The Chant of Savant

Wednesday 29 June 2016

Dk Kanywaji kuwalinda watawala wastaafu no


             Baada ya Rahis Joni Kanywaji Makufuli kutoa hakikisho kwa walaji wakubwa, Kijiwe kimeamua kumtolea uvivu kumwambia kuwa hana power wala uhalali kisheria kufanya hivyo.
Mijjinga ndiye analianzisha, “Jamani mmesikia namna rahis anavyoanza kujichanganya na kutuchanganya kiasi cha kushindwa kuelewa nini kinaendelea?” Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachangia, “Kumbe ulikuwa hujaliona hilo! Ulitegemea awe salama wakati nyuma yake kuna Chama Cha Maulaji (CCM) ambacho sera yake kubwa ni kulindana na kula pamoja?”
Mijjinga anaendelea, “Hili la chama cha maulaji na sera yao ya kulindana nalinyaka sana. Kilichoniponza ni mbio rahis za kupambana na ufisadi kiasi cha kuwakuna wachovu wengi wasijue ni mbio za sakafuni. Sikutegema kama mkuu angeweza kutamka aliyotamka kuwa atawapa ulinzi wale waliosababisha kaya yetu ifikie hapa ilipo kiasi cha kumhangaisha huku akilalamika mara kwa mara. Kumbe sharia yetu inatumika kwa kuangalia sura ya wahalifu siyo? Nadhani walindwa sasa wanafurahi wakitononoa usingizi wasijue ndiyo sekeseke linaanza. Wallahi mie sikubali kura yangu itumike kuwalinda wahalifu hata wawe wakubwa kama tembo.”
“Kaka siasa hizo. Warabu wa Pemba hujuana kwa vilemba hukuambiwa? Kumbe m wenzangu ulisahau ule msemo wa usanii uliokuwa ukitawala wakati wa usanii uliopita siyo! Na bado mtanganyikiwa zaidi msijue la kufanya usawa huu wa kutumbuana kwa upendeleo na kuangalia sura.” Anachomekea mzee Maneno huku akibwia gahawa yake.
Mgosi Machungi anakatua mic, “Hapa azima aisi ajue; sisi tiinchagua na kumtuma afanye kazi tiiyomtuma ya kuhakikisha usaaama na maendeeo ya wanakaya na si wazito kama anavyoanza kufanya. Yeye ni mtumishi wetu na si mtumikishaji wetu.”
Msomi Mkatatamaa leo hangoji. Anamua kula mic, “Tuache kujidanganya. Huyu bwana hana uwezo huo kikatiba kwani kazi ya kuwalinda wanakaya ni ya kila mwanakaya na katiba na si rahis. Hapa atapaswa asaidiwe na wataalamu wa katiba tusije kufikishana kwenye vyombo vya sharia kimataifa. Haiwezekani tuone madudu yanafanyika nasi tuwe mashahidi. Mbona kila jambo liko wazi kuwa tunachotaka ni utawala wa katiba na bora si bora utawala unaoweza hata kuvunja katiba? Hata hivyo, naona kama kuchanganyana, kuchanganyikiwa na kujichanganya. Kwani, juzi nilishuhudia na kusikia mwenyewe pale Biafra akisema kuwa anachotaka kufanya ni kupambana na wezi wachache waliokuwa wakila njuluku za umma. Aliongeza kusema kuwa kama wanataka kula waende wakale njuluku za bibi zao. Kwani hawa anaotaka kuwalinda si wachache na hawana bibi zao wanaopaswa kula njuluku zao?”
Mpemba anachomekea, “Hata miye nilikkuwepo pale wallahi akitoa vipande kwa wezi wa fedha za umma. Na mie hii kauli wallahi ilinchanganya na kunifanya nianze kushuku kuwa kumbe kilichokuwa kikinkata hadi kunshabikia huyu bwana nkubwa sasa chaanza kuwa mbio za sakafuni.”
Kanji akawanyua mic,”Kweli dugu yangu mimi iko sikitika sana. Iko anza ona shaka kuba sana jamani. Kama katiba nasema nalinda chovu vote kwanini sasa linda kuba tu? Hapa iko kitu kama naona vatu naanza piga tama venyeve. Aibu kuba kweli kweli dugu zanguni.”
Mipawa anaamua kumchomekea Kanji, “Hata mimi nahisi kuchanganyikiwa na kizungumkuti kugundua kuwa kuna wanakaya wasioona madudu kama EPA,Richmonduli,Kiwila,NBC, Lugumi, Escrew,UDA na mengine si wizi wa fedha za umma. Je umma huo anaomaanisha huyu bwana ni upi kama haoni huu umma unaotaka wanene waliovurunda wapelekwe kwa pilato? Au jamaa amejigeuza pilato kiasi cha kulewa maulaji asijue kila jambo lina mwanzo na mwisho?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kukamua,”Mie wala sishangai. Tangu mjomba wangu alipovunjiwa nyumba yake wakati walioiba nyumba za umma wanahakikishiwa ulinzi, sina hamu na kinachoendelea na najutia hata hiyo kura yangu ya kula. Hatuwezi kuendelea hivi. Lazima kijiwe kichukue hatua ili kuondoa haya mazabe kabla hayajageuza majipu. Lazima yatumbuliwe bila kujali nani anamtumbua nani. Hii kaya ni yetu sote na si ya wakubwa wala nini. Si yao wala ya bibi zao.”
Msomi anarejea tena, “Kwa hali iliyojitokeza hivi karibuni kiasi cha kuchafua hali ya hewa, nadhani tendo lolote huwa ufisadi au halali kutegemea nani aliyelitenda. Kosa likitendwa na mkubwa linasamehewa. Likitendwa na mlalahoi linakuzwa na kuwa big deal even from nothing. Hayo madudu yote uliyoongelea yangekuwa kashfa na jinai kama yangetendwa na wachovu. Yakitendwa na wakubwa ni halali hasa ikizingatiwa kuwa sasa mamlaka yameamua kujifichua kuwa yako pale kuwalinda wanene kwa kuwaumiza wadogo. Hamuoni wanavyolipwa mabilioni ya madafu kwa kutuibia na kuvuruga kaya yetu kiuchumi? Hii ndiyo Bongolalaland ambayo huwa mzee Mpayukaji anaongelea mara kwa mara kama alivyo-coin hili jina.”
Mchuguliaji aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kuchomekea, “Namna hii sijui tumwamini nani wakati tunarudishwa kwenye arifu na ujiti na wale tuliozugika na kuwaamini kuwa wangetuvusha wakati lengo lau ni kutuingiza mkenge na kutuzamisha.”
Kapende anachomekea, “Tusipokuwa makini na wakali dhuluma hii inaweza kufanikiwa. Hukuwasikia wanene wakisema kuwa kuanzia sasa hakuna siasa bali kuchapa kazi ili wakubwa wanaolindwa waendelee kuhomola ima kwa kutumia waliowaacha nyuma au kuongezewa marupurupu? Hapa–wakati mwingine–unashindwa kutofautisha jipu ni lipi usawa huu wa kuchanganyana hadi kuchanganyikiwa na kujipiga mitama hadharani.”
Mgosi naye anarejea tena, “Mimi naona tisikubai hii dhuuma. Azima tipange mikakati ya kuandamana ii kupinga hii agizo la kuindana na kupeana motisha kutiibia zaidi. Haiwezekani kama mbwai mbwai.”
Mpemba naye hajivungi, “Yakhe sasa nimeelewa kwanini jamaa alishindwa na kupuuzia dhulma ya Zenj aliyofanya yule habith Jechia Salimuni Jechia ya uchakachuaji.”      
Kijiwe kikiwa kinanoga ulipita msafara wa munene. Wala hatukuushangilia zaidi ya kuzomea kimoyomoyo.
 Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: