The Chant of Savant

Saturday 1 January 2011

Katiba mpya Kikwete kasoma alama za nyakati





The New Constitution is about you and me. It is not about president and bigwigs.It is about my kids their kids, you all and myself. For, in a common person you can see president but you can nary see a common person in president. President starts as a common person but the common person does not end as president.


Mwaka mpya umeingia. Tuliojaliwa kuuona tunamshukuru Mungu tena na tena. Muhimu ni hotuba ya rais Jakaya Kikwete,pamoja na mapungufu yake mengi tu hasa uongo, ndoto na chuku, ambaye baada ya kimya kirefu, angalau ameonyesha utashi na mwelekeo kwa kuridhia kuandikwa katiba mpya.

Kwangu hili ni jambo muhimu sana. Kwani kwenye malengo yangu makuu ya mwaka huu mojawapo ilikuwa ni kuendelea kupigania kupatikana kwa katiba mpya kwa nguvu na akili zangu zote.

Kutokana na tamko hili, katiba mpya kwa Tanzania siyo suala la mjadala tena. Je Kikwete aaminiwe kirahisi hivi hivi au tuwe makini na ahadi hii isije kututokea puani tukapote mwana na maji ya moto?

Kinachopaswa kuanza kujadiliwa ni mchakato wa kuipata. Hapa lazima tuwe makini. Tusibebwe na furaha za kuahidiwa katiba mpya bali ithibati ya utekelezaji wa ahadi hii muhimu.

Tufanye hivyo kutokana na uzoefu kuwa rais wetu amekuwa bingwa wa kutoa ahadi na bingwa wa kutozitekeleza. Hivyo basi, tushikilie msimamo kuhakikisha katiba mpya inaandikwa. Na si kuandikwa tu bali itokane nasi kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.

Tusikubali ama rais na watu wake au chama chake waiteke na kutuandikia katiba mpya isiyo mpya bali mkenge mwingine mpya.

Wadau wote lazima tuhakikishe tunakuwa sehemu ya mchakato huu ili kupata katiba itokanayo nasi kwa ajili yetu.

Kuridhia kwa Kikwete kuandikwa katiba mpya ni suto kwa wote wenye mawazo mgando waliojaribu kupinga. Hapa lazima watu kama Yusuf Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na mwanasheria mkuu wa serikali (AG) Fredrick Werema waone aibu na kutambua kuwa katiba ni haki na stahiki ya watanzania.

Kinachoanza kuleta utata ni ile hali ya AG yule yule aliyepinga wazi wazi kuwa mojawapo ya watakaosimamia mchakato huu. Kama itakuwa hivyo, kuna haja ya kumwekea masharti na si kumruhusu aandike katiba inayokidhi matakwa ya watu wachache anaoonyesha wazi kuwatetea hasa mafisadi kama alivyojionyesha kwenye masuala ya katiba mpya na wizi wa Dowans. Tusiruhusu AG afanye kama alivyofanya kwenye mkataba wa Dowans na mikataba mingine ya kijambazi.

Kuahidi katiba mpya ni jambo moja na kuiandika inavyopaswa ni jambo jingine. Hivyo, tusibweteke na ahadi bali tuwe makini na mchakato mzima kwa kuumilki vilivyo.

Je tunahitaji tume ya katiba (Constitution Commission) au kusanyiko la katiba (Constitution Assembly)?

Haya ni baadhi ya maswali muhimu tunayopaswa kuyapatia majibu kabla ya kuuingia mkenge kutokana na furaha ya kuahidiwa tunachokitaka.

Tungemshauri Kikwete na watu wake wafuate njia aliyofuata rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye alichafuka kila sehemu lakini akaokolewa na kuridhia kuandikwa katiba mpya.

Hata Kikwete hajachelewa. Atupe katiba mpya safi na madhambi yake yatabakia historia huku akijijengea legacy inayomeremereta.

Dokezo

Lazima katiba mpya tarajiwa iweke misingi ya taifa jipya kwa kuweka wazi vifungu vya uwajibikaji, kupambana na ufisadi, matumizi mazuri ya fedha na raslimali za umma kwa manufaa ya watanzania na si wawekezaji na wakimbizi wa kiuchumi kama ilivyo sasa, itamke ulazima na uwepo wa serikali ndogo inayofanana na uchumi wetu na kulinda haki za watanzania wote kwa vitendo, haki na usawa.

Pia katiba mpya lazima iwe na mawazo na misingi mipya ya kulikomboa taifa hasa toka kwenye makucha ya mafisadi wachache wanaoifuja nchi.

Tunampongeza Kikwete kwa kusoma alama za nyakati. Tunamshauri asiyumbishwe. Maana nchi ni zaidi ya yeye na kundi lake na chama chake.

Haya shime tuanze mchakato wa kuunda mawazo yatakayokuwamo kwenye katiba yetu ambayo inapaswa kuwa endelevu na ya kistaarabu yenye kuleta maendeleo na haki kwa watu wetu.

Wenye hofu na katiba mpya tuwatoe hofu kuwa hatutaandika katiba yenye kulipiza kisasi au kuwalinda wachache na kuwaumiza wengi. Wasihofu. Kwani katiba yetu itaandikwa na watu wote na si kikundi cha watu wenye maslahi fichi. Hivyo tusisitize kuwa tusiruhusu makundi yenye maslahi uchwara kuiteka katiba yetu mpya.

Ningependa, baada ya kumaliza kazi ya kuandika, kupitisha na kuifanya katiba mpya kuwa sheria, kama mwananchi niseme au tuseme kila mmoja wetu:"Exegi monumentum aere perennius."
"I created a monument that will last longer than if it were of bronze." Bila kuwa na jeuri na fursa ya kujitapa hivi, yote yatakuwa usanii usanii mtupu. Hata hivyo, ningeshauri sana wahusika wabadilike nasi tusonge mbele.


Msisitizo ni kwamba ahadi ni kitu kimoja. Kutekeleza ni kitu kingine. Nisingetaka tuishie kuwa ama na KATIBA YA NDOTONI kama Kanani au Katiba mpya ya wale wale wala nchi na si wananchi. Tunapaswa kumchunga mtu wetu kwa kuangalia historia ya matendo, maneno, ahadi zake na waliomzunguka wakimwendesha watakavyo hasa mafisadi.


Tunawatakia mwaka mpya wenye kila neema mojawapo ikiwa ni katiba mpya.

3 comments:

Anonymous said...

ccm wameshapoteze mvuto, sidhani kama katiba mpya wanaitaka kweli lazima kuna maslahi wanataka wayachomeke, simwamini kikwete na ccm kwa ujumla, wanajua mabadiliko ya katiba itakula kwao,tusubiri tuone, waibe kura waingie madarakani, waibe kodi za wananchi ili waingie madarakani, waibe kura za udiwani waingie madarakani, wasign mikataba ya utapeli, pesa zirudi kwa wafadhili wa chama, hapana na wasiwasi sana, ni agenda tuu ta kuvutia upepo kwao, mtu mwenye tamaa ya madaraka kama kikwete na wana ccm wenzake wasiotaka mabadiliko hawajawahi kuwa na mapenzi mema kwa nchi hii na siwaamini ngo

Anonymous said...

ni unafiki tuu, hotuba ya jana nilisikiliza nikashikwa na hasira nikazima redio, badala ya kuongea pointi anaongea majungu, just imagine anasema wanafunzi wavyuo vikuu waligoma kwa kusaidiwa na vyama vya upinzania anataka kumdanganya nani kuwa wanafunzi wanasoma katika mazingia mazuri, nenda udoma uone sewageinavyoleak ovyo, maji hakuna, miaka 3 sasa, hakuna PT, vyuo vingine wanafunzi hawana makazi, wengi hawajapata mikopo, leo anadanganya kuwa walishawishiwa ili wadai haki yao, real kikwete mimi ni mwanafunzi na sikulisikia hilo ila nasoma katika mazingira magumu, i hate you, kwa tumia akili unapopambanua mambo, unataka kuvutia vijana ccm, hatutaipenda ccm kamwe labda vijijini

Anonymous said...

Umesema kweli mwandishi. Tusibweteke kwa vile CCM ni mafisadi. Kikwete hana nia safi na katiba. Tuwa makini na macho hii ni CCM.
Amfukuze Werema kwanza ndipo tumuamini. Pia atuachie wananchi tuunde katiba yetu.