The Chant of Savant

Sunday 31 July 2016

Je uraia wa nchi mbili ni kwa wageni tu Tanzania?


Japo watanzania wamekuwa na mawazo na misimamo tofauti kuhusiana na uraia wa nchi mbili, kitu kimoja kiko Dhahiri; sheria ya Tanzania hairuhusu raia yoyote wa Tanzania kuwa na uraia wa nchi mbili. Rais Magufuli–sawa na watanzania wengine analijua au anapaswa kulijua hili–hivyo alichosema si kuteleza kwa ulimi wala utani. Hata hivyo–hivi karibuni katazo hili la kisheria lilionekana kuwa la kibaguzi–tokana na ukweli uliofichuliwa na rais John Pombe Magufuli. Akimkaribisha mgeni wake waziri mkuu wa India Narendra Modi aliyetembelea Tanzania hivi karibuni, rais Magufuli alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Amejisikia [Modi] raha sana; alivyoona anakaribishwa na wananchi wengi wa Tanzania ambao naamini katika wale waliomkaribisha wengine ni miongoni mwao waliompigia kura kwenye jimbo lake.” Maneno haya yanajifafanua hasa ikizingatiwa kuwa kwanza, Modi si mtanzania–ni mhindi tena kiongozi wa nchi–hivyo, kwa sheria ya Tanzania, hawezi kuwa na wapiga kura. Pili, kwa mujibu wa rais, Modi–pamoja na sheria za Tanzania kukataza–anajua kuwa ana wapiga kura nchini hata kama ni kinyume cha sheria. Tokana na ithibati ya rais wetu ambaye mara nyingi amekaririwa akieleza wazi anavyochukia unafiki na uongo, aliyosema ni ya kweli tupu na si unafiki wala kufurahisha genge. Pia, tokana na ukweli huu na uzoefu wa watanzania walio wengi hasa wa mijini, unaweza kujenga mahitimisho na kugundua ni kwanini:
Kwanza, wengi wa mafisadi wakubwa wanaoshirikiana na mafisadi wakubwa wazawa serikalini ni wahindi.
Pili, wahindi wamekuwa wakiwabagua waafrika kwa miaka yote waliyokaa Tanzania bila kushughulikiwa kwa vile wana haki zaidi ya wazawa.  Hatutaki kutoa madai bila kutoa ushahidi. Kwa miaka zaidi ya mia waliyokaa Tanzania, nionyeshe ndoa hata tatu baina ya waswahili na wahindi nitaondoa hoja hii na kuomba msamaha. Najua ukweli huu ni mchungu. Lazima usemwe ili tuweze kusonga mbele kama taifa baada ya kujisuta na kusutana kama watanzania bila kujali rangi ya ngozi zetu. Isitoshe mie si wa kwanza kuliona hili. Marehemu Christopher Mtikila aliliona na kuliongelea sana na kwa undani bila woga wala unafiki. Nanachofanya hapa ni kukumbusha tu ili kuondoa kuendelea jinai ya ubaguzi.
Tatu, waziri mmoja wa uchumi wa zamani aliwahi kusema kuwa uchumi wa Tanzania ulikuwa–kipindi fulani–unashikiliwa na wahindi kumi tu. Hili ni kweli. Kwanza, wahusika hawakukanusha na ukweli unaonyesha hivyo.
Nne, matajiri wengi nchini ni wahindi hasa ukiangalia uwiano wa idadi ya watu. Kama hii haitoshi, wengi wa matajiri hawa wanaishi kwenye nyumba za msajili wa majumba kwa bei nafuu wakati wana mahekalu yao wakiyapangisha kwa dola au wana uwezo wa kujenga majumba yao wenyewe.
Tano, Tanzania imeruhusu jamii hii kuwa na shule, dini, na shughuli nyingine za kibaguzi za jamii moja ukiachia mbali kubariki mfumo wao wa kikaburu wa kitabaka (caste system) ambao licha ya kuwa wa kibaguzi ni kinyume cha sheria na haki za binadamu.
Sita, rais alisema kuwa Bunge la Tanzania lina wabunge kumi wenye asili ya kihindi, jamii ambayo hivi karibuni imesifika kwenye vyombo vya kimataifa kwa kuwabagua waafrika ikiwaita nyani au absii, bander au kalu. Rejea kupigwa na kudhalilishwa vibaya kwa mwanafunzi wa kitanzania nchini aliyekuwa akisoma kwenye Chuo Kikuu cha Acharya, Bangalore, India hivi karibuni baada ya msudani mmoja kusababisha ajali ya barabarani bila kutaja mwanafunzi toka DRC Masunda Kitada Oliver aliyeuawa May kwa kugombea Bajaj.
Kweli usilojua ni usiku wa kiza. Sijui kama waswahili wangekuwa huko ugabacholini wangepewa hata ujumbe wa nyumba kumi chini ya mfumo wa kikaburu wa caste system. Ni bahati mbaya kuwa waswahili walifundishwa kujikana na kuwapapatikia wageni kiasi cha kuwa na methali isemayo mgeni karibu mwenyeji apone kuonyesha utegemezi na kutojiamini kwao. Walevi wana shaka na huu ushuhuba wa ajabu ajabu ambao haulengi kutatua matatizo kama vile utoroshaji raslimali zao, ubaguzi wa moja kwa moja tena wa muda mrefu na madudu mengine mengi ambayo tawala karibia zote zimekuwa zijifanya haziyaoni. Wenzetu husema charity begins at home, au hisani huanzia nyumbani.
Tumalizie hapa kwa kumtaka rais Magufuli na serikali yake ima kuruhusu uraia pacha au kuupiga marufuku kwa watanzania wote badala ya kubagua hata kusifia ubaguzi huu. Sheria ni msumemo kama ambavyo rais Magufuli hupenda kusema; haipaswi kubagua wala kupendelea, kutumika kibaguzi au kuwa utashi wa mtu, kikundi cha watu wala taasisi bali utashi wa sheria. Ni aibu kugundua kuwa taifa huru linaweza kuwanyima raia wake wazalendo na kuwaruhusu raia wa kigeni wautumie kuliibia. Je yote haya yanafanyika hivi kwa faida ya nani? Sijui kama India inaweza kuruhusu ujinga kama huu tena kwa waafrika ambao wanasifika kwa wanavyobaguliwa nchini India hata kwenye bara lao wenyewe kutokana na kuwa na uongozi wa kifisadi na usiojithamin kukosa uzalendo na kujiamini.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili.

4 comments:

Anonymous said...

Salamu Mwalımu Mhango,
Niweke kando kwanza kuhusu hii kadhia ya uraia pacha pamoja na umuhimu wake ulivyo kwa wananchi wa Tanzania kuweza kupewa haki hiyo kama ni haki ya kitabia baada ya dunia kubadilika na kuwa ni kijiji kimoja.

Tatizo kubwa Mwalimu Mhango,ni sisi waafrika kuwa vıctims kutoka kwa watu wengine wote duniani wasiokuwa waafrika.Mwarika huyu nje ya Afrika ni mwenye kunyanyaswa.kudhalıshwa na kuonekana kwamba astahiki kuwa na sifa za mwanadamu kamili,na hatimae mwafrika huyu kana kwamba ameikubali hiyo na kujıtahidi kwa kadri anavyoweza kuukataa uafrika wake,mila na desturi zake na hata dini yake.

Mwalimu Mhango,Kadhia ni utumwa wa kiakili na utamaduni wa kitumwa na kwetu sisi waafrika wa Bara Mama hali yetu ni mbaya zaidi ya kuukubali utumwa huu wa kiakil na utamaduni huu wa kitumwa kwani sisi waafrika wa Bara Mama tunachopıganıa daima ni kujınasibisha na wale wote waliotusababishia huu utumwa wa kiakili na utamaduni wa kitumwa.Sisi waafrika wa Bara Mama ndio ambao tunaoinua bango la "FORGIVE AND DO NOT FORGET".Swali linalojiuiza hapa kwa nguvu ni hili,kwa nini tu ni sisi waafrika ndio wenye kusamehe na pia ni wenye kusahau?

Anonymous said...

Tunawasamehe na kuwasahau wale ambao waliotuathiri kwa kutufanya watumwa na hadi hii wanaendelea kutufanyia utumwa mambo leo,tunawasamehe na kuwasahau wale ambao wametukoloni na bado wanaendelea kutukoloni ukoloni mambo leo na hatimae ni sisi wafrika ndio tumeaamua kuwa walinzi wao wa utajiri wetu ambao wananufaika nao kuliko sisi wenyewe waafrika na dio sisi tunaopigania masilahi yao kwa kila njia na ya kila aina likiwemo hili la hata kupewa wao uraia pacha ıli wazidi kuyalinda masilahi yao kwa kadiri iwezekenavyo.

Mwalimu Mhango.endapo hukulelelewa au kujengewa tangu udogo hisia ya kujifaharia taifa lako,uafrika wako.rangi yako.dini yako,na mila desturi zako kamwe hautokuwa mwenye kutambuliwa na kuheshimiwa na watu wengine.Je Mwalimu Mhango.umeiona Tanzania ya leo ya wanasiasa wetu wakiwaamkia wananchi wao katika majukwaa ya kisiasa na ya kıjamii maamkizi ya dini za kigeni Asalaamu Alaykum.Na asifiwe Bwana.Tumsifie Yesu Kristo?Hivi ni kweli tumefelisika kwa kiasi hiki hata yakawa maamkizi ya kidini kuwa ndio maamkizi yetu katika siasa na katika mahafali ya kijamii?Kwa nini maamkizi hayo yasibaki tu misikitini na makanisani?Namalizia kwa kuandika kwamba kuna hizi power za nje zinazofanya kazi nyuma ya pazia zikishirikiana na wengi wa viongozi wetu wa Kiafrika kuhakisha kwamba masilahi ya wageni wa race isiyokuwa ya kiafrika yanatetewa hadi mwisho wa dunia na kama kiongozi wa kiafrika atakwenda kinyume cha hayo atawekewa mibiginyo yote stahiki kwake na watu wake lumumba,ıddı Amını na hatimae Mugabe ni mfano hai.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Hata kama nimechelewa kujibu kutokana na kutingwa na majukumu, nakubaliana na nyingi ya hoja zako zenye mashiko. Hata hivyo, kama tutaangalia ukweli wa mambo, ni kwamba taifa letu na Afrika kwa ujumla iko utumwani chini ya ukoloni mamboleo anbapo kujikana kumegeuka fasheni. Siwashangai wanaotumia salamu za kigeni kutokana na ukweli kuwa wanaonyesha wao ni nani. Asiyevuta kamba nasi si mwenzetu. Hawa -hata kama wamesoma -ni waathirika ambao kuwatofautisha na wajinga sipati. Ni bahati mbaya kuwa tumefundishwa kujikana na kujitukana huku tukitetemeka tunaposhauriwa kuasi utumwa huu wa kiakili na kimwili. Walipoleta mila zao wakaziita dini, wakabadili majina yetu na kutupa yao kama mbwa, tulipoteza kila kitu. Hivyo, tunachopaswa kufanya -kwa wale wanaojitambua -ni kuasi na kuendelea kupiga kelele. Huenda kuna wachache tutawaokoa na kuwaongoa.
Kwa ufupi hayo ndiyo mawazo yangu; pia nakushukuru kwa mchango wako adhimu na adimu.

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,
Najuwa fika kabisa kwamba wakati wako upo finyo kiasi gani lakini cha kushukuru tu kwamba kuwapa umuhimu na kutowapuuza wasomaji wako pale wanapotoa machango wao wa kimawazo hata ikiwa kwa uchache kiasi gani,hili linatupa moyo na nguvu sisi wasomaji wako kuweza kukufuatilizia na kukusoma.Sisi wengine kutokana na pilika pilika na majukumu ya kimaisha katika ulimwengu wa tatu kama unajvyojua tunakuwa hatuna wasaa wa kutosha wa kuweza kuwa karibu na matandao mara kwa mara,lakini ikitokea tu kupata nafasi tunaitumia nafasi hiyo katika kukusoma na kama kuchangia maoni tunakuwa hatusiti kufanya hivyo,

Tunamuomba tu Mwenyezi Mungu akupe uhai mrefu ukiambatana na afya njema ili uzidi kupandikiza mbegu za mawazo ambayo mimea na miti yake watafaidika nayo kizazi kijacho na kujiuliza kwa nini kizazi cha wakati wako hawakufaidika na mimea hiyo na miti hiyo.kwani kizazi chetu hichi tumekuwa wavivu wa kujisomea na kushiriki katika changamoto za kuchangia mawazo baki salama na kila kheri.