The Chant of Savant

Saturday 1 June 2013

Gesi Mtwara, nilisema mtumie 'GESHI' si jeshi


Juzi niliposikia kuwa wananchi wasio na hatia kule Ntwara `walibondwa’ na hata wengine kunyotolewa roho, niliumia sana. Hadi ninapoandika pombe na bangi vimenitoka kiasi cha kuwa normal na kuandika kitu serious seriously.
Usishangae kuona naandika kwa kuchanganya lugha. Ni sababu ya huzuni na usongo. Kama wao wanachanganya mambo, kwanini mlevi nisichanganye japo sijachanganyikiwa na kuishiwa kama wao. Sijui haya matumizi mabaya ya jeshi yanalifundisha nini?
Katika nasaha zangu kwa watawala wetu wanaoanza kuonekana vichwa ngumu, nilishauri mgogoro wa gesiasili watumie nguvu ya ‘GESHI’ yaani Gawaneni, Elimishaneni, Shirikianeni, Heshimianeni na Ishini (kwa haki na amani).
Pia nikaasa kuhusu ‘POLISH’ yaani Pataneni, Ongeeni, Laumianeni Ila Siyo Hujuma. Mie wala sikumaanisha mtumie jeshi na polisi. Kwani kazi ya polisi ni kulinda usalama au kuuvuruga kama ilivyotokea Ntwara?
 Mbona kazi ya jeshi ni kulinda mipaka yetu na si kupiga watu.  Kumbe jamaa hawakunielewa! Laiti wangenielewa wasingeaibika na kuhatarisha mstakabali wa kaya bila sababu yoyote ya maana, zaidi ya roho mbaya na uroho.
Au hawakunisoma. Je, walinisoma wakanielewa ila wakaamua kujifanya hamnazo na kufanya vitu vya ajabu ambavyo mwisho wake, unaweza kujikuta  wana poop kwenye debe kule The Hague kama akina Chaz Taylor na Laurent Badboy na nkewe?
Chonde chonde ndugu zanguni. Hii kaya ni yetu sote kwa pamoja na kwa usawa, japo kuna wanaoiibia huku wengine wakifa makapuku.  Japo kuna ngurumbili wanajiona wao ni wenye na wala kaya na wanakaya ni mabwege, kuna siku kibao kitawageukia wajute kuzaliwa.
Siamini kama tuna haja ya kufika huko mapema hivi. Je, haya ndiyo maisha bora mliyotuahidi ambapo mnatupa maisha balaa ya vipigo na udhalilishaji? Sioni sababu ya kugombea neema ya gesiasili kiasi cha kuigeuza kuwa laanaasilia.
Sioni mantiki ya jeshi linaloitwa la walevi kuwatwanga hata ‘kuwadedisha’ na kuwapora walevi ambao kimsingi ndiyo wanaotoa uchache wa kulisha na kuliendesha.
Jamani, tusikubali aibu na jinai hii. Naaamini mheshimiwa Mkubwa ananisikia. Kama hanisikii watu wake wananisikia na kunielewa. Siku hizi Jeshi la Walevi wa Tanzia, usichanganye na lile la Wananchi, please. Sitaki kichapo japo kwa making- fu yangu hakuna wa kuniweza.
Jeshi la walevi imegeuka Jeuri ya Walaji Teketeza Walevi. Sisi walevi huwa tunalipa jeshi ulabu na maisha bure. Linakula na kunywa bure. Je hii ndiyo shukrani au ni shukrani ya punda?
Tunafanyiwa hivyo kwa sababu ni walevi au what? Kama wana maguvu kwanini wasiende kupambana na mafisadi na majambazi yanayoibia kaya yetu na kutuacha walevi apeche alolo?
Tahadhali. Leo sijapiga ulabu wala kuvuta sigara kubwa. Nina akili timamu na uchungu ambavyo vimenisukuma kuandika waraka huu kwa watulao wetu wote, ambao walevi huwaita watawala.
Sioni mantiki ya wachukuaji waitwao wawekezaji wasiowekeza kitu zaidi ya ghilba na milungula kututesa kiasi hiki. Basi badilini jina la kaya kutoka Tanzia kwenye Tanzawekezaji au Tanzachukuaji tujue ili tusiendelee kuwaghasi bure.
Walevi, kwa mfano, wanataka wajue ni kwanini zabuni ya kujenga m-bomba wa hiyo gesi inayoaanza kutuchoma kabla ya kutumulikia, ilitangazwa lini na nani na kwa vigezo gani na vipi?
Nauliza kutaka kujua na si kuwachokonoa wakubwa wenye maulaji yao ya siri na hovyo kwenye mradi wa gesiasili.
Hao Wachina wanaojenga hilo bomba walishindana na nani kupata hiyo tenda? Je haya ndiyo mantiki ya ziara ya bwana elephant Amdaraman Kinamna kule China hapo mwezi Machi mwaka huu?
Naomba mnielimisheni hata kama elimu yenu imeishageuka mitumba ambapo watoto wanafelishwa tena baada ya kulanguliwa kununua ujinga na wakubwa, eti wanafuta matokeo utadhani wao ndiyo Baraza la Mitihani.
Si mkubali na kusema kuwa mmeshindwa tena vibaya? Kila siku `rongo rongo’ maisha bora maendeleo wakati ni urongo mtupu. Mnadhani maisha bora na maendeleo yenu yana- reflect walevi wote? Acheni uhuni jamani tukae tujenga kaya na kuishi kwa neema badala ya nakama.
Katika majibu nitakayopewa ili nielimike halafu niende kwetu Ntwara, niwaelimishe akina Njomba na Somoe sitaki kusikia upuuzi wa J4 Kawa-dog, ambaye nimeishamwamuru aachie ngazi lakini anang'ang'ania eti kwa vile anatoka sehemu moja na Njaa Kaya mkuu.
Wazungu huhoji, what do you expect when "The blind leads the blind?" yaani kipofu akiwaongoza vipofu wote wataangamia kwenye mashimo. Juzi eti yule tapeli bingwa wa kughushi aitwaye Emmy Nchimvi, alikwenda Ntwara kusuluhisha.
Asuluhishe nini wakati naye anahitaji kusuluhishwa na kusulubiwa kwa kashfa yake ya kughushi? Nilitaka kupasuka niliposikia eti na Saydu Mwemae alikuwapo.
Aende kule kusaidia nini iwapo ndata wake wanaoongoza kwa kuwanyotoa roho walevi kwa risasi zilizonunuliwa kwa njuluku zao? Wajomba zangu kule Bush-angle husema ‘Kachenjere’ wale wa kule Ithekahuno husema ‘Thie ngui iwe.’
Kwa ushenzi sitatoa tafsiri ila wenye akili wamenideku. Mnaaendekeza uroho halafu mnajifanya wazalendo wa kaya wakati ni wasaliti maafriti watupu. Shame on you once again!
Nina `mihasira’ kiasi cha kutamani niende niyanase vibao na kuyafunga pingu na kuyatupa Segerea na Ukonga kama Saddam alivyofanyiwa, kwa kutupwa kwenye gereza la Abu Ghraib alikokuwa akifungia na kunyongea walevi wa kayani mwake.
Asijue naye siku moja ataingia  na kunyongewa pale Kadhimiya ambako nilihudhuria majilini kumsanifu kama alivyokuwa akisanifu wale aliokuwa akionea na kunyonga.
Nilidhani kashfa ya uuzaji wa vipusa na mibwimbwi ingewafungua macho jamaa lakini wapi.
Hebu tujiulize swali moja dogo. Inakuwaje jeshi linalopaswa kulinda mipaka yetu inayochezewa na wageni kama ilivyoripotiwa hivi karibuni, kuwa wasomali kadhaa wanaingiza watu kayani watakavyo hailindwi.
Badala yake linatumika kubonda na kudedisha walevi wa Ntwara ambao dhambi yao ni kudai haki yao? Hili ni jeshi tena au geresha?
Tumalizie kwa kutoa ushauri mpya ingawa magamba yameishaanza usanii wa eti kutaka wakubwa wa Ntwara wafukuzwe wakati wa kufukuzwa ni mkubwa wao wote.
Don’t throw innocent officials under the bus to spere his boss who always has proved to sleep on the wheel.  Kuna kipindi inabidi watawaliwa waongoze njia watawale na watawala wafuate waone raha ya kufanya hivyo hasa pale wanapothibitisha kuwa wameshindwa kulhali.

Chanzo: Nipashe Juni 1, 2013.

3 comments:

Jaribu said...

Naona wakihitaji kuwatwanga na kuwaibia wananchi hawahitaji hongo wala usafiri, lakini ukiwaambia wachunguze uhalifu wanakuja na sababu lundo. Anayehitaji kutwangwa na kukamatwa ni mwenyewe Fisadi Mkuu, Dr Clueless.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

We Jaribu, Dr who? Is it clueless or cruelty? Gosh! Tanzania went to dogs the day this guy became presider.

Jaribu said...

You are so correct, Dr Clueless bin Cruelty.