MANENO ya ajabu yaliyotelewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda yametufanya tusononeke na kuogopa. Tunaomjua Pinda hatuamini kama siku hiyo alikuwa barabara.
Yawezekana alikuwa ameficha uhovyo huu ambao ni ushahidi kuwa sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefilisika na kuishiwa vibaya iwapo watu kama Pinda wako hivi.
Kwa nafasi yake, Pinda kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, kutoa kauli zenye kuvunja sheria na katiba na kushabikia jinai, uonevu na vurugu ni aibu na pigo kubwa kwake, serikali yake na chama chake.
Pinda alikaririwa akihimiza fujo na mashambulizi kwa raia hata wanapodai haki zao. Alikaririwa akisema bungeni; “Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”
Kumbe uongozi wa CCM umechoka wananchi na kuwaona kama wafanya fujo pale wanapodai haki zao? Je, viongozi waliochoka wanapaswa kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma?
Je, alitaka wananchi wawapende viongozi waovu na wababaishaji? Je, inapofikia baba akawaambia wanae kuwa amewachoka, kweli baba wa namna hii hajivui ubaba? Je, Pinda hakujua uzito wa nafasi yake na maneno yake? Je, Pinda alikuwa ameficha uhovyo wake kiasi cha kuonekana kuwa mmoja wa viongozi makini wachache wakati siyo?
Japo si nia yetu kumchambua Pinda badala ya hoja, inaonekana ameishiwa, tena vibaya sana. Hivi Pinda anaishi dunia gani asiyejua kuwa Watanzania wameonewa na polisi kwa kiwango cha kutisha? Je, kama wote tutakuwa na mawazo mgando na ya vurugu kama ya Pinda nchi hii itatawalika?
Je, Pinda hajui kuwa umma una nguvu kuliko hilo jeshi lake la polisi ambalo serikali yake imekuwa ikilitegemea kuendelea kuwa madarakani? Nitashangaa kama ataendelea kuwa waziri mkuu japo katika taifa letu kwa sasa lolote linawezekana.
Pinda anawakilisha mawazo ya serikali na bosi wake Rais Jakaya Kikwete aliyeendelea kutanua nchini Uingereza hata baada ya kupata taarifa za kulipuliwa bomu na kuua watu.
Kwa vile alikuwa akijua kilichotokea kama alivyokaririwa akisema, aliona mpira ni bora kuliko wafuasi wa CHADEMA ambao hata hivyo ni Watanzania sawa na yeye.
Tumeshuhudia akina Barack Obama wakiacha mambo mengi kwenda kuhami wahanga na kutoa msimamo kama viongozi waadilifu na wanaojua wanachofanya.
Mtu anafanya madudu na kupandishwa cheo kama ilivyotokea kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Kamanda huyu alipandishwa cheo pamoja na kushutumiwa kusababisha mauaji ya mwandishi Daud Mwangosi.
Ni bahati nzuri kwa watawala kuwa waandishi wa habari wa Tanzania nao wameathirika. Bila hiyo wangegomea kuandika habari za serikali ili waone kama ingefanya kazi.
Pinda licha ya kuwadharau na kuwabagua Watanzania, amehatarisha maisha yao kwa kutoa amri na shinikizo kwa jeshi linalosifika kuwatesa na kuwadhulumu kuwapiga litakavyo.
Hii maana yake ni kwamba tujiandae kushuhudia mauaji mengine kama ya Mwangosi na utekaji na utesaji waliofanyiwa Absalom Kibanda aliye Mhariri Mtendaji wa Habari Corporation (2006) na Dk. Stephen Ulimboka.
Tutarajie mashambulio mengine ya mabomu kama lile lililotokea Arusha. Je, viongozi wa namna hii ni wa kuvumiliwa au kushughulikiwa na umma? Je, ni kulewa madaraka au kuishiwa?
Wataalamu wa mawasiliano wana kitu kinaitwa ‘frontstage’ na ‘backstage’. Alichosema Pinda ni ‘backstage’ yake ambayo hakupaswa kuonyesha kwa wananchi waliomwamini na kumthamini kama kiongozi wao hata kuendesha maisha yao kwa kodi zao.
Kiongozi asiyejua la kusema mbele ya umma na nyuma ya pazia lazima ima awe ameishiwa, au amekuwa kiongozi kwa bahati mbaya tu. Je, nini kimemsibu Pinda ambaye hupenda kujiita mtoto wa mkulima wakati ni tajiri wa kutupwa anayeweza kuvaa saa ya dhahabu akidhani watu hawaoni?
Je, Pinda, tena mwanasheria, amesahau kuwa kama mauaji ya kinyama na kigaidi yanaweza kutokea chini ya amri yake anaweza kujikuta mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) huko The Hague? Nani atamwokoa Pinda kumshauri aachane na njia ya kupotoka anayochukua kwa hiari yake?
Je, Pinda anathibitisha ile dhana ya CCM kuwa chama ni zaidi ya wananchi wakati asijue kinategemea hao hao wananchi? Kwa kauli yake ya kizembe, naamini hata wanachama wa CCM wataipinga na kuanza kufikiri upya kuendelea kuwa wanachama wa chama kisicho na mwelekeo hadi kushabikia mauaji na mateso ya wananchi.
Pinda alipaswa kujitofautisha na watu kama Mwigulu Nchemba, William Lukuvi na Nape Nnauye ambao wanaweza kujisemea lolote wakati wowote bila kutathmini athari za matamko yao kutokana na uwezo wao haba na ile hali kuwa wanatuhumiwa kughushi sifa zao. Japo tabia yao haikubaliki inaeleweka na inafafanana na uwezo wao kufikiri.
Kwa kiongozi kama Pinda, alipaswa kungoja angalau uchunguzi wa polisi utoe jibu la nani yuko nyuma ya shambulizi la kigaidi la Arusha. Kama serikali na chama chake hawahusiki, ni kwanini amekurupuka?
Je, Pinda aliamua kujipayukia kwa vile katika wahanga hakuna ndugu yake? Je, angekuwa amepoteza mke, dada au mtoto au baba angekuwa anayesema hayo anayosema? Je, kushindwa kuliona hili si ubinafsi wa ajabu?
Kitendo cha Pinda kutoa amri kwa polisi kupiga watu ni kinyume cha sheria na cha kulaaniwa ukiachia mbali kuwa uvunjifu wa sheria wa wazi. Na hii si mara ya kwanza kwa Pinda kuonyesha uhovyo wake.
Aliwahi kukurupuka wakati polisi walipofanya mauaji ya raia huko Arusha waliokuwa kwenye maandamano ya amani yaliyoitishwa na CHADEMA tarehe 5. 1. 2011 na kusema kuwa hakukuwa na raia wa Kenya aliyekuwa ameuawa wakati alikuwapo akijulikana kwa jina la Paul Njuguna Kayele.
Ni bahati mbaya hata kuwa Pinda hakujifunza kufikiri kabla ya kusema. Ni bahati mbaya kuwa Pinda aliendelea kuamini kuwa angeendelea kukingiwa kifua na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyefikia hatua ya kumtoa nje Mbunge wa Arusha Godbless Lema alipodai Pinda ni muongo.
Tumalizie kwa kumuasa Pinda aombe msamaha kwa vile ni binadamu, yaishe tuendelee na safari. Ila bila ya kufanya hivyo atazidi kuukoleza moto ambao huko tuendako hataweza kuuzima.
|
1 comment:
The question is not who is at the helm of affairs but what is at stake. national interest has continue to determine foreign policy trust of leading economies today. Today is Obama tomorrow may be you. What is directing the course is economic interest. For an elaborate treatment of this topic See the University of Nigeria, Nsukka public lecture on Foreign policy trust 2013 or http://www.unn.edu.ng
Commando171379. UNN.
Post a Comment