakufanya kama maaskofu waliokuwa wakikemea serikali ya Kikwete?
Gwajima anadai kuwa alipigiwa simu kuombwa msaada wa kumhujumu Magufuli. Hapa ndipo utamu ulipo. Lazima abanwe awataje waliompigia simu.
Ili kumsaidia Gwajima na wengine wenye mawazo na tabia kama zake, serikali inapaswa kufanya yafuatayo:
Kwanza, achunguzwe ana mali kiasi gani na amezipataje
Pili, achunguzwe kama analipa kodi na kama vyanzo vyake vya kipato ni halali na ni vipi.
Tatu, achunguzwe alivyopata uaskofu anaoutumia kisiasa na kibinafsi.
Nne, aitwe na vyombo vya usalama ili kuthibitisha madai yake na akishindwa afikishwe mahakamani.
Tano, achunguzwe kama kuna watu wanaomtuma au anajituma na anafanya hivyo kwa sababu gani.
Sita, afahamishwe kuwa wakati huu si wa siasa za kibabaishaji, kupakana matope, majitaka na kulindana.
Saba, afahamishwe na kuonywa kuwa Magufuli ahitaji utetezi wake.
Nane, afahamishwe kuwa hawezi kumtapeli Magufuli na wala asijifanye mtetezi au msemaji wa Magufuli ambaye ana watu wa kufanya kazi hii tena walioisomea na walioajiriwa na si wa kujipendekeza au kujiajili.
Tisa, aeleze alikuwa wapi au alifanya nini kupinga maovu anayotaja kwa sasa na amesukumwa na nini ambacho kilishindwa kufanya hivyo wakati maovu yakifanyika wakati alikuwa nchini na akiwa na nafasi–hata kama ni ya kujipachika–aliyo nayo sasa.
Na kumi, je ana ugomvi binafsi na anaowatuhumu au ana taarifa ambazo wengi wangependa kuzijua baada ya kutolea ushahidi madai yake.
Tumalizie kwa kuuliza; Je Gwajima anatumwa au anajituma na ili iweje? Je anamchafua Magufuli ili iweje?
Chanzo: Mwanahalisi Jumatatu.

No comments: