Friday, 1 July 2016

Mlevi kuomba appointment na rahis kupata maelezo


            Sipendi kujisifu; juzi nilipata mwaliko kwa Mama kuwashauri juu ya kura ya namna ya kujitoa kwenye jumuia ya Ulaya; na walisikiliza ushauri wangu ambao pia nitautoa kwa kaya kujitoa kwenye Jumuia ya Afrika Masharika. Hivyo, yaliyotokea kayani yalinipita; ingawa niliporudi bi mkubwa alinipasha kila kitu. Mambo yote yalikuwa swali isipokuwa jambo moja tu. Nikiwa nimerejea kutoka kupiga ulabu–hasa ikizingatiwa kuwa kule kwa mama ulabu ni aghali–bi mkubwa alinitonya kuwa rahis Joni Kanywaji Makufuli alitoa hakikisho la kuwalinda walaji wakubwa waliochezea ulaji kwa kuruhusu wizi na kujihomolea kana kwamba kaya haikuwa na mwenyewe. Hii ni baada ya walevi fulani kutaka watumbuliwe kutokana na mauzauza waliyotenda kama vile kusababisha upigajiwa EPA, Escrow, Kiwira, kutorosha wanyama wetu umangani, ujangili, SUKITA, Richmonduli, Kagoda, NBC, TANESCO na madudu mengine makubwa tu.
Tokana na kuwa huwa namwamini sana bi mkubwa–nisipomwamini nitakaribisha baridi itanipige usiku–sikushuku taarifa yake iliyioniacha nikiwa nimechanganyikiwa nisielewe mantiki ya hakikisho hili. Usomi na uzoefu wangu wa sheria unaniambia kuwa katika kaya yetu suala la kumlinda au kutomlinda mbongo haliko mikononi wala chini ya mamlaka ya yeyote isipokuwa katiba. Hivyo, nitakapopata appointment na munene Kanywaji, nitataka kumpa shule ya bure kuwa hakuna awezaye kumhakikisha mwanakaya ulinzi isipokuwa katiba. Katika hata ile yenye viraka ya walevi inasema wazi kuwa wanakaya watalindwa dhidi ya jinai na uovu lakini si kulindana katika uovu kama hakikisho hili–ambalo hadi sasa sijaamini kama kweli katoa rahis–linavyosema. Haiwezekani rahis atoe hakikisho juu ya mambo yanayopingana na kuvunja sheria. Kazi yake si kuamua nani atumbuliwe au asamehewe bali kutenda haki na kuhakikisha haki inaonekane inatendeka.
Siku hiyo nitavuta kitu yangu tu bila kuonja kanywaji ili niweze kumpa shule ya uhakika. Kwanza, nitamwambia apewe nakala yake ya katiba; kwa sababu nami nitakuwa na yangu. Nitamuomba anijulishe alikopata haya mamlaka ya kusamehe madhambi utadhani yeye Mungu. Pili, nitamtaarifu achunge asidanganywe akafanya mambo kama muungu mtu kwa vile yale mamlaka aliyo nayo si yake bali ya wananchi. Baada ya kuishi ulaji wake atafungasha virago na kurejea kwao akiwa kifua mbele au kichwa chini kutegemea alitekeleza au hakutekeleza wajibu wake. Akiboa, anaishi kwa taabu akitegemea wa kumlinda kama anavyotaka kuwafanyia hawa jamaa aliowahakikishia ulinzi japo hana mamlaka ya kufanya hivyo. Hapa ndipo walevi wamenituma nimkumbushe kurejesha katiba ya walevi iliyoka wanene wakataofanya madudu wavuliwe kinga na kusulubiwa bila kujali ukubwa wa vyeo vyao.
Tatu, nitamtaarifu kuwa kazi ya rahis si kujipangia na kupanga kazi bali kupangiwa kazi na katiba kwa niaba ya wanakaya anaotaka kuwakomboa toka kwenye uchafu wa waliomtangulia. Sasa–kama kweli anataka kuwakomboa walevi -atawezaje wakati anaahida kuwalinda wale waliowakwamisha na kuwashikinisha kwa kuruhusu ukwapuzi, uzembe, uzururaji, ujangili, ujambazi, bwimbwi na ushenzi mwingine?
Nne, nitamtaarifu kuwa wajibu wake ni kuwatumikia walevi na si kuwatumia; yeye si bwana bali mtumishi tu wa walevi. Lazima rahis atimize mapenzi ya walevi na si mapenzi yake, wakubwa zake au marafiki au chama chake.
Tano, nitamtaarifu kuwa kazi yake ni kutekeleza maagizo ya walevi na si kuwapa maagizo au amri. Kwani hii kaya ni yao na si ya rahis. Nitamuonya kuhusu mfano anaotaka kuuweka kwa viongozi wajao. Maana ukilinda wizi na uongozi wa hovyo–ina maana–unatoa motisha kwa viongozi wengine wezi na wa hovyo wajao wafanye madudu tena makubwa kuliko haya aliyokuwa akilalamikia mara kwa mara. Pia, nitamfahamisha kuwa alichosema–kama kweli alisema kwa makusudi na si utani–basi linamfanya aonekane kujipinga na mtatanishi anayeweza kusema hili kesho akasema lile.  Huu si uongozi ni uongo tu wa kawaida ambao sidhani kama mheshimiwa rahis anaweza kuuendekeza achilia mbali kuufanya.
Sita, pamoja na ulevi wangu–kama ningekuwa nimechaguliwa kuwa rais wa kaya–sidhani kama ningeweza kujidhalilisha kuwalinda wababaishaji, wezi, wazembe na wapiga dili waliochezea ulaji wao. Nisingefanya hivyo kwa mkono wa kushoto wakati mkono wa kulia nabariki na kulinda hiki ninacholalamikia.
Nane, nitamshauri bwana rahis aangalie lugha anayotumia. Kwa mfano, nitamshauri awe anasema sirikali yangu kwani sirikali anayoongoza ni ya walevi na si yake kama familia yake au duka la akina kanji.
Tisa, nitamshauri rahis asiwe anatumia lugha ya ninataka bali walevi wamenitaka nifanye kadha kadha lakini siyo ninataka kufanya kadha wa kadha kana kwamba kaya ya walevi ni mali yake binafsi.
Kumi na mwisho, nitamshauri munene aangalie namna bi mkubwa wake anavyoanza kujiingiza kwenye biashara hasara ya akina Salima Njaa Kaya na Ana Tamaa Nkapa ya NGO za uongo na ukweli. Nitamwambia bila woga kuwa bi mkubwa atamchafua kama Ana tamaa alivyomfanyia chinga fulani wakati fulani kwa kuendekeza njaa na uroho wa utajiri uchwara.
Nimalizie kabisa; nikishamaliza kikao chetu lazima nifanye kama magabacholi. Nitazisambaza kila mahali ili kila mlevi aniheshimu hata nikitaka anikatie mshiko afanye hivyo bila kusita. Tuonane wiki ijayo walevi wenzanguni. Atakayeudhiwa na kitu hii ajue yeye ni jipu.
Chanzo: Nipashe Jumamosi.

No comments: