Saturday, 23 July 2016

Makufuli tumbua wachunaji

Image result for photo of gwajima na helkopta
            Juzi nilisika saka saka ya mchunaji mmoja anayejiita mchungaji akiihangaisha sirikali. Wabongo kwa kukuza mambo, hakuna mfano. Kwani, mchunaji mwenyewe punde si punde si alijitokeza. Wacha ndata wamzukie waishie kumgwaya. Kwani, tumepashwa kuwa alikwenda pale kituoni kama mtu anayekwenda mgahawani kupata chai na kuishia zake kwenye hekalu lake ambalo nalo hatujui alivyolijenga. Kwa kazi gani au ni kwa kutumia sadaka?
Huyu jamaa ambaye alijizolea umaarufu baada ya kumpa tafu Eddie Luwasha kwenye uchakachuaji uliopita ameniacha hoi baada ya kumkana na kujifanya anamzimii dokta Joni Kanywaji Makufuli. Ya kweli haya au ni janja ya kusaka ulaji ukiachia mbali kuogopa asitumbuliwe usawa huu anapomilki chopa bila kueleza wala kuonyesha alivyochanganya njuluku hadi akawa bonge la mkwasi ghafla bi vu? Kwa jeuri aliyoonyesha si haba. Who knows. Huyenda naye ana sirikali yake yenye siri kali kubwa kiasi cha ndata kumgwaya. Au ni kwa vile amejitoa kwenye upingani; hivyo, matamshi na tabia zake havihatarishi amani ya walaji wakubwa kayani? Bahati yake, angekuwa bado kitanda kimoja na Ewassa huenda hata hiyo chopa na hekalu vingekuwa vimeishanyakwa baada ya kutumbuliwa.
Ngoja niulize kibangibangi na kigongongo. Je huyu jamaa huwa anafanya kazi gani zaidi ya uchunaji? Hata hivyo sishangai. Baada ya neno la Bwana kugeuka bidhaa adimu ambayo kila tapeli anaweza kutumia kuukata, who knows hata kama uchunaji ni joho tu la kufichia biashara nyingine kubwa? Huoni wanavyoibuka wachunaji kila uchao hadi wengine kumuingiza nkenge Dokta Kanywaji hadi akawazukia kwenye maduka yao? Juzi nilinusurika kuzimia baada ya kusikia wachunaji wengine eti wakiandaa mkutano mkubwa wa kuombea kaya kana kwamba kaya inahitaji kuombewa badala ya kuambiwa ukweli kuwa ni shamba la bibi na kichwa cha mwendawazimu cha mzee Ruxa tulichokiona wakati wa Njaa Kaya na genge lake la ulaji na uzururaji. Tumekuwa na wanene wabovu kiasi cha kufuga mijizi ambapo kaya ilikuwa kwenye outpilot kila mchovu akijifanyia atakavyo. Hata hivyo, chini ya rahis Kanywaji, nina imani mambo yatabadilika kama hawatambadilisha kabla hajawabadilikia na kuwabadilisha.
Siku hizi si ajabu kuona wachunaji wakipanda mingoma mizito na kuishi kwenye mahekalu wakati yule bwana mkubwa wanayemhubiri alikuwa apeche alolo akiombaomba. Rejea Kaisari alipomtakisha kodi. Si alikuwa amewaka kiasi cha kuikopa njuluku kwa samaki? Sasa hawa wachunaji wanapata wapi hii ya kuwa matajiri wakati Yesu mwenyewe alisema kuwa ni heri ngamia kupita tundu la sindano kuliko wakwasi kuingia kwenye ufalme wa God? Msiseme nazusha. Hamuwaoni walivyo na mimali lukuki isiyo na maelezo?
 Linapokuja suala la watu kuwafisidi na kuwaibia wachovu, kaya yetu inaweza kuwa kinara. Hata hivyo, bwana mkubwa aliwahi kusema, “Macho wanayo. Lakini hawaoni. Masikio wanayo. Lakini hawasikii.Wengi wa wachunaji hata ukiona sura zao ni wababaishaji wa kawaida tu waliojificha nyuma ya majoho na madhabahu wakinajisi na kuibia wachovu wa God. Kwanini wachovu wanashindwa kuelewa kitu simpo kuwa; huwezi kutumikia mabwana wawili yaani bwana God na ukwasi ukauona ufalme wake. Kinachowapa ulaji ni ile hali ya wachovu na walevi kumsahau baba yao Kibwetere aliyewabwetere kondoo kwa kuwatia nari na kuondoka na mali zao. Japo nisemayo ni ya kilevi na bangi, sitashangaa kusikia Kibwetere mwingine akiibukia Bongo muda si mrefu. Chukulieni hili kwa makini. Kwani ni utabiri swaafi wa nabii wa walevi.
Wengi wamefikia hata kujiita mitume na manabii wakati ni mitumba na majangili. Hivi anaweza kupatikana mtume au nabii usawa huu kwenye dunia ya walafi na mafisi na mafisadi ambapo mali imechukua nafasi ya God siyo? Mara hii mmesahau aliyenaswa na nyara za umma akijifanya mchungaji wakati ni jangili. Ni manaigeria mangapi walishanaswa na bwibwi huku wakiwa wamevalia kama wachungaji wakati ni wachunaji na wasafirisha bwibwi? Wengine wanajiita watu wa Mungu wakati ni watu wa unga. Ukiangalia biashara fichi ya wachunaji, mbali na wengine kutumia misamaha ya kodi kuingiza bidhaa za wafanyabiashara wezi, kuna kila sababu ya kuamini wana biashara nyingi haramu nyuma ya pazia. Hapa hujagusia michango wanayowatwisha mbumbumbu wengi wenye matatizo na wizi wa sadaka.
Hata hivyo, hawa wachovu wajinga na wapumbavu wana bahati. Kama si mlevi kuwa mcha God, angeweza kuanzisha dhehebu lake la Ufufuko na Utajirisho ili awaibie mchana kweupe kama wanavyofanyiwa na matapeli tena wengi ambao hawakupiga buku kama mimi. Kwa elimu yangu ya saikolojia–kama ningeamua kuwaibia ningekuwa tajiri–kutokana na kuwachezea kisaikoloji. Jitu linatoa mimba linaishia kushindwa kupata mtoto eti linakwenda kuombewa baada ya kutapeliwa na waganga wa kienyeji wanaoishia kulibaka. Kama haitoshi, jingine linaolewa na kushindwa kutunza ndoa yake. Mambo yakiharibika linakimbilia kwa wachunaji. Kimsingi, kinachoendelea kayan–licha ya kuwa ushirikina na wizi wa mchana–ni zao la kukosa kujiamini na kukabili matatizo kama yalivyo. Kimsingi, wachunaji na waganga wa kienyeji tofauti yao ni majina. Sitashangaa siku moja–baada ya kuzoea kuona wachunaji wakibambwa na bwibwi–kusikia kuna wachunaji wamenaswa na viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi. Anyways guys, msinichukulie seriously kwa vile nimeutwika leo. Muhimu, Makufuli anapaswa kuwatumbua hata wachunaji.
Chanzo: Nipashe Jumamosi.

No comments: