Thursday, 7 July 2016

Hapa Dokta Magufuli akubali ameteleza


Hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli aliwashangaza, kuwazodoa, kuwanyamazisha na kuwachanganya mengi ukiachia mbali naye kujichanganya. Akipokea ripoti ya uchaguzi mkuu wa 2015, Magfuli aliwamua–kwa makusudi kabisa–kufyatua kombora lake la kwanza lilioacha mashabiki na wapenzi wake wakigawanyika na wengine kuanza kutia shaka spirit na sincerity ya juhudi zake za kupambana na ufisadi. Hii ilitokana na kutoa hakikisho kwa watangulizi wake dhidi ya kashfa mbali mbali zinazowakabili kiasi cha baadhi ya watanzania kutaka wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.
 Magufuli alikaririwa akiwaambia marais wastaafu hawa akisema, “Wala usisikilize kelele nyingine hizi za ovyoovyo. Wewe uko salama na hilo ndilo jukumu langu kama Rais wa Awamu ya Tano kuhakikisha viongozi wote wastaafu wako salama.”  Sijui hapa tuamini nani kati ya katiba na rais? Maana, wajibu wa kumlinda kila mtanzania bila kujali cheo chake ni wa katiba na watanzania wote bila ubaguzi wala upendeleo. Pia marais wastaafu wana kinga kikatiba na si kwa matakwa wala hakikisho la rais. Rais anapata wapi mamlaka ya kuwalinda marais wastaafu? Je hii haiwezi kutafsiriwa kama rais kujiweka juu ya sheria jambo ambalo linapingana na matakwa na matarajio ya waliomchagua?
 Kuzidi kuwatoa hofu aliowaita wazazi wake hofu–pamoja na mengine mengi–Magufuli aliongeza, “Mjue mimi mtoto wenu nipo. Watachonga lakini nataka kuwahakikishia mtaishi kwa amani. Mengine hata mkiyasikia, tupa pembeni kwa sababu mimi ni kiongozi wenu mwenye jukumu la kuliongoza Taifa hili nipo pamoja nanyi.” Je Magufuli anadhamiria kufanya hivyo–huku akijua ni kinyume cha kiapo chake cha kuwatendea kwa usawa watanzania–au alikuwa anatafuta kuungwa mkono kwenye mchakato wa kukabidhiana uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulikokuwa kumeanza kuzua utata ukiachia mbali kukwama hata kutokea shutuma za kukwamishana kwa kuogopa kutumbuana? Je Magufuli alikuwa anatania au ulimi uliteleza? Maana Magufuli aliapa kulinda na kutekeleza katiba ya nchi bila upendeleo, huba wala chuki.  Wapo wanaohoji anakopata uhalali, jeuri na nguvu ya kusema haya aliyosema Magufuli. Je anayepaswa kusamehe mtu makosa yake zaidi ya mahakama ni nani nchini? Kama watanzania wanataka wahusika washitakiwe, yeye ni nani au anataka kuifanya Tanzania mali yake binafsi?  Tundhani ni busara rais awasikilize wananchi wanataka nini na si yeye anataka nini; vinginevyo akiri kuwa yuko madarakani kuwatumia na si kuwatumikia wananchi.
 Wakosoaji wake wanaona kama Magufuli anaufanya urais wake kuwa urithi na si dhamana aliyoaminiwa na wananchi anaoanza kuwapiga teke sasa akikumbatia wale waliowanyonya na kuwaongezea umaskini kwa sera mbovu na kuendelea kulipwa marupurupu makubwa na lukuki wakati wengine hakuna walichofanya zaidi ya kuliangamiza taifa kiuchumi. Tunadhani rais hana haja ya kuwapa silaha wakosoaji na wapinzani wake kwa kujiingiza kwenye siasa za kulindana ambazo ni kinyume cha katiba na ahadi alizotoa kwa watanzania kuwatumikia bila ubaguzi wala upendeleo. Rejea maneno ya Magufuli mwenyewe ambaye amekuwa akiwatuhumu watangulizi wake kuridhia utapeli kama vile wafanyakazi hewa, kutofunga mita ya kupima mafuta yanayoingia nchini, kutwaa mali za umma kama vile Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, UDA, Escrow na kashfa nyingine nyingi. Ni kama Magufuli anaanza kujichanganya, kuwachanganya wananchi na kujipiga mwenyewe.
Wapo wanaoona kama rais anaanza kuwasha moto ambao hawezi kuuzima hasa wakati huu ambapo taifa lipo msambweni baada ya wabunge wa upinzani kuhujumiwa bungeni. Hapa kinachotakiwa ni busara na si siasa za mitandao ya kulindana. Nadhani hata ndani ya CCM Magufuli alisifika kutokuwa na mitandao. Sasa iweje sasa aanzishe mitandao hata kama ni ya wastaafu? Kama watanzania wanataka wahusika washitakiwe yeye ni nani au anataka kuifanya Tanzania mali yake binafsi? Rais awasikilize wananchi wanataka nini na si yeye anataka nini vinginevyo akiri kuwa yuko madarakani kuwatumia na si kuwatumikia wananchi. Nadhani Magufuli alichaguliwa na kuapa kuilinda na kuitekeleza katiba ya nchi bila upendeleo, huba wala chuki. Yuko ikulu kuwalinda watanzania na si watawala wa zamani wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, ubabaishaji, kuisababaishaji na kuiingiza nchi kwenye umaskini bila sababu. Nadhani Magufuli anajua tuhuma zinazowakabili wahusika. Wapo wanaotuhumiwa kwa kashfa kama vile k uuza mbuga ya wanayama ya Loliondo, EPA, NBC, Kiwira na uwekezaji wa kijambazi wakati wakati wengine wakikabiliwa na wizi wa EPA, Escrow, UDA, utoroshaji wanyama hai, ujangili, uzembe, uzururaji, matumizi mabaya ya fedha za umma na mengine mengi. Siku zote Magufuli amesikika akisema anakerwa na uovu. Je hayo yaliyoorodheshwa hapo si uovu au anachagua nani awe muovu na nani asiwe?
Ifahamike kuwa Tanzania ni ya watanzania wote na si watawala wao wawe waliopo au waliopita.
Kazi ya Magufuli ni kuhakikisha usalama wa kila mtanzania na si marais wastaafu vinginevyo tubadili katiba inayotamka kuwa Tanzania ni mali ya wananchi na si watawala.
Wapo wanaoona kama maneno yake ni tofauti na kauli zake za kuleta Tanzania mpya isiyo na ufisadi wakati anakumbatia ufisadi wa wakubwa akiwapatiliza wadogo.    
Tumalizie kwa kumkubushia kauli yake aliyotoa hivi karibuni akihutubia kwenye kufungua mradi wa mawasiliano wa polisi kwenye viwanja vya Biafra aliposema, “Watanzania wamechoka na fedha zao kuliwa na watu wachache… wakale mali za bibi zao kule.” Kwa waliomsikiliza vizuri, walishangaa mantiki ya kauli yake. Hivi hawa wachache anaoongelea Magufuli ni wapi wakati anaowakingia kifua ni wachache pia; au ni kwa vile walikuwa na madaraka? Je kunani kwenye ndoa hii baina ya rais na marais wastaafu? Inatoa picha gani kwa viongozi wajao?
Chanzo: Mseto wiki hii.

No comments: