Thursday, 16 June 2016

Nasi tujiandae kuwachunguza marais wetu


            Ingawa hili linaweza kuonekana kama jambo la ajabu–hata wengine kudhani ni kushikana uchawi–taifa letu linapaswa kuenga kila kona ili kuhakikisha mageuzi ya kweli anayolenga kuyafanya rais John Pombe Magufuli yanafanikiwa kwa haki na usawa. Hadi tunaandika, kuna maafisa wengi wa umma wameishatumbuliwa majipu tokana na ima utendaji wao au historia ya utendaji wao. Pia wapo ambao hawakutarajiwa walioachwa nje ya serikali yake. Kadhalika, wapo ambao hawakutarajiwa wala kufaa wamo kwenye serikali yake.
            Hivi karibuni nchini Brazil walianza safari ya kujisafisha ili kuweza kusonga mbele. Kwa kuanzia, walimsimamishakazi ili kumchunguza rais wao Dilma Rousseff ambaye kwa sasa anapambana vikali kusafisha jina lake na kurejea madarakani.
            Nigeria ilifuatia; kwa kumchunguza rais mstaafu Goodluck Jonathan ili kuweka mambo sawa. Israel walikwenda mbali hadi kumchunguza mke wa waziri mkuu aliyeko madarakani, Sarah Netanyahu kwa kashfa ya kutumia fedha za umma kununulia samani kwenye nyumba yao binafsi.
Kutokana na madudu ambayo rais John Pombe Magufuli amekuwa akilalamikia, kuna haja ya kuchunguza marais wote waliopita bila kuwasaza na wale wa Visiwani. Inabidi ieleweke; kutaka kuchunguza marais waliopita siyo kuwahukumu kabla ya kupatikana na hatia. Wala nao wasiwe na wasi wasi kama wanajua hakuna baya walilotenda hasa utumiaji vibaya madaraka.
            Mifano miwili ya Brazil na Nigeria ni ya kuigwa. Mfano wa tatu wa Israel unafaa sana hasa ikizingatiwa kuwa kuna wanafamilia wa marais waliopita ambao wametokea kuwa matajiri kwa sababu wazazi au waume zao walikuwa madarakani. Tuchunguze Asasi Zisizo za Kiserikali (NGO) walizoanzisha wake wa marais wetu waliopita kwa ajili ya kujipatia utajiri kwa kisingizio cha kuwasaidia akina mama na wasichana wakati kuna wizara maalumu kwa ajili hiyo. Tuchunguze hata washirika na marafiki wa viongozi wetu. Wala tusiwaonee aibu; kama leo–kwa mfano–rais Magufuli anawatumbua majipu watumishi wa umma, kwanini nasi tusiwachunguze marais waliopita hasa ikizingatiwa walikuwa watumishi wa umma. Hakuna aliyeko juu ya sheria wala hakuna anayeweza kuaminika kwa sababu tu alikuwa rais au alikuwa na madaraka makubwa serikalini au chamani.
            Kuwachunguza viongozi wastaafu kuna faida kadhaa:
Mosi, kutawaondolea shutuma ambazo zimekuwa zikiendelea kichinichini au wazi wazi dhidi yao. Pili, kutawaumbua wale waliotenda uovu ili uwe mfano kwa wengine wajao. Tatu, kutarejesha maadili ya uwajibikaji. Nne, kutajenga dhana kuwa hakuna aliyeko juu ya sheria. Tano, kutaondoa ufisadi ulioanza kuzoeleka ambapo madaraka ya umma hugeuzwa mali ya familia.
            Karibu kila rais mstaafu–isipokuwa marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere–ana kile waingereza huita skeletons in the closet. Kwa mfano, rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliondoka na kashfa ya Loliondo ambapo sehemu ya mbuga ya taifa iliuzwa kwa waarabu kinyemela jambo ambalo liliendelea kumuandama hata miaka zaidi ya 20 tangu aondoke madarakani. Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa naye hakunusurika. Ana kongwa zake kama vile kujitwalia Machimbo ya Makaa ya Mawe ya Kiwira, ubinafsishaji wa kijambazi na kuruhusu mkewe kuwa na kampuni almaaruf NGO ambayo aliitumia kijipatia utajiri wenye kutia shaka.
            Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiyo usiseme. Hata kabla ya kuingia madarakani alishahusishwa na kashfa ya EPA iliyotokomeza mabilioni ya shilingi zote fedha za umma. Akiwa madarakani, licha ya kuzembea kwenye usukani, kuzurura na kutumia vibaya fedha za umma na madaraka, Kikwete anasifiki kama rais ambaye unaweza kumuita ajali ya kisiasa kwa taifa letu. Funga kazi ya Kikwete ni pale alipoondoka madarakani akiwa ameacha kashfa zenye kuzamisha mabilioni ya shilingi za umma kama vile Escrow na UDA ambazo karibu zote ima zinamhusisha yeye au watu wake wa karibu.
     Mwanahalisi online (11 Novemba 2014) ilikuwa na haya ikimhusisha Kikwete na kashfa ya Escrow. “Kampuni hii ya PAP iliyopewa tuzo hiyo ya 400bn kwa kuwekeza 6mTsh tu ni ya nani? Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, 50% inililiwa na Singh Sethi (singasinga) na mwanae na asilimia 50% zinamilikiwa na kampuni ya Simba Trust ya Australia.”
Mwanahalisi online iliongeza, “Simba trust ni nan.? Uchunguzi umeonesha kuwa Simba trust ya Australia inamilikiwa na watu wawili ambao ni salima Kikwete na Miraji Kikwete.” Nao mtandao mkubwa wa kijamii kuliko yote Tanzania, Jamii Forums (28 Januari 2015) haukuachwa nyuma kumfichua Kikwete. Kwani uliandika, “Taarifa zinasema, familia ya Rais Kikwete imepata zaidi ya Sh. 9 bilioni, kutoka katika mgawo wa fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow.”
            Nalo gazeti la Dira ya Mtanzania la Novemba 30–7 Desemba 2015 halikuachwa nyuma katika kuiunganisha familia ya Kikwete na kashfa ya UDA. Kichwa cha habari ongozi kwenye gazeti hili kilisomeka, “UDA kutua kwa Magufuli, yabainika ilitwaliwa bila malipo, Ridhiwani Kikwete ahusishwa.”
            Kwa uchache ni kwamba huo mnyumbulisho wa madudu ya watawala wetu waliopita ni jipu tena lenya kansa, kubwa na linalonuka ukiachia mbali kutishia mustakabali wa taifa letu.
            Tumalizie na tulikoanzia; tukihimiza kuwa ipo haja ya kuchunguzana ili kuweka mazingira ya uwajibikaji sawa na wa kweli baina yetu tayari kwa kusonga mbele. Naomba kuwasilisha hoja. Viongozi wetu wala wasiwe na wasiwasi kama wao si majipu wala magamba.
Chanzo: Mseto, leo.

No comments: