Ile safu ya Jicho la Kijiwe imehamia rasmi Nipashe kutokana na sababu ambazo si vizuri kuzieleza. Safu hii ilisifika sana kwenye gazeti la Tanzania Daima. Ilikuwa safu ndefu karibia kuliko zote kwenye gazeti hilo. Safu hii chini ya kichwa cha Hekima na hekaya za Mlevi itakuwa ikitoka kwenye gazeti la Nipashe la Jumamosi. Tunawashukuru wasomaj wetu wa safu hii wa zaidi ya miaka mitano.
Tukutane huko
Wapendwa wasomaji wa mipasho na umbea, habari za zali,
Ninayo furaha kuwaleteeni habari njema ya ukombozi itakayo wajaza
furaha na wengine majonzi. Tusameheane. Kama mjuavyo, kwa vile hii ni ngoma mpya
kwenye uwanja huu ingawa mtambo si mpya, kama ada, lazima nifanye kitu wazungu
huita intro.
Kwa
ufupi naitwa Dk, Profesa, Al Haj, Mwalimu, Field mashall, shehe,
ulamaa,maulana, Man and a half, askofu Nkwazi Mhango
aka Mpayukaji Msemahovyo bin Wapashe bin Waelewe bin Mtoboasiri aka Kiwanda cha
Maneno aka Ngoma Kubwa. CV au Resume yangu ni ndefu kiasi kwamba
nikiandika sifa zangu zote naweza kujaza barabara. Nitawapa kiduchu tu. Nina
PhD
(Commonwealth Nonexistent University), PhD (Havazard),
PhD (Edenbug), PhD (Quacks’
Open University of the World (QOUW), New York na PhD (Make-believe
University), Bangalore, India. Pia nina Masters nyingi toka vyuo kama Msoto
University, Uswekeni, Uswazi na Kijiweni universities.
Kitaalamu naitwa Seer, nobleman, PhD Phil, MA (Abracadabra and
Hypothetical Thinking), BSc (Lies and truth), Dip (Corruption and Mafia
Management (CCM), Masters (Public funds Terrorizing), MBA, Masters (Money-making
and Forgeries), etc.
Najua wengi wananifahamu kutokana na kuchezea timu ile
ambayo nimeitema kutokana na sababu ambazo ni Top secret kwa ajili ya
usalama wa walevi na wavuta bangi wenzangu.Kama akina Messi wanahama timu
kwanini nami nisifanye hivyo? Nauza ujuzi wangu bwana hata kama ni wa kilevi.
Mie nilizaliwa nikiwa nimelewa kiasi cha kuitwa Mlevi. Nilianza kuongea nikiwa
na miezi miwili ndio maana niliitwa Mpuyukaji. Haya si makosa
yangu bali bi mkubwa aliyekuwa akipiga ulabu wakati wa ujawepesi wangu.
Ninayoandika siku zote huwa ni mawazo ya kilevilevi. Kama nikikushika pabaya
huna haja ya kwenda kwa pilato. Maana ukinishitaki na akiniona mahakamani,
atanitoa mkuku right away. Nilishashitakiwa sana kwa ulevi. Ndata
walishaninyaka sana hata kunibambikizia kesi. Kila wakifanya hivyo pilato
hunitema kwa vile ana ushahidi tena toka kwa daktari wa akili kuwa mambo
upstairs kwangu si normal. Hivyo, kama ukiona nimekugusa pabaya
umezee na kunisamehe huku ukijirekebisha.
Pia
huwa ninao wenzangu tunaokunywa na kuvuta pamoja. Sisi hujichukulia ni kama
bunge la kutetea walevi na wale wote wanaotendewa kilevi na walevi wakubwa wenye
maulaji ya mamlaka.
Nilipata bahati ya kusoma hadi ng’ambo japo haikuzuia kuendelea kuwa
mlevi. Wahenga walisema: Elimu ya mtu haiondoi ujuha wake. Tusingekuwa na watu
wenye madigrii gunia wakifanya ufisadi kiasi cha kuwaacha watu hoi? Hivyo,
msinishangae bali msome niandikayo ili yawe darasa msiwe kama mimi. Kitu cha
kujivunia ni kwamba ulevi wangu unalipa. Kwani kuna kipindi wazito huniita lau
wanikatie mshiko nisiwaumbue au niwape ushauri. Wanajua nimebukua kama sina
akili nzuri. Bahati nzuri, pamoja na ulevi wangu, sikughushi wala kufeli. Wakati
nikiwa chuoni kule Uskochi alikosoma Mwalimu Mchonga niliondoka na GPA ya 4.00
kiasi cha kuombwa nisirejee nchini badala yake nifundishe chuoni pale. Jina la
chuo usiniulize ila siyo Edinburg.
Katika shahada yangu ya kwanza nilisomea Upayukaji yaani
Rhetorics. Shahada ya pili nilisomea uhalisia yaani
Realism.
PhD nilisomea Uchakachuaji na Usemahovyo. Nina masters
na PhD kadhaa.Nasisitiza. Sikuzipata online wala kughushi
wala kupewa za heshima. I toiled for my degrees. Hivyo, nimebukua
kama sina akili nzuri. Najua wengi wakibahatika kuonana name hawataamini
kutokana na pombe, bangi na bwimbwi vilivyonibangua na kuninyuka. Ila aminini
nimesoma sana. Ndiyo maana nilikataa hata kuajiriwa kwenye ofisi za umma ili
nisipate vishawishi na kuuma umma kama wenzangu wenye shahada za kweli na za
kughushi wanavyouuma umma. Mie nauma mma.
Kwa
vile waswahili wengi huamini kuwa kusoma ni kumwaga umombo, huwa siachwi nyuma.
Nachonga umombo hadi ufransii. You know what? I speak English like the
Queen. So too I speak French like Napoleon Bonapatre. C’est tres vrai. Je
parle Francais comment Parisiennes ou quelque un qui habit au France.
Loo!
Nshahararibu! Kwa vile leo nakuja na inshu ya introduction, acha nitambae
na misifa yangu.
Nimeishawaeleza kisomo changu. Ngoja niwape kidogo juu ya maisha
yangu hapa Bongo. Ninaishi Uswazi na mtaa na nyumba navyo ni top secret.
Kwa ninavyowananga mafisadi na wengine wanaofanya mambo ambayo siyo, siwezi
kutoa anwani yangu. Niaminini. Hata mhariri hajui mitaa yangu. Maana
ninavyochukiwa na jamaa zangu hasa ndata wanaoniwinda ili wanitie nguvuni kwa
kunywa gongo, nikitaja nitakuwa nimejihukumu kifo.
Mie
ni mpenzi wa gongo, kahawa na bwimbwi. Kwa vile bwimbwi na gongo ni chanzo
kizuri cha mapato kwa ndata wanapokubamba, huwa sitaji mitaa ninayoishi wala
kunywa.
Huyo
ni mimi. Kuna wazee wenzangu tunaoshirikiana kuendesha bunge la walevi. Hawa leo
siwatambulishi ili wasiharibu intro yangu. Loo! Nilitaka kusahau mtu
muhimu kwangu! Huyu si mwingine bali bi mkubwa mama Kidume Nesaa Mpayukaji
Msemahovyo almaarufu Mother Lioness. Huyu si mlevi wa gongo kama mimi;
ni mlevi wa migold na mapambo. Ukimuona huwezi kuamini kuwa
anashare bedroom na mlevi kama mimi. By the way, yeye akiulizwa
alinipendea nini husema siri ya mtungi aijuaye kata. Je lipi bora kati ya mlevi
kama mimi na mafisi na mafisadi mnaowaita waheshimiwa?
Kwa
wasiojua ukweli ni kwamba hata wale wanafalsafa maarufu mnaopenda kuwanukuu
akina Socrates, Sophocles, Heraclitus na wengine wengi walikuwa walevi wa ukweli
kama mimi. Hii ndiyo sababu ya kupenda ulevi kuliko ushufaa na uheshimiwa wa
shilingi mbili utokanao na hongo, uchakachuaji na ufisadi.
Leo
sitasema mengi. Mengi mtayaona kwenye nondo zangu zitakazofuata. Onyo: mafisi,
mafisadi, warongo, wezi, wauza unga, wala rushwa, wasanii, wababaishaji,
matapeli, wanaoghushi na wengine hawa ndiyo target yangu.
Au
revoir and Sii yu!
Chanzo: Nipashe Februari 2, 2013
1 comment:
Ahsante kwa taarifa!!
Post a Comment