Tuesday, 19 July 2016

Kijiwe chastukia uraia pacha wa Kanji

Image result for photos of narendra modi and magufuli
            Baada ya rais Joni Kanywaji Makufuli kufichua siri kuwa Bongo ina wapiga kura wa India, kijiwe kimembana Kanji aeleze kama naye yumo na yuko wapi kati ya Bongo na India.
Mheshimiwa Bwege ndiye anaanzisha mada. Baada ya kumuamkua Kanji na kumpa ofa ya kahawa anasema, “Kanji dugu yangu, iko sikia kuwa veve iko piga kura ya kula kule Indiani. Je hii iko kweli au ongo na veve iko sema nini dugu yangu?”
Msomi Mkatatamaa anadakia, “Hata mimi hili la mkuu kutoboa ukweli huu–ambao hata hivyo, si mpya–lilinistua na kunishangaza; hasa kugundua alivyoridhika nalo badala ya kutamka wazi kuwa ni kinyume cha sheria. Nadhani mkuu anapaswa kuambiwa kuwa anachofanya si kusifia ujinga na ubaguzi kama huu bali kupambana nao kwa vile nalo ni jipu tena la muda mrefu. Inakuwaje waswahili wazuiwe uraia wa nchi mbili nyinyi akina Kanji mruhusiwe? Hivi Mkuu hajui kuwa hiki ndicho chanzo cha kutorosha njuluku na mali za kaya? Nadhani Kanji anaweza kutupa jibu sahihi wakati tukingoja la mkuu mwenyewe.”
Kanji anajitetea, “Veve onea mimi bure dugu yangu. Veve wahi ona gabacholi nakuja kunywa gahawa hapa na veve? Mimi haiko gabacholi; iko hindi sikini nishi na Swahili sikini. Ile gabacholi tajir nabagua hata mimi hata kama haibagui kama nafanya veve Swahili. Kwanini veve lau hindi. Kwani hindi diyo naunda serikalini yenu?”
Mgosi Machungi anakamua mic, “Hata sisi imetishangaza kusikia kuwa kumbe kuna Wadanganyika wanaopiga kua huko ugabachoini. Sijui kwanini wanatinyima sisi hii haki na kuwapa wageni wasio na uchungu na kaya yetu? Hapa azima mkuu atieeze hadi ti-understand na ku-compuihend.” Anamegeukia Kanji na kusema, “Hata veve Kanji iko gabachoi. Huoni unavyosema seikai yenu na siyo seikai yetu? Hii maana yake ni kwamba veve haiko raia ya kaya hii. Hii nayo baguzi kuba ndugu yangu Kanji.”
Mipawa anampoka Mgosi mic, “Mwenzenu sikushangaa; hasa nikizingatia namna jamaa hawa ambavyo wamekuwa wakishirikiana na mafisadi wazawa kusikinisha kaya. Mara hii mmesahau namna majambazi kama Chavda, Saileth Vithlani na magacholi wengine walivyoibia kaya wakaishia kuondoka kayani kwenda kutanua ulaya?”
Kabla ya kuendelea, Mchunguliaji anamchomekea Mipawa na kusema, “Mbona Chavda alisharudi na anapiga mbonji mitaa ya Upanga au hujui. Hii Bongolalaland aka Danganyika bana. Waliwadanganya kuwa Chavda alikimbia kaya wakati yuko Upanga akihomola na kula kuku kama hana akili nzuri. Jiulize, yale mashamba ya mkonge waliyosema alitumia kuibia mbona hayajawahi twaliwa kama kweli aliondoka kayani?”
Mipawa anaendelea, “Hilo nililisikia na lisirikali halikuwa tayari kukanusha au kutoa maelezo. Hata hivyo, silaumu; kwani, wakati wa utawala wa Njaa Kaya, nani angepoteza muda kutoa maelezo? Nadhani lao moja na wao ni dugu moja kwenye kuibia kaya shamba la bibi au siyo?”
Leo ni kuchomekeana mtindo mmoja mmoja. Mpemba anakwanyua mic, “Yakhe hata mie sikushangaa. Nyie mwaongelea akina Chavda, Kagoda na wale wenginewe wa zamani. Mbona yupo huyu Kamran Ahmed aliyetoroshwa wanyama hai zaidi ya mia jana tu naye alitolewa rumande na kupewa pasipoti na pipa akaondoka zake na kaya ikaishia kula hasara? Hawa ndiyo magabacholi alioonya marehemu Chris Mtikisa. Na sasa ameondolewa, sijui nani atawatia kashkash wabaguzi hawa wa kunuka?”
Mijjinga naye anaamua kukamua mic, “Mkuu hakukosea. Huenda ulimi uliteleza au alitaka kuanzisha mjadala kama huu ili asionekane kalianzisha yeye.  Mimi sikushangaa hili la uraia wa kaya nyingi. Nadhani mnapaswa kuelewa kuwa kaya hii ina sheria moja inayotumika tofauti kwa kuangalia rangi na ukwasi wa mhusika. Ukiwa kigogo kama Jimmy Rugemalayer, Singasinga, Andi Chenga au Ni Zero Kadamage unaengwa wakati wezi wa kuku wakisulubiwa kwa uvivu wao wa kufikiri wakaiba kuku badala ya maburungutu.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Usemayo kaka Mijjinga ni kweli tupu. Huoni wanavyofaidi nyumba za Msajili wa Majumba wakiitana kila uchao wakati waswahili wakiendelea kunyanyaswa kwenye mbavu za mbwa za kupanga au kuangamia mabondeni wakati nyumba zinazoitwa zao zikikaliwa na wapiga kura wa India? Nani anashupalia hili jambo ambalo ni ubaguzi wa wazi?”
Kapende anakula mic, “Nadhani tunapaswa kupigania uhuru upya ili tujenge kaya isiyo ya kibaguzi na kigabacholi.sijui kama waswahili wangekuwa ndiyo wanaishi ugabacholini kama wangepewa upendeleo kama huu. Kama kaya, tunapaswa kuwatoza kodi kubwa–kwa vile ni matajiri–ili kuweza kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya walalahoi wetu walionyonywa tangu ukoloni hadi sasa. Hapa hakuna cha nini wala nini bali kutendeana haki na kuuangalia ukweli kama ulivyo hata kama ukweli wenyewe ni mchungu. Mnasemaje wazee?”
Kijiwe kikiwa kinango si akapita manzi wa kigabacholi! Wacha Mbwamwitu ajisemee, “Kusingekuwa na ubaguzi huu wa ki-caste, huenda huyu manzi angekuwa bi mkubwa wangu.”
Kanji anajibu, “Dini yetu haikoruhusu Swahili oa hindi.”
Wanakijiwa tunageuka na kuangaliana kugundua kuwa jasiri haachi asili. Kwa pamoja, tulipanga kwenda kukuu kuamuru lisirikali lianze kushughulikia ubaguzi huu wa kizamani na kijima.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: