Sunday, 12 June 2016

Watanzania hakikisha mnamlinda Magufuli


            Rais John Pombe Magufuli amesikika mara nyingi akiomba watanzania wamuombee. Hii ni kutokana na ugumu na hatari ya kazi na mambo anayofanya. Bila shaka, Magufuli anajua hatari inayomkabili kama kiongozi na kama binadamu. Hivyo, kuonyesha wasi wasi si jambo la kushangaza wala kuchanganya. Anajua fika yaliyowakuta waliojaribu anayofanya mmojawapo akiwa marehemu Edward Moringe Sokoine, waziri mkuu wa zamani aliyekufa kwenye mazingira tatanishi tokana na msimamo wake wa kuchukia maovu hasa ufisadi. Pia, Magufuli si mgeni katika siasa za taifa letu. Anajua kila kitu ugumu na hatari zake. Hivyo, anaposema amejitoa kafala anamaanisha linaloweza kumtokea toka kwa makundi ya wahalifu waliozoea kupata utajiri wa haraka utokanao na kuhujumu na kuidumaza nchi yetu. Pia, anajua mifano mibaya iliyoachwa na waliomtangulia ukiondoa marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere aliyeacha rekodi iliyotukuka ya uongozi na utendaji.
            Tokana na hatari na kitisho kinachomkabili rais Magufuli, tunadhani kumuombea pekee hakutoshi. Watanzania, hasa wale wanaoridhishwa na mipango, kasi na utendaji wake, wanapaswa kuwaambia wale wanaopanga kumkwamisha au kumdhuru kuwa ikitokea wakafanikiwa kutekeleza jinai yao, nchi hii haitakalika.
            Kuomba kunaweza kuwa njia ya kumridhisha mhusika na wanaomuombea. Lakini hakuaminiki; ikizingatiwa kuwa hata wanaoteseka, kufa, kufukarishwa na wengine wengi huomba; lakini maombi yao ima huchelewa, hukubaliwa au kukatawaliwa. Tofauti na kumlinda Magufuli, kama wale wanaotaka kumkwamisha au kumdhuru wataelewa madhara ya kufanya hivyo, bila shaka watafikiria mara mbili.  Magufuli hafanyi anayofanya kwa faida binafsi na familia yake. Yeye ni tofauti na wengi waliomtangulia ambao walitanguliza matumbo badala ya utaifa na watu wake. Kimsingi, Magufuli licha ya kuwa tofauti na watangulizi wake watatu, ni suto na kero kwao kutokana na alivyowaumbua. Wengine wapo wapo wakihaha wakijaribu kujinasua na madhambi waliyotenda ikizingatiwa kuwa hadi sasa hawajui kama Magufuli atawalinda au kuwatosa. Anapotoa yake ya moyoni, wengi mioyo inawauma wasijue nini utakuwa mwisho wa matendo yao machafu kwa taifa. Ushahidi uko wazi: wote waliowekwa kwenye mifuko ya wahalifu na matajiri, hawawezi kumpenda wala kumuunga mkono Magufuli. Wanaweza kufanya hivyo hadharani; ingawa nyuma ya pazia hali ni tofauti.
            Kwa vile wahanga wa jinai ya kuacha nchi itafunwe ni watanzania wenyewe–ambao Magufuli anataka kuwakomboa–ni jukumu lao kuhakikisha hadhuriki wala kukwamishwa. Kwani hili likitokea, watakaopata hasara ni watanzania na si Magufuli.
            Kutokana na ukubwa wa tatizo, tunamshauri Magufuli awe anawashughulikia kwanza kabla ya kutangaza nini atafanya. Maana kufanya hivyo, kutawanyima wabaya wake fursa ya kujua anachowapangia. Magufuli anapigana vita kubwa na ya hatari. Hivyo, hapaswi kuweka mipango na mikakati yake wazi; ili maadui zake wasiitumie kumkwamisha au kummaliza.
            Tunaamini watanzania walio wengi ambao walikuwa wamepigika na kuathirika–na bado ni wahanga wa hujuma hii vibaya tokana na utawala mbovu–hawataruhusu kundi dogo la wahalifu liwakwamishe kwa kuwanyang’anya tunu yao. Kama ilitokea kwa Sokoine, basi inapaswa kuwa somo tosha. Tusikubali kuona wahalifu wakiendelea kuweka nchi yetu rehani kwa sababu wana fedha, ushawishi na uroho. Sipendi nionekane namkweza Magufuli. La hasha.Tukimlinganisha na awamu tatu mbovu zilizopita na mateso tuliyopata, si haba; Magufuli ni lulu inayopaswa kutunzwa kwa gharama yoyote.
             Unapotoa madai lazima utoe ushahidi. Awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi inasifika kwa uholela uliofanywa chini ya kauli mbiu mbovu ya ruksa ambayo, kimsingi, ndiyo mama wa ufisadi unaotuhangaisha kiasi cha rais wetu kujihisi yumo hatarini. Awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa ilianza vizuri kabla ya kushauriwa vibaya kuhusiana na uwekezaji ulioishia kuwa uchukuaji ambapo hata Mkapa mwenyewe alijichukulia Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ambao umegeuka kongwa shingoni mwake. Laiti Mkapa angeliona mbali. Magufuli angekuwa anazama kwenye viatu vyake. Awamu ya nne imeonyesha kuwa ya hovyo kuliko zote hasa baada ya rais kugeuka mzururaji akiombaomba huku akiachia raslimali na mali za nchi zikiibiwa na kuvujwa kana kwamba haikuwa ikimhusu. Hakuna sehemu Kiktwe alijikaanga vibaya kama kukiri kuwa ana orodha za wahalifu wote kuanzia mafisadi, wauza unga, majambazi na wala rushwa lakini asikamate hata mmoja; tena bila kutoa sababu wala maelezo. Pia Kikwete anaonekana kuwa mbovu kuliko wote kutokana na kuingia madarakani kwa madai kuwa alitumia fedha ya wizi wa mabilioni ya umma chini ya kashfa ya EPA asikanushe wala kuongelea hata siku moja. Magufuli, tofauti na wote, anasema wazi. “Unapoona watu wanashangaashangaa sana kwa sababu hawakuzoea haya. Na walifikiri nitakuwa part of them (mmoja wao), never (hasha), not me (si mimi). Haya ni maneno mazito ya mtu mwenye uchungu na taifa lake. Lazima tumuunge mkono na kumlinda kwa gharama yoyote. Watu kama hawa hutokea mara moja katika miaka mingi. Ni kama kushinda bahati nasibu.
            Tuhitimishe kwa kuwataka watanzania wasiishie kumuombea rais Magufuli. Wanapaswa kumlinda, kumsaidia, kumkosoa na kumuongoza pale anapozidiwa. Yeye ni binadamu sawa na wao na analikubali hilo kiasi cha kujinyenyekeza kwao huku akishupaa dhidi ya wale wanaotaka kuendelea kuwaibia, kuwadhalilisha na kuwanyanyasa.
Chanzo: Tanzania Daima, leo.

No comments: