The Chant of Savant

Saturday 16 July 2016

Tulia Ackson anapaswa kutulia

            Pamoja na kwamba uhuni Bungeni haukuanza jana–hasa kiti cha Spika kinapotumika vibaya kwa sababu binafsi au za kisiasa–Bunge la 11 linaweza kuvunja rekodi katika baadhi ya mambo tena yasiyopendeza wala kukuza demokrasia nchini. Zamani uspika ilikuwa ni taasisi yenye kuheshimika sana nchini; hasa ikizingatiwa kuwa ni moja na mihimili mitatu ya dola. Bunge linapaswa kuwa huru bila kuingiliwa au kuingilia mihimili mingine ya dola. Hata hivyo, baada kuingia ushindani wa vyama vingi, Uspika ulianza kugeuzwa sehemu ya utawala jambo ambalo ni kuupunguzia heshima na kuuingilia mhimili huu kati ya tatu ziundazo dola yaani Bunge, Mahakama na Utawala.  Hili si jambo jema kwa taifa hasa Bunge linapofikia mahali ukawa ni uwanja wa kulipiziana visasi kisiasa na kiutendaji.
            Dhana nzima ya kuwepo Bunge ni kutaka kutoa fursa ya mihimili ya tatu kutekeleza wajibu wake ambao kwa Bunge ni kupokea miswaada ya sharia, kuipitisha, kutunga, kurekebisha na kufuta sheria kunakofanywa na wabunge wanaowawakilisha wananchi moja kwa moja.  Baada ya hivi karibuni baadhi ya Wabunge wa kuteuliwa–tena na wakuu wa dola–ambao Spika wa zamani Samuel Sitta aliwahi kuwaelezea kama mizigo kuweza hata kuruhusiwa kugombea uspika au unaibu Spika japo hawamwakilishi yeyote zaidi ya matumbo yao na aliyewateua, ithibati ya Bunge imeanza kushuka au kupotea kabisa. Hali ya Bunge inakuwa mbaya pale inaposimamiwa na mtu au watu wasiotokana na kura za wananchi na badala yake wakateuliwa kirahisi tu. Kwani–mbali na kutowakilisha umma–wahusika hawajui machungu na mikiki mikiki ya kuupata Ubunge. Hivyo, wanaweza kutumia nyadhifa zao watakavyo ima kujiridhisha au kuwaridhisha waliowateua kama ilivyo sasa ambapo ukada na unazi vinaanza kuzoeleka Bungeni tangu kuchaguliwa kwa naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
            Hata hivyo, Uspika si sehemu ya kuonyesha ukomavu, uongozi na uzalendo na si mabavu, ubabe wala upendeleo; bali kutenda haki hasa nafasi hii inaposhikiliwa na mtu anayejinakidi kuwa na shahada ya uzamivu katika masuala ya sheria. Inashangaza mtu mwenye kuitwa daktari wa sheria kushindwa kumaizi jambo rahisi kama hili. Je tatizo hapa ni busara, elimu za kuungaunga au uzoefu?
            Kwa wanaoujua thamani na umuhimu wa elimu, wengi walidhani daktari huyu wa sheria angejua umuhimu wa elimu; hivyo, kuonyesha umahiri wake katika kusimamia na kukuza demokrasia badala ya vurugu na kuiminya demokrasia. Hata hivyo–tokana na kadhia tulizoshuhudia ambapo naibu Spika wa Bunge Dk Ackson akionyesha wazi kulalia upande mmoja wa Utawala na kushindwa kujitofautisha na Spika aliyepita Anna Makinda aliyesifika kwa uburuzaji tokana na alivyopatina na kiwango chake cha elimu, wakati mwingine tunashindwa kuwatofautisha wawili hawa japo wana viwango tofauti vya elimu.
            Wengi waliofuatilia vikao vya Bunge na wingi wa Wabunge wa upinzani walioadhibia kwa kuzuia kuhudhuria vikao wanajiuliza: Je tatizo ni Wabunge au naibu Spika? Pamoja na udhaifu wake, mbona wakati wa kipindi cha Makinda, Wabunge hawakuadhibiwa kwa wingi na mfululizo kama ilivyotokea hivi karibuni? Ukiangalia utendaji wa Bunge kwa vipindi mbali mbali vya karibuni kuanzia uongozi wa mzee wa Viwango Samuel Sitta ambaye alikuwa pia mwamanasheria, watakubaliana nasi kuwa Wabunge wengi hasa wa upinzani wameadhibiwa kipindi Dk Tulia alipoendesha Bunge baada ya Spika kuwa nje kwa matibabu tena ndani ya muda mfupi.
            Makinda aliwasimamisha  Wabunge Tundu Lissu (Singida Magharibi), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiah Wenje (Nyamagana) mnamo  tarehe 18, April 2013.
            Ackosn amewasimamisha wabunge Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe, Tundu Lissu (Singida Magharibi, Godbless Lema (Arusha Mjini), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Esther Bulaya (Bunda Mjini). Mei 2016.
 Suzan Lymo (Viti Maalum) na Anatrophia Theonest (Viti Maalum) Juni 2016
Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Saed Kubenea (Ubungo) na James Milya (Simajiro) Julai 2016.
            Ukiangalia mfuatano, ni kwamba, karibuni kila mwezi Ackson alikuwa akifukuza wabungu kwa wastani wa wabunge wanne au mbunge moja kila wiki. Je hapa tatizo ni Wabunge au naibu Spika mwenyewe? Mbona huko nyuma hakuwahi kutokea? Kimsingi, Ackson ataingia kwenye historia ya vitabu vya bunge kama mtu aliyekalia kiti cha Spika na kuvunja rekodi–si ya kufanikisha bunge–bali kuwatimua Wabunge wa upinzani. Je huu si ukada wa wazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho wakubwa zake nao wana rekodi ya kumteua kwa vyeo tofauti ndani ya muda mfupi? Kama Ackson ana mapenzi na ukereketwa wa chama chake hivi, si aende akafanye kazi za ndani ya chama badala ya kuaminiwa wadhifa wa kitaifa ambao ameonyesha kuutia aibu ukiachia mbali kutumia vibaya kiti cha spika?
Tumalizie kwa kumtaka Dk Tulia kutulia na kuonyesha ubobezi wake  katika sheria na si kufanya vinginevyo jambo ambalo linalishushia heshima Bunge naye binafsi kama msomi na kiongozi wa umma. Unapofukuza wabunge–licha ya kuwanyima wananachi uwakilishi–ni kuwafukuza wananchi kwenye chombo chao.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili.

No comments: