Wednesday, 1 June 2016

Kijiwe chalaani akina Mkamia


            Baada ya muishiwa mmoja aliyewahi kutishia usalama wa uhuru wa vyombo habari kujipayukia akidai wapingaji wana sura mbaya wakati naye msura wake ni huo huo kama ubaya ubaya, kijiwe kimeamua kuja kulaani.
Jamaa huyu aiwaye Jumaaa Mkamia alitoa mpya aliposema, “Sasa nyie mnaoshangilia humu mna sura mbaya na mnatamani kutapika.” Kijiwe kinashangaa mambo ya ubaya na uzuri wa sura yanatafuta nini mjengoni! Kinazidi kukshangaa kwanini njengo umegeuzwa kituo cha daladala bila sababu nuzuhu.
            Mgosi Machungi analianzisha, “Wagosi, mnaona hii picha ya jamaa mwenye sua nzui hii hapa toto la kiangi? Wenye kutaka kuwowa jiandaeni mkakague sua. Hao hao!”
            Mpemba anamchomekea Mgosi akisema, “Wallahi acha nkuchomekee kabla hujamaliza utamu. Wallahi hili toto la kilangi mie lankata kusema ule ukweli. Sijui si mtoto riziki wala sina habari mie. Maana ukisikiliza anosema ushangaa ulijali wake wallahi. Mambo ya uzuri wa sura na mwanaume wapi na wapi yakhe!”
            Mijjinga anakula mic, “Mie simshangai huyu jamaa tangu akiwa waziri mdogo kwenye uhabithi uliopita hasa matamko yake ya kutumia masaburi badala ya kichwa. Hii si mara ya kwanza kulianzisha huyu jamaa. Nadhani tusimlaumu bali wazazi wake waliomlea vibaya. Sasa tazama anawaadhiri ukiachia mbali chata lake.”
            Kapende anakatua mic, “ Hata waliomchagua imekula kwao. Bahati yake ni kwamba wengi hawajui mambo yake. Maana wakiyajua mbona hata huo uishiwa atavuliwa asivyo na maadili hata kidogo. Kama anasema wapingaji wana sura nzuri ana matatizo. Sijui kwanini amesahau hata maneno ya baba wa taifa alipoulizwa swali la kijinga kuhusu kinyago chake cha mpapure alipokuwa akipanga kukizungusha kayani mwaka 1995.”
            Kabla ya Kapende kuendelea, Mipawa ananyakua mic, “Huyu mkumbaff anayesema wapingaji wana sura mbaya kwani tunatafuta wachumba njengoni au kuna kiti chamwasha kama si kuwa mtoto si riziki hasa ikizingatiwa kuwa siku hizi watu wanaigizi upuuzi huu na kujiona wameendelea. Si atangaze kama akina anti nanihii ili tumjue?”
            Msomi Mkatatamaa ankula mic, “Mie simlaumu huyu Mkamua sorry Mkamia. Kwanza, tukumbuke kuwa mjengo ulijifia zamani pale ulipogeuzwa uwanja wa mipasho na wavuta bangi kutumia kiswangilish na lugha nyingine za kihuni. Hamkumsikia yule muishiwa fyatu aliyewapa vipande vyao waishiwa wa dezo kuwa ni ma-mababies wakaamua kumjia juu wakati kuna ukweli ndani ya madai haya?  Ukiondoa hawa wanaoambiwa wana sura mbaya, kwangu mjengo hauna tofauti na kituo cha daladala cha Mwenge zama zile. Wamejaa wahuni wanaopaswa kuwa wapiga debe au majogoo lakini si waishiwa.”
            Sofia Lion Kanungaembe anakula mic, “Huyu kaka ameingiliwa na nini yarabi! Mbona huko nyuma hakuwa hivi? Analeta uzuri mjengoni asijue wanaweza kumtafsiri vibaya kuwa ana anachotafuta? Kuna haja ya kuwaambia wakubwa zake wamwajibishe na si kumkingia kifua kama bi mdogo Microphone alivyofanya alipoombwa mwongozo wa kutaka kumshughulikia kidhabu huyu.”
            “Audhubillahi Miina ashetwain rajiim huyu nsen… alipaswa  tolewa ukumbini. Huyu sioni tofauti bainaye na yule Mlemavu nilonsikia juzi akitaka mdandia maalim Seif asijue ule nlima. Waishiwa vibaya hawa. Kama yeye ntoto wa ntu na ana sura nzuri si atulie afaidi hiyo sura yake na vitu vyake yakhe?  Ukiwa na sura nzuri shurti uolewe. Si yeye na wanio na sura nzuri aache njengo wetu wende olewa au jiuza Ohio?” analaamika Mpemba huku akibusu kombe lake la gahawa.
            Kanji naye hajivungi, “Veve hapana chukia kama mimi. Ile mimi sikia ile tusi tamani ile toto pelekwe Bombei. Kana napenda hiyo kitu naenda Bombei tauzwa arabuni. Kama nafika arabuni naolewa kabisa bila ficha nacheva veve na watu ya arabuni!”
            Mheshimiwa Bwege naye anaamua kutia guu, “Kanji kwa mara ya kwanza umenivutia sana.”
            Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea, “Wewe! Amekuvitia vipi mbona sikuelewielewi Mheshimiwa? Eti Kanji amekuvutia.!”
Kanji anajitetea, “Veve acha changanya jambo. Mimi hapana vutia kama hii Kamia na sura zuri. Navutia na neno zuri.”
            “Ehee! Kumbe hata maneno matamu Kanji unayo! Kweli dunia imefika mbali! Nimevutiwa na maneno yako” Anachomekea Mbwamiwtu.
            Mheshimiwa Bwege anaendelea, “Jamani, msigeuze kijiwe kama mjengo wa mipasho. Mie wallaaahi simaanishi mambo ya Mkamia kuhusiana na kuvutiwa na Kanji. Amenivutia kwa kuliona tatizo kama lilivyo na ushauri wake wa kumtaka Mkamia asipate shida wakati watu kama yeye wanaweza kutumika arabuni tena bila ya kulazimika kuwatukana wenzao. Hata kama ana sura nzuri, kwani sura yaliwa na kama alivosema Dk Kapende, kwani tunatafuta nchumba mjengoni au hoja?”
            Msomi anarejea, “Mie simkamii wala kumlaumu huyu Mkamiwa. Nalaumu mfumo mbovu wa nambari wani kujaza wahuni mjengoni wasijue wataumbuka. Ukiangalia walivyotamalaki wahuni mjengoni utashangaa tunawkenda wapi. Kuna haja ya kumwambia dokta Kanywaji ayatumbue haya majipu. Nawaonea huruma walipoteza kura zao kuchagua mtoto kama huyu anayekwenda mjengoni kuuza uzuri badala ya kujenga hoja kwa ajili ya maendeleo ya wale waliomkopesha kura.”
            Kijiwe kikiwa kinango si likapita shangingi la mtoto mzuri mzuri tuliyeNkamia. Kama si dereva wake kuchanganya wese huenda sasa ashaozeshwa hadharani tena ndoa ya nkeka!
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: