Tuesday, 5 July 2016

Milioni saba kwa dakika; kijiwe chanena


            Baada ya vyombo vya umbea kuripoti jinai ya jizi moja kutengeneza madafu milioni saba hadi nane kwa sekunde, kijiwe kimekaa kutathimini baadhi ya mambo.
Mgosi Machungi analianzisha, “Jamani mnaona hii picha ya jizi toka umangani sijui ugabachoini inaotiibia kana kwamba hakuna siikai?”
Mijjinga anakula mic, “Unashangaa kuliwa wakati ushaambiwa  hili shamba la bibi lililokuwa likisimamiwa na kichaa kiasi cha kuligeuza kuwa kichwa cha mwendawazimu! Wala mie sishangai hasa nikiona magabacholi wanavyoshindana kuja kayani kusaidiana na wezi wetu kujihomolea.”
Kapenda anampoka mic Mijjinga, “Dokta Mijjinga nakubaliana nawe. Hii kaya kweli shamba la bibi lililokuwa likisimamiwa na chizi. Hujaona hata wachainizi wanavyojaa kuja kumalizia tembo wetu waliosalia baada ya wengine kusafirishwa umangani wakiwa hai? Umesikia amefungwa gendaeka hapa? Kwanini wasialikane kuja kufaidi vya bure?”
“Mwenzenu nilipomsikia Dk Kanywaji akitoboa uhalifu huu nilipandwa na presha. Kwanza, sikujua kuwa kumbe kaya inaliwa hivi. Pili, sikuamini kuwa Dk Kanywaji angegwaya kutaja jina la mheshimiwa mwizi huyu ambaye bila shaka anawakilisha mtandao wa wazito.” Anasema Mipawa huku akisogeza gazeti pembeni na kuendelea, “Mimi, hata hivyo, sishangai hasa nikiangalia miskandali kama Lungumi, Escrew na mingine inavyopigwa dana dana huku walioaiasisi wakiahidiwa ulinzi. Kwa taarifa yenu huyu jamaa atapotea kama alivyopotea Chavda baada ya wazito kuogopa kufichuliwa siri zao. Hii Danganyika ati.”
Mpemba anakula mic, “Yakhe mie nshangaa sasa. Sijui yawaje waloendesha serikali ilobariki ujambazi huu sasa wanaenziwa na hawa hawa wanaotufunga kamba kuwa watapambana na ufisadi wakati wanaonea wadogo na wale wasiokula nao? Huyu ntu angekuwa Uchina ashaoza baada ya kufilisiwa. Laiti kama Uchina wasingekuwa wana mizigo yao ya wasaka tonge wallahi mie ningehamia huko.”
Mzee Maneno anakula mic, “Mie mwenzenu niliposoma habari hii nilitamani kuchukua panga na kwenda kuua magabacholi japo mmoja.” Kabla ya kuendelea anamtazama Kanji ambaye naye anamtazama mzee Maneno. Kabla ya kuendelea, Kanji anamchomekea, “Dugu yangu siyo hindi yote mizi bana. Hii mbona maarabu na si hindi? Dugu yangu nakosea sana. Veve fikiri hii hindi na mizi nyingine naiba pekee yake. Kama vote natoka nje nakuwaje ijue vapi iko juluku ya kuiba? Iko Swahili mingi naleta hii mizi baba yangu. Kwanini nageuza hindi bata. Kuku iko kunya veve sema bata.  Hata kama iko hindi nasirika na Swahili kuiba, naonea hindi bure dugu yangu. Si hindi yote baka dugu yangu.”
Msomi anakula mic, “Nakubaliana nawe Kanji. Wizi mkubwa huu lazima uwe na wakubwa nyuma yake. Leo mnashangaa hivi vimilioni saba had inane. Je waliofunga mita ya mafuta walikuwa wakitengeneza bilioni ngapi kwa siku? Je walioruhusu mibwimbwi ijae na kupitishwa kayani hadi Bondeni wakanasa maguni walikuwa wakiingiza bilioni ngapi? Je watoto wa vigogo pale BoT wanaingiza bilioni ngapi kwa siku? Kama alivyosema Dk Mipawa ni kwamba kaya hii ni ya skandali na mali ya chizi. Mie nadhani hapa tunachopaswa kufanya kama wahanga ni kuingia mitaani kudai zirudishwe sheria za maadali ya utumishi na si utumiaji umma ili kila atakayekuwa anapata anachopata aeleze amekipata wapi.”
Anakunywa kahawa. Inamkwama na kukohoa sana kiasi cha kutoa machozi. Anaendelea baada ya kutulia na kusema, “Nakubaliana wanaosema kuwa hii ni dili ya wakubwa. Sitashangaa kugunduliwa ujambazi mwingine kama huu hasa ikizingatiwa kuwa wakubwa waliouwezesha wameahidiwa ulinzi na mkubwa ambaye amekuwa akitufunga kamba kuwa anapambana na ufisadi ili tupate maisha bora wakati anahangaisha wezi na mafisadi wadogo.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Kaka hapa umemaliza kila kitu. Hizi kama si kamba ni Sanaa kama kawa ndugu yangu. Huwezi ukapambana na vifaranga kwa kunya ndani wakati uko kitanda kimoja na jogoo yaani baba yao aliyewafundisha kunya ndani. Huu ni utani mbaya na jipu la aina yake. Sijui nani alitumbue iwapo mtumbuaji ameamua kulisamehe?”
Mbwamwitu aliyekuwa akisoma gazeti na kunong’ona na Mchunguliaji anakula mic, “ Kuna jamaa yangu wa usalama wa Kaya amenitonya kuwa mafisadi wakubwa watapeta hasa ikizingatiwa kuwa wapingaji wamepigwa pini wasiwaletee wenye maulaji yao kelele wala kuwawazidishia mbu. Hivyo, mjiandae kuliwa sana.”
Kabla ya kumaliza Mgosi anamkata jicho na kusema, “Kama kuiwa waiwe wao. Haiwi mtu hapa vinginevyo tutapigana zongo bue ohooo.”
“Hakuna cha zongo wala nini. Kama zongo kawapige hao mafwisadi wanaoendelea kutufilisi wakisaidiana na wezi wetu wa kuzaa wenyewe. Mbona zongo lako hilo hujawapiga akina Escrew, EPA, mzee wa Vijsengi, Lungumi na majambazi wengi bila kumsahau mwanaharamu Kagoda na washitiri wake wa Richmond waliomtosha zigo lao Eddie?”
Mpemba anakula mic tena, “Yakhe umekumbusha. Haya mambo ya kupigana zongo hayatosaidia kitu. Dua la kuku halinpati mwewe ati. Tuamue tufanye kitu hasa kuisulutisha sirikali itusikize badala ya kutegemea maamuzi ya ntu mmoja eti kwa vile tulimpa madaraka. Yeye awatumbua wenzie tena kwa kunchagua atakaye. Je yeye nani antumbua?”
“Ami sasa inaonekana hujitaki. Unaanza hata kuwashuku watakatifu na wenye vifua wakati weshasema hakuna wa kuwashauri kwa vile wao wanajua kila kitu?” anachomekea da Sofia huku akiweka rinda lake vizuri kichwani.
Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita mkewe na jambazi wa bilioni saba. Acha tumtoe mkuku ili tumfanyie kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: