Friday, 3 June 2016

Mlevi kumlinda Makufuli


            Naona yule anacheka na kutikisa kichwa hata kabla ya kusoma habari nzima. Usitoe hukumu kwa kusoma kichwa cha habari tu. Don’t judge a book based on the cover dude.  Naona yule anasonya akidhani bangi na ulevi sasa vinafikisha pabaya. Kwa taarifa yenu leo sijapata mma wala msokoto. Ndiyo nimeamka toka kitandani ambako niliyofanya usiku hayawahusu. Kwa ufupi mimi ni sober and normal sane na kamili.
            Baada ya rais Joni Kanywaji Makomeo kuwa analalamika juu ya hatihati ya maisha yake tokana na wale anaowatumbua majipu kutaka kumdhuru, Mlevi nimejitoa nikiwa na akili zangu timamu, bila kutarajia malipo yoyote wala ujiko na bila kushawishiwa na ngurumbili yoyote kujitoa mhanga kumlinda rais Kanywaji. 
            Kwanza si vibaya kugusia kidogo juu ya sifa zangu. Nina mkanda wa juu wa karate, gojolyuu na jet kune doo na madudu mengine magumu. Pia nimefanya kozi ya ukomando kwenye kaya ambayo ni top secret kutaja. Ni mlenga shabaha ambaye hajawahi kutokea duniani. Pia nimesomea intelligence, ushushuu na madude mengine ambayo si busara kuyataja dunia nzima. Nina PhD kama kumi kwenye masuala ya ulinzi na usalama bila kusahau ulevi.
            Tukiachana na maujiko yangu kwenye madude magumu kuelewa, ngoja twende kwenye mada yenyewe. Rafiki yangu mmoja shushuu amenitonya kuwa kuna gendaeka wenye mipango na nia mbaya wanataka kumfanyia kitu mbaya rais wetu. Ila inaonekana wamesahau kitu kimoja;mabo yamebadilika sana. Bongo ya sasa si ya 1984 alipouawa Eddy Morning Sokoine. This time, these putas and buggers should think twice; and they got it terribly wrong. Walevi hawako tayari kupata hasara nyingine baada ya hii ya Sokoine. Wamenituma niseme bila kumung’unya maneno kuwa atakayemdhuru kipenzi na mkombozi wao Mtumbua Majipu ajue hatafanikiwa. Patachimbika bila jembe; na patakuwa hapatoshi.
            Walevi wamechoka kuona kaya yao ikigeuzwa kichwa cha mwendawazimu na shamba la chizi. Hivyo, wale waliozoea vya kunyonga wajiandalie vya kuchinja. Walevi watachinja yoyote atakayemdhulu kamanda wao wa kupambana na ufisadi kwa njia ya kutumbua mapunye, vipele na majipu.  Kama wewe ni jipu jiandae kutumbuliwa lakini si zaidi ya hapo. Wale waliozoea kujiona wapo juu ya sheria wamechelewa. Wale waliozoea kutumia ofisi za umma kama maduka yao, wamepotea. Wale waliozooea kuugeuza urais urahis, walaaniwe na kutumbuliwa. Wale waliozoea kufanya mambo kwa mazoea, washike adabu na adabu iwashike. Uchangu wa kisiasa mwisho wake ni kwa Dokta Kanywaji.
            Tofauti na waganganjaa na matapeli wanaotaka kumtumia Dk Kanywaji kwa maneno na maombi na matunguli, Mlevi hana muda huo wa kutafuta ulaji na ujiko wakati hakuna lolote. Wengi wanaodai wanataka kumuombea Dk Kanywaji wana dhambi kasi kwamba hata sheitwan mwenyewe hawataki. Wengi wao wanahitaji maombi. Wao wametoa urongo wao. Yeye ametoa mwili, roho na damu yake kuhakikisha anasimama bega kwa began a Dk Kanywaji ili kufanikisha ukombozi wa walevi. Walevi hawana dini. Hawaendi kwa vigagula wala hawabembelezi wala kuzuga kama matapeli wa maombi. Wao hufanya kweli. Tunachukua michupa yetu na kwenda kumshughulikia yoyote tunayehisi anataka kumdhuru Dk Kanywaji. Usiombe kukosana na wavuta bangi tena wanaokula kitu inaitwa gongo. Hawaogopi hata ndata wala vigagula wala hawatapeliwi na yoyote isipokuwa mama mwenye baa. Wakiamua wanakuja na kumaliza udhia bila kujali yatakayofuatia.
            Acha nitumie fursa hii kumwambia Dk Kanywaji kuwa asihofu kitu; walevi tuko nyuma yake. Ila asiulize ili tumfanye nini. Tuko nyuma yake kumlinda dhidi ya washenzi wanaotaka kumkwamisha. Tutawakwamisha na kuhakikisha hapakaliki. Tunamwambia kwa kinywa kipana kuwa aendelee kutumbua majipu usiku na mchana wala bila wasiwasi wala kuangalia ukubwa wa majipu. Hata yale majipu yaliko chamani au kwenye serikali yake asiyaache. Hata yale yanayojipeleka ikulu mara kwa mara kutaka kumzuga ayatumbue. Hapa ni kazi tu; kutumbua majipu. Muhimu, asitumbue walevi. Maana, walevi si tishio kwa usalama wala ustawi wa kaya zaidi ya kaya zao.
            Kabla ya kusahau, tumkumbushe Dk Kanywaji. Akitaka kuondoa mzizi wa fitina, aangalie pale alipoanzia na wale waliomalizia pale. Asiangalie nyani usoni wala kuangalia ukubwa wala umaarufu wa nyani husika. wala asijali vicheko na mikenuo ya nyani wahusika wala ushawishi wa kujifanya wanamchekea wakati wangetaka wacheke kwenye matanga yake. Take on them without looking into their faces. Look into their eyes and tell them; this is it. Mlifanya ushenzi mliofanya; lazima malipo yawe hapa hapa kayani na duniani au vipi?
            Leo sitachonga wala kuzoza sana. Nakwenda kupiga tizi ili niwahi ikulu kuanza kumlinda Dk Kanywaji. Pia natoa taarifa rasim; wote mnaokula njama kumhujumu Dk Kanywaji–kama alivyoonya hivi karibuni kule Katesh–mnacheza na maisha yenu. Heri Mlevi kunyotoka roho akimlinda mkombozi wao kuliko kungoja wamhujumu halafu wawadedishe walevi kwa dhiki na ufukarishwaji, ukapa, ukwete na umwinyi. Message sent.
            Ombi; kwa wale wote wenye nia nzuri wanaotaka kumlinda Dk Kanywaji tukutane kwa Mfuga dog kwenye Dojo langu kuanza mazoezi ya kujichua tayari kuanza kumlinda mkombozi wa walevi mwana wa mlevi aliyempa jina la Kanywaji. See you then and thither guys.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: