Sunday, 26 June 2016

Punguza na toza kodi mafao ya marais wastaafu


            Hakuna ubishi kuwa viongozi wetu wastaafu wanapewa marupurupu mengi na makubwa, jambo ambalo kiasi fulani linawakwaza watanzania wengi hasa walio maskini. Hii ni kutokana na kutwisha mzigo wa kuwatunza viongozi wastaafu kuanzia marupurupu, kulipia matibabu yao na familia zao, kulipia wafagizi, watunza bustani, walinzi, madereva, wapishi na wengine. Kimsingi, viongozi wetu wanaishi–kwa kukopa maneno ya rais John Pombe Magufuli–wanaishi peponi wakati wanaowagharimia wakiishi motoni au wanaishi kama malaika wakati wanaowagharimia wanaishi kama shetani.
 Hata hivyo, rais Magufuli alionyesha mfano wa uongozi alipoamuru mafao ya wabunge yakatwe kodi. Magufuli hakuishia hapo; aliamuru na mafao yake yakatwe kodi. Huu ni mfano wa kuingwa na kupongezwa. Tunamshauri rais asonge mbele kwa kupunguza na kutoza kodi mafao na marupurupu ya viongozi wastaafu ambao–kwa nchi maskini kama yetu–wanapewa fedha nyingi hata wasizohitaji wakati umma ukiendelea kuteseka na kubebeshwa mzigo. Kwa mfano, huwa nashangaa kulipia matibabu ya marais wastaafu ndani ya nje hata kwa wale walioua huduma za afya. Tunawalipa kwa kazi gani? Wanalipiwa walinzi, wafagizi, watunza bustani na maeneo mengine kiasi cha kuishi peponi wakati watanzania walio wengi wakiishi motoni. Tunaunga mkono hatua za makusudi za Magufuli za kupambana na ufujaji na wizi wa fedha za umma. Unashangaa, kwa mfano, kuona marais wastaafu wakirundikiwa marupurupu huku wananchi walipa kodi na wachapakazi wakizidi kuminywa. Marais wetu wastaafu wanaishi peponi. Unaweza kuona hili kwenye namna ya wanavyoishi.
Hakuna kitu kinafanya wananchi wawachukie viongozi wao kama kuona wanavyojipenda wakijilimbikizia marupurupu kwa upande mmoja na kuwa kama wafalme huku wakihubiri usawa kwa upande mwingine. Unashangaa kama kweli wanaamini katika yale wanayofanya ukilinganisha na kuangalia walichofanya wakiwa madarakani. Unashangaa na kuhoji mantiki, kwa mfano, ya kumpa marupurupu kiongozi mstaafu ambaye kuna ushahidi wa wazi kuwa uongozi wake uliingizia taifa hasara. Je mtu kama huyu–anayepaswa kufikishwa mahakamani kwa makosa aliyotenda–anazawadiwa marupurupu yote haya kwa kazi gani kama siyo kulea majipu yanayopaswa kutumbuliwa bila simile wala huruma? Je hii–licha ya kuwachochea na kukakatisha tamaa wafanyakazi wa chini–inaleta picha gani na kutoa mfano gani? Heri Magufuli ameliona hili na kulifanyia kazi. Hata hivyo, inashangaza kwa rais Magufuli–kwa mfano–kupunguza mshahara wake na ile ya baadhi ya watendaji wa umma huku akifumbia macho marupurupu ya viongozi wastaafu ambayo ni makubwa bila sababu. Tungeomba rais aliltolee hili ufafanuzi ili kuwapunguzia walipa kodi masikini mizigo isiyo na ulazima. Tunadhani tumpe muda tuone atafanya nini kuliangalia na kulishughulikia hili ili kuondoa ubaguzi katika kufaidi keki ya taifa ambayo imegeuzwa ya watawala familia zao, marafiki zao na wote wenye ushawishi iwe wa kifedha au kimadaraka.
Wapo wanaopendekeza hata hizi kinga walizojipa viongozi ziondolewe au kuwekewa masharti mfano, mhusika apewe marupurupu baada ya kubainika kuwa alifanya kazi aliyochaguliwa kufanya vizuri na kwa ufanisi ili kuepuka kulinda na kuwazawadia waovu jambo ambalo ni kishawishi cha uchu wa madaraka na utendaji maovu. Watahofia nini iwapo wana kinga. Kuondoa kinga, licha ya kuleta uwajibikaji na uchapakazi, utaondoa dhana kuwa urais ni sehemu ya kuchumia utajiri wa haraka kwa mwenye kuushika, familia yake na marafiki na washirika wake. Tufike mahali tubadilike na kuyaangalia mambo kama yalivyo.
Marais wastaafu hawastahili marupurupu makubwa wanayopata hasa ikizingatiwa kuwa walikuwa wakijilipa mishahara mikubwa walipokuwa madarakani ukiachia mbali wengine kutumia ofisi kujineemesha. Ushahidi wa kujipa mishahara mikubwa uko wazi. Rejea hatua adhimu za rais Magufuli kupunguza mshahara wake. Alifanya hivyo kutokana na kugundua kuwa mshahara husika ni mkubwa hasa kwa nchi maskini na ombaomba kama yetu. Hata hivyo, Magufuli alikaririwa juzi akiwakiwazodoa wanaotaka viongozi wastaafu washughulikiwe. Amewahakikishia ulinzi kiasi cha kuwachanganya watanzania wanaodhani anataka kutenda haki kwa watanzania wote kwa usawa katika kupambana na ufisadi. Kilichojitokeza ni kwamba Magufuli–kama alivyokaririwa akisema hivi karibuni–yupo madarakani kuwalinda watawala wa zamani na si watanzania. Sijui huku ni kujichanganya au kuwekwa sawa, sijui; na kweli sijui.
Je Magufuli anaanza kujipambanua kuwa siyo yule yule tunayemuona na kumsikia majukwaani? Je ameonywa kuwa naye ataondoka madarakani siku moja? Je kuna yake tusiyoyajua ambayo–hawa aliwaahidi ulinzi hata wale anaowalaumu wazi wazi kuharibu nchi–wanayojua ambayo hatuyajui na Magufuli asingependa yajulikane? Je ni ule ule usanii wa CCM na sera yake kuu ya kulindana? Hakika sijui.
Tumalizie kwa kusema kuwa hakikisho la ulinzi kwa viongozi wastaafu ni ushahidi kuwa sheria za nchi yetu zinatumika kitabaka kwa kuwapatiliza wasio na madaraka na kuwalinda wenye madaraka. Hakiki, hili, litammaliza Magufuli kiasi cha watanzania kujutia ni kwanini waliiamini tena CCM wakati wakijua kuwa ni ile ile iliyotekwa na wenye madaraka pindi tu alipong’atuka baba wa taifa. Hata hivyo, tuseme; Tanzania si mali ya watawala wala ya Magufuli bali ni mali ya watanzania. Wanachotaka kinapaswa kupewa kipaumbele kuliko maslahi uchwara na haramu ya watawala. Ni vizuri wahusika wakaelewa na kutambua kuwa taifa ni zaidi ya genge la watu wachache wenye madaraka au ushawishi.
Chanzo: Mwanahalisi Jumatatu.

No comments: