The Chant of Savant

Thursday 3 February 2011

Amani na utulivu ilivyotudumaza Bongo

NAJUA wasomaji wengi watashangaa hata kuchukia watakaposoma hii. Ima watadhani nimelishwa limbwata (mabaki ya ufisadi) kama wale fisi watu akina Tambo Hizo, au waandishi uchwara kama wale wa Rostitamu wa Kagodoga bin Dowans.

Hapana sijalishwa kitu bali ni mambo ya maisha. Hii maana yake ni kwamba msishangae hapo baadaye tukageukana. Wale waliokuwa wakikamia damu ya mafisadi wa Dowanis na Lisirikali mtawakuta wakiitetea kama dini yao!

Matumbo haya! Ukiyaendekeza unaweza kuvua hata nguo ukatembea uchi usijue!

Nimepata tetesi kuwa Mkuu wa Kaya anaweza kuniteua kuwa mkubwa wa ofisi yake ya propaganda na habari. Hivyo, naanza kujipendekeza ili anipe. Ila naonya. Kama hatanipa, nitarejea viwanjani.

Ngoja nianze kupalilia kibarua changu kipya cha aibu hata kama kinaweza kujaza hili tumbo langu lisilo na shukrani kama shimo.

Bongolalaland ni nchi pekee duniani yenye mshikamano na amani vya aina yake. Hali hii imefanya maadui wengi wa taifa kuionea wivu kiasi cha kutaka kuivuruga. Watu hawa wasiojua siri ya vitu hivi wanatuonea wivu na kutaka tuanze hata kugeukana na kufungana jambo ambalo si la kistaarabu hata kidogo.

Chukulia mfano matukio madogo kama ya AR au uchakachuaji ambapo baadhi ya vyama vinadai kura zake kuchakachuliwa. Hatuwezi kuviruhusu kuja na madai kama haya yanayotaka kuvuruga ulaji na mshikamano wetu.

Najua hili litawaudhi viherehere walioshupalia mauaji ya AR. Kuna kosa gani kwa mwenye shamba kuchukua kondoo wawili, watatu akafanya matambiko yake ili mambo yake yaende sawa? Anayebishia hili ajiulize. Kama kuna wabongo walidedishwa huko Arusha then what next? Si mmeishawasahau na kuendelea kuponda raha na shida zenu kutegemea uko kundi gani kati ya wadanganyika na mafisiahadi?

Chini ya amani ya pekee na mshikamano wa kupigiwa mfano, Bongolalaland inashika rekodi za juu kwa mambo mengi hasa yenye kuhusu amani na mshikamano.

Kwa mfano ndata akimchapa mtu shaba hakuna haja ya kuandamana hadi kupinduana bali kumtwisha mzigo ndata hata kama katumwa na topu wake kama ilivyokuwa AR. Kwa amani yetu ndata hafungwi bali kuwavunga walevi na mambo yanaishia hapa.

Kitu kingine kilichowezesha “amani na mshikamano” kuwepo ni kale ka ungonjwa ka kusahau ka wabongolalalanders. Nani anakumbuka Oko? Tumia Oko hadi mzee ruksa akaitwa kuzindua huu utapeli. Baada ya muda hapakuwa na cha Oko wala Koho bali wajanja kumwingiza mkenge rais na kuondoka na njuluku kama Richmond na sasa Dowans.

Haya mambo hayakuanza jana sema ni ile hali ya walevi kusahau kirahisi. Tuyaache watu wahomole. Maana imeandikwa walevi ndiyo waliowao.

Tusonge mbele. Chini ya dhana hii unaweza kughushi vyeti vya taaluma na kuitwa daktari wakati ni kilaza na tapeli wa kawaida. Kwa vyeti hivi vya kughushi unaweza kupewa hata uwaziri na hakuna anayekugusa kwa kuogopa kuvuruga mshikamano na amani.

Wabongolalalanders ni watu wakarimu wasiopenda kuitana majina mabaya kama vile jizi, tapeli, msanii, mbabaishaji na fisadi. Wabongolalalanders hupenda kuitana waheshimiwa hata ndugu wakati mwingine hata kama hawana heshima. Wana mshikamano wa kweli ambao umewezesha nchi kuwa ya amani. Unaweza kuliibia taifa tena mabilioni na kuendelea kuwa panga lenye makali japo la zamani na majina mengine kama hakuna mchapakazi kama wewe.

Ni Bongolalaland tu ambapo tapeli yeyote anaweza kujiita daktari wakati ukweli ni mganga wa kienyeji tena tapeli wa kutupwa.

Ni Bongolalaland pekee ambapo kwa mfano, kugombea ubunge hakuhitaji uadilifu wala rekodi nzuri. Kuwakilisha wananchi ni kuwakilisha wananchi na si kupimana uadilifu.

Ni Bongolalaland pekee ambapo unaweza kuwahimiza watu wawe waaminifu lakini wewe usiwe na wasikusumbue kutokana na kuogopa kuvuruga mshikamano na amani.

Ni Bongolalaland pekee ambapo mwizi wa kodi za wanuka shida anaweza kuwahimiza walipe kodi kwa sana ili atanue na kuchezea kama kuwalipa majambazi wa Dowanis na hakuna anayekuja juu wala kuingia mitaani kama kule Tunisia, Misri na Yemen.

Unaweza kununua dege na rada bomu na kuficha pesa nje na bado ukaendelea kupeta.

Hivi ni baadhi ya vitu vinavyofanya nchi nyingi duniani zituonee wivu. Nchini Japan ukifanya vitu kama hivyo, kutokana na roho mbaya yao, utaishia kujinyonga kutokana na aibu. Kule China ukifanya hata nusu ya hayo utaishia kutundikwa risasi kutokana na Wachina kutokuwa na mshikamano na amani kama vyetu.

Bongolalaland ni nchi pekee ambapo, kwa mfano tume ya uchaguzi inaweza kuchakachua kura na matokeo na wahusika wakaendelea kuheshimika na kulipwa tofauti na nchi za wenzetu ambao hawana mshikamano na amani kama vyetu.

Tuliona wenzetu na jirani zetu wa Nyayoland walivyovuruga mshikamano na amani zao kwa madai ya uchakachuaji ambapo kwetu tumeamua yaishe kinamna ili tusivuruge amani ya nchi na mshikamano wake.

Ni Bongolalaland tu ambapo mgeni anakuja maskini na kuondoka akiwa tajiri wa kutupwa hata kwa kuchota toka benki za umma au kutorosha fedha za kigeni na asiguswe kwa kuogopa kuleta jina baya na kuvuruga amani na mshikamano.

Katika Bongolalaland, kila kitu kinawezekana. Unaweza kufanya biashara bila leseni, kutolipa kodi hata kuuza bidhaa za viwango vya chini na usisumbuliwe kwa kuogopa kuvuruga amani na mshikamano. Ni kwa Bongolalaland tu mtu anaweza kuuibia umma halafu akauhonga pesa hiyo hiyo kwa njia za misaada.

Ni nchini Bongolalaland tu ambapo wanasiasa wanaweza kuunda vyama na kupingana kwa miongo halafu ghafla wanapatana na kupeana ulaji wakiwaacha wanachama waliopigwa na butwaa wasifanye lolote kwa kuogopa kuvuruga amani na mshikamano huu wa ulaji.

Ni Bongolalaland pekee, kama nilivyosema awali, ndata wanaweza kuua waandamanaji na bado wakasema waleta na kulinda amani kama ilvyotokea visiwani. Ni sehemu pekee ambapo amani hulindwa kwa vitisho, vurugu hata uongo.

Rejea jinsi Jeshi la Polisi lilivyotembeza vipigo na mabomu ya machozi wakati wa uchakachuaji na utangazaji wa matokeo yake na amani inaendelea kiasi cha watawala kuwahimiza watu wasiruhusu madai ya uchakachuaji yaivunje.

Tuonane wiki ijayo kwa sasa nawahi Mahakama Kuu kuweka pingamizi Dowans wasilipwe, ingawa kuna watu wamenitonya kuwa njuluku zimeishaanza kulipwa kama wiki tatu zilizopita.

Ngoja nisokote bange langu linibangue nikamsake Rostitamu na vibaka wenzake niwatie nari.

Chanzo: Tanzania Daima Februari 2, 2011.

4 comments:

Jaribu said...

Unasema kweli, Mhango. Tumedumazwa na propaganda za kijamaa za CCM na dini. Tunasubiria mafisadi waje kuhukumiwa siku ya kiyama. How about holding these scoundrels accountable now, instead of waiting for afterlife?

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu,
What a smart idea. In fact, if anything, that is what I have always advocated and agitated for. Tufikie mahali tuache kujidanganya. Mafisadi wanajua upuuzi huu wa kujidanganya wakati tunazidi kuteketea. Thanks for visiting me.

Jaribu said...

You are welcome. Nilifikiria ni mimi peke yangu niliyochoshwa na status quo, kwa hiyo nilifurahi kugundua web site yako. Keep up the good work by spreading the word.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Thanks, Indeed I will. Tunapaswa kuwaamsha watu wetu wajue fika kuwa ukombozi wao uko mikononi mwao.Wajue kuwa hakuna kikwazo kingine kwa maendeleo na mstakabali wao bali wao wenyewe. Kwanini wengine tena wenye population ndogo waweze sisi tusiweze? Changamoto na suto kwetu.