Sunday, 31 July 2016

Mlevi atamani kufanya biashara na NSSF


            Kwanza, nimpongeze rafiki, kaka yangu na msomaji wangu rahis Joni Kanywaji Makufuli kwa kuwatumbua walaji wa Shirika la Utafunaji wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii au Nominal Social Syndicate of Fraudsters (NSSF) baada ya jamaa kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa. Nampongeza kwa kupewa rungu na nambari wani kuwatumbua majipu yote hata kama ni yale yaliyomkabidhi rungu lenyewe. Nasema bila kumung’unya “Tumbua Kaka.” Nashauri hata kauli mbiu yako ibadilishwe na kuwa “Hapa Kazi na Kutumbua Tu” au siyo? Ila katika kutumbuatumbua angalia usinitumbue mimi. Ukifanya hivyo utakosa ushauri na inshu. Hivyo, nakupa greenlight utumbue kila jipu isipokuwa mimi ambaye ujipu wangu ni wa kupiga mma na kuchoma jani. Pia naomba unikumbuke kama Lyatongolwa  najikomba kwako ding.
Baada ya kumpongeze mnene kupewa rungu ambalo–sina shaka–atalitumia bila huba, upendeleo wala uonevu kuwashughulikia walogeuza kaya shamba la chizi chini ya Jk, sorry, Njaa Kaya.
Hivi karibuni aliwatumbua vigogo wa NSSF tokana na ujinga na uroho ambao hata fisi–pamoja na uroho wa kupindukia–kusema ukweli, hana.  Mnakula hata nyayo wanahizaya nyie msie na aibu wala adabu! Shame on you! Sasa mtakoma na kukomaa. Hapa lazima Dokta Kanywaji afe na gendaeka. Hivi kweli unaweza kuamini; kiwanja kilichopaswa kununuliwa kwa madafu bilioni moja na nusu kilinunuliwa kwa madafu bilioni 15? Ukisikia kiwanja chenyewe unatamani ukamate gendaeka uwafanyie kitu mbaya. Hebu fikiria. Kiwanja Bongo, tena madongo kuinama, kinapunyua madafu bilioni zaidi ya 15 za walevi wanaonuka umaskini wa kutengenezewa na watawala washenzi na wapuuzi kama tulivyowashuhudia hivi karibuni Dk Kanywaji akiwananga kuwa waliachia kaya ikaliwa kama haina mwenyewe. Wakati mwingine unashindwa kuielewa miswahili.  Mijitu inakula hadi mapembe na kwato? Mbona hata Tokyo–kule Ujep na New York kwa Joji Kichaka na Obamiza–ambako viwanja ni aghali kuliko vyote duniani bei haijafika huko? Unashangaa kusikia eti hawa nao eti ni wasomi kweli? Tokana na sakata hili, Mlevi apanga kuonana na rahis Dk Kanywaji–si kujikomba kama Lyatongolwa–kumtaka abatilishe uteuzi wa aliyekuwa bosi wa wizi huu wa mchana aliyemteua balozi. Huyu alipaswa kuwa Keko lakini si zaidi. Anapewa ubalozi wa nini wakati mchezo wake mchafu ndiyo umefumka? Au Dk Kanywaji alipompa ubalozi alikuwa hajapata hili jipu alilotumbua hivi karibuni? Nalo hili nikipata appointment naye nitalipenyeza ili jamaa aende zake lupango akajiunge na wenzake.
Pia, nitamuomba Makufuli ima aniteue kuwa mnunuzi wa mali za NSSF; au niwe muuzaji kwake ili nichanganye njuluku hasa kutokana na kugundua kuwa kumbe kuna fursa za kutengeneza ukwasi kama sina akili nzuri.  Hapa uhitaji kutumia akili. Kinachotakiwa ni kutembeza hongo.  Kwa vile mimi ni msomi wa kweli na mzalendo tena muaminifu, nitakula kidogo na kubakiza kikubwa tofauti na hawa waliokuwa wakiiba kikubwa na kidogo ukiachia mbali kupokea chochote kile katika ujambazi huu wa mchana.
Kwa vile wizi wa mabilioni na matrilioni umezidi kayani, nitamshauri Dk Kanywaji afanye utaratibu wa kupeleka mswaada bungeni wa kuhakikisha wanaokwapua mabilioni na matrilioni wananyongwa sawa na majambazi wa kawaida.  Pia, nitashauri wahakikishe wahusika wakimatwa wasihukumiwe kifo chapchap. Waachwe; kwanza wasote lupango ili ndugu zao wawaletee habari chafu na chungu za washirika zao wa bedroom kuwa na washikaji wapya wa kuwadoadoa. Kwanini wasipate habari chafu wakati wao wameumiza walevi wengi kwa kuhomola njuluku zao?  Lazima hapa wafanyiwe kama akina Hasi Kitiliya, Sirori na Sinari. Unadhani washirika zao huko nje wako salama?  Bahati yao, niko mbali nao, nami ningetia timu kuwabugulia mali zao kama walivyobungua mali zetu. Tena, nilivyokuwa mnoma, usishangae wengine nengewaachia mbegu za walevi kwenye uzao wao ili wanikumbuke milele. Japo si vizuri kumuombea mja maafa, wahanga wa ushenzi huu wanaomba hawa jamaa wanyotoke roho haraka kama lile jambazi la Banki Kuu lililozikwa hivi karibuni kule Moro. Siku hiyo walevi tulikunywa na kuvuta kama hatuna akili nzuri.
Katika kuhakikisha njuluku za walevi hazipotei, napanga kumshauri Makufuli akamate mali za wahusika haraka kabla hazijatobolewa tobolewa na washirika wao. Pia, ahakikishe yule aliyeuza kiwanja kwa mabilioni haya naye anaunganishwa haraka kabla hajatorokea ughaibuni kama ilivyo fasheni ya baadhi ya washirika wa jinai hii hasa wenye uraia wa kaya nyingi.
Pia nitamshauri Dk Kanywaji kuchunguza gharama za ujenzi wa Daraja la Mzee Mchonga pale Kigamboni. Maana, kama wezi hawa wameweza kupaisha bei ya kiwanja, hilo daraja itakuwaje? Kwanza, mwenzenu nilishaapa kuwa sitakaa nipite kwenye daraja hilo kuelekea Mji Mwema. Kwa vile hii ni kaya ya kitu kikubwa na kidogo, nina wasi wasi limejengwa chini ya kiwango kama mighorofa mingi ya Bongo inayongoja kunyotoa walevi roho kama ule wa Uhindini.
Ama kweli Njaa Kaya alijua kututenda! Ajabu eti bado anakingiwa kifua. Achia rungu la ukiti utumbuliwe na wenzako. We ngojeni. Hawa wa NSSF walie tu. Lazima walipe;maana kula na kulipa ndiyo mwendo wa usawa huu.
Chanzo: Nipashe Jumamosi

No comments: