Baada ya
kugundua kuwa rasimu ya katiba mpya inanipa power ya kugombea urais kama mgombea
binafsi, leo nawapongeza wananchi walioipendekeza na waliokusanya maoni hata
kama walikuwa wanakwamua mabilioni ya njuluku.
Nampongeza jaji
Jose Warioba kwa kusimama kidete na kuhakikisha anakuja na kitu ambacho kitaua
muungano kistaarabu. Sijui kama jamaa zangu ambao wamekuwa wakilewa na
kulalamikia muungano kama wameipata. Mlitchotaka sasa kitakuwa na tutagawana
mbao baada ya kuvunja hiyo ndoa ya muungao ambayo kwa ulevi wenu mliiona kama
mgongano badala ya muungano. Ila tukubaliane. Ukishavunjika sitaki nisikie vilio
tena. Au vipi mkubali tuendelee kuachana taratibu kwa njia ya kuwa na sirikali
tatu na marais mia kidogo. Sasa muungano umekuwa mgongano dhahiri.
Japo sipendi
utitiri wa sirikali tena kwenye kaya kapuku na ombaomba kama yetu, hili la
kuondosha viti vya ubunge wa kashfa rushwa na kila aina ya unyonyaji limenikuna.
Huenda hiyo pesa waliyokuwa wakikusanya bila kufanya kazi yoyote ndiyo itaenda
kwenye serikali tatu.
Hata hivyo,
msiwe na shaka. Nikishashinda urais nitaondosha sirikali tatu na kutangaza moja
tu. Atakayetaka matatizo apinge mbinu hii adhimu na takatifu ya kuwaunganisha
walevi toka kwenye unafiki na kila kipande kutaka ulaji wa dezo na ujiko. Nasema
wazi tena kwa kinywa kipana. Mkinichagua sahau sirikali mbili au tatu.
Nitaunganisha kaya hata kwa ntutu wa bunduki. Atakayeona hili halifai basi kila
mtu aende kivyake. Wao waende na Zenj yao nasi na Danganyika yetu au vipi?
Kwanini kuendelea kunyimana raha bure? Kama wapo walioshiba ulaji wetu au sisi
wao basi kila mmoja akale kwake ila aangalie isile kwake. Ngoja nibadili
gea.
Hakuna kitu
kilikuwa kinanikera kama kuwa na wabunge tena wakiitwa waheshimiwa
wasiomwakilisha yeyote isipokuwa matumbo yao. Rafiki yangu Sofia Lion na Anae
Andallah mnanipata siyo? Kweli imekula kwenu. Lazima hapa mtafuta kazi ama ya
uhausigeli au kuuza nyanya. Hakuna kitu kimenikuna kama kuondoa upuuzi wa spika
kuwa muishiwa sorry mheshimiwa tena mwenye kupendelea chata lake huku
akiwaburuza waheshimiwa utadhani mjengo mali ya baba yake. Shame on her! Anna
Makidamakida unapata? Umekuwa ukiniudhi kwa kuvurunda kiasi cha
kutamani siku moja nikushukie na kukupa kibano kama si kicha... we koma na ishia
hapo. Hizi bangi na gongo vitakuja kunilaza lupango siku moja. Jobless Nduguy
lazima uwe unalia kama kichanga kwa kunyimwa ulaji ambao ulikuwa ukiutumia kwa
nyodo kana kwamba hakuna mwisho wa kila kitu chini ya jua.
Yawezekana
ni Danganyika pekee yenye wabunge watokanao na vitu vyenye kila aina ya kejeli,
ubaguzi hata udhalilishaji chini ya dhana ya viti maalumu. Kwa wanavyochuma
uchache bila kufanya kazi yoyote, kuna siku walevi watawaita MPigs kama
ilivyotokea kule kwa Nyayo ambayo rais wake unachukua jina la nchi na kuongeza
ta imetoka hiyo. Kuna mlevi husema eti waishiwa hawa huwa hawana na kazi yoyote
mjengoni zaidi ya kungojea posho na sifa ndogo ndogo magazetini.
Jamani naandika kama mlevi asemavyo. Hakuna haya ya wahishimiwa kuanza
kunitafuta waninyotoe roho au kunihoji kama vile niko mbele ya pilato. Mjumbe
hauawi ati.
Juzi nilikuwa
na maongezi na waziri mkubwa wa Ukanada ambaye aliomba nisimtaje jina ili
wafisadi wasimjuejue wakati tukipata ulabu kwenye mitaa ya mji mmoja uitwao
Arawa. Nilimuuliza anaonaje mfumo wa kuwa nauishimiwa wa msukule. Kwanza,
alishangaa inawezekanaje mtu kwenda kwenye mjengo kuwakilisha tumbo lake!.
Alisema wazi kuwa hiki nacho ni chanzo kizuri cha umaskini wa kaya. Aliongeza
kuwa katika kaya yao hili haliwezekani kwa vile lazima kila mtu apambane kuupata
uheshimiwa. Anasema wao wanapambanisha uwezo na si jinsia wala mitandao ya
kifisadi ya kivyama kama ilivyo huko kulikoungua shoka ukabaki mpini.
Nilishangaa aliposema kuwa uhishimiwa wa namna hii ni matusi ya nguoni. Hata
hivyo, nilifurahi kusikia akiongea lugha ya kilevi ya kuliita kulego kulego na
si kijiko kikubwa. Acha nitafsiri kwa lugha rahisi. I call a spade
a spade not a big spoon like some hypocrites who can’t tell those hishimiwas
that they are screwing our hunk up. Shame on them all!
Walevi kusema
ukweli hawajawahi kuona mantiki kwa mfano mtu anapochaguliwa kuwakilisha vijana
kwenye mjengo huku vijana hao hao wakiishi kwnye jimbo lenye mbunge. Je huyu
mbunge wa kawaida ambaye jimbo lake lina kila aina ya binadamu atawakilisha
nani? Je vijana au wanawake wana nini hadi kuwa na wawakilishi zaidi ya mmoja?
Hawa hawana tofauti na wale waishiwa toka Zenj wanaowakilisha majimbo yao kwenye
muuganiko. Inatisha kuona kijipande cha ardhi sawa na wilaya ya Ushoto kuwa na
maulaji kuliko hata mikoa. Japo huwa napenda umoja na kuunganika, nikiangalia
ndoa ya sisimizi na tembo huwa uzalendo unanishinda na kusema waache wende zao
na kipande chao cha ardhi wakamalizane. Sisemi hivi kwa ubaya wala ulevi.
Jamaa
walituzidi akili. Baada ya kugundua kuwa tuna maulaji mengi ya kuwapa hawaachi
kudai kila uchao ili tuendelee kupumbaa. Nimekumbuka kikao cha walevi juzi
ambapo wengi walikandia muunganiko wakisema eti unawanyonya na kuwakosesha
raha. Hakuna ninachokumbuka kama maneno ya mgosi Machungi pale
aliposema, “Ila siku wakiambaa na walevi wabara wakaamua kuwaambia kuwa kila mtu
ave na kwao basi watazamisha kila kipande cha ardhi kutokana na wengi wao
kuzaliana sana upande wa pili.”
Baada
ya kuona mgosi anavuka mipaka kwa kuanza lugha ya kilevi ambayo wasiopenda
ukweli wanaweza kuiita ya kibaguzi, niliamua kuondoka zangu kwenda kusoma kitabu
cha yule Mchungaji kidhabu Mtikisa kiitwacho Sera ya Magabacholi na Saa ya
Ukombozi. Hakuna mstari ulinichekesha kama ule usemao, “Wakituita
machogo nasi twaita machokoo.” Sikukisoma sana kutokana na lugha
ya jamaa. Inaoneka huyu jamaa alisoma volume langu la SAA YA
UKOMBOZI nililotunga kuonyesha jinsi ya walevi wanavyoweza kuongoza wasiolewa
kwa kuwapiga chini kwa njia ya kura ili wakose kula ya dezo kama ilivyo. Hata
hivyo, tuache utani. Wazenj wanaopigapiga kelele kila uchao hasa baada ya
kusikia kuwa kuna dalili ya kuwa na wese wajiandae kama tutaamua kila mtu aende
kivyake baada ya mlevi kutaka kuunganisha pande la kaya na kipande cha kakaya na
kutengeneza kaya moja.
Ngoja nikavute
kwanza!
Chanzo: Nipashe Jumamosi Juni 15, 2013.
No comments:
Post a Comment