Hii si fununu
si umbea na udaku. Kwa vile katiba mpya imetangaza rasmi kutambua mgombea
binafsi, mlevi sasa natimiza azma ya kugombea urais kuwakomboa walevi. Japo
niliwahi kugusia kuwa nina mpango wa kugombea urais, sasa natangaza rasmi;
kwenye uchaguzi ujao nitakuwamo kwenye sanduku la kura.
Juzi nililewa
na kuvuta kama sina akili nzuri. Nilikesha nikisherehekea hatua hii adhimu ya
kuwakomboa walevi toka kwenye mikono michafu ya mafwisadi na majambaziii.
Naona yule anasonya. Mwingine anacheka utadhani
utani. Kwa taarifa yenu, nitagombea urais tena wa muunganiko na si wa
Danganyika. Nataka niwe top boss wa kaya hii ya walevi ili niwaonyesha wavivu wa
kufikiri jinsi ya kuongoza na si kutawala.
Huna haja ya
kucheka wala kushangaa mlevi kugombea. Kama inawezekana kwa mafisi na mafwisadi
kugombea, nini tatizo mlevi kugombea huu ulaji wa dezo? Kwa taarifa yenu, nina
sifa zote za kuwa rais. Kwanza, nina elimu ya kutosha. Nina shahada gunia za PhD
tena si za heshima wala za kughushi kama akina Emmy Nchimvi, Bill Lukuvi, Marry
Nagu, Makorongo Mahanga,Didass Makalio na wengine wengi walioogopa umande ima
wakaishia kughushi.
Pia nina sura
nzuri ya kuvutia wapika kura ya kula. Afya yangu ni fiti. Hata nikinywa, kubwia
na kuvuta sianguki kwa vile niko gado kishenzi. Hivyo, kwa sifa za haraka haraka
mie ndiye kidume pekee anayefaa kuwa rais wa kaya hii inayohitaji mkombozi
ambaye imemngojea kwa miaka mingi. Mie ni yule aliyetabiriwa na manabii kama
Mchonga huku nikapigwa vita na mashetani kama yule habithi Shehe Yaya.
Pia nina
mitandao ya kutosha ambayo lazima iingie viwanjani na kunisakia kura kwa udi na
uvumba. Sina haja kuiibia Banki Kubwa wala kujiingiza kwenye biashara ya
Kikagoda wala kuwatoa kafara walevi kwa wachukuaji waitwao wawekezaji. Mie ni
mzalendo wa kupigiwa mfano.
Ili
kuwashawishi walevi wanipe kula, nina mpango wa kufanya yafuatayo.
Mosi,
nitatangaza mali zangu za bi mkubwa na vitegemezi na marafiki zetu.
Pili, nitaarifu
walevi kuwa nikiingia madarakani, nitapunguza baraza la mawaziri. Nina mpango wa
kuwa na mawaziri 20 tu ambapo watapatikana kwa njia ya kuomba kuajiriwa na si
kuteuana wala kulipana fadhila.
Tatu,
nikiishaingia madarakani, nitafuta cheo cha First Lady. Hili nalo juzi lilitaka
kuvunja ndoa yangu na bi Mkubwa. Nilimwambia fika kuwa nikiwa rais sitaki
nisikie habari za NGO za uongo na ukweli wala yeye kwenda kushindania vyeo vya
kichovu kwenye chama changu na Pilau Mahanjumati Ulabu na Pilau (MUP).
Juzi kulikuwa
hakukariki nyumbani kwangu. Maana baada ya kumwambia bi mkubwa kuwa sina mpango
wa kumruhusu aitumie ikulu kufanya biashara alitangaza mgomo wa kila kitu
kuanzia jikoni hadi kwenye bedroom. Nilipomtaarifu yaliyowapata marais kama Lora
Gbagbo ambaye ananyea debe na mkewe, alinielewa. Bila kumuelimisha nadhani
angeanza kuhujumu harakati zangu ya kuwania ukuu. Maana, baada ya kusema wazi
kuwa utawala wangu hautakuwa biashara ya familia kama wale, bi mkubwa na
vitegemezi vyetu walianzisha kigwena kuhakikisha sipati ukuu. Baadaye
niliwahakikishia kuwa serikali yangu haitakuwa family business wala ya ubia kwa
vile ni hatari ikitokea ukaondoka madarakani.
Baada ya
waambia vitegemezi vyangu yanayomkuta yule jamaa wa Masri Mubaraak Kibaraak na
wanae walinielewa wakakubali kuwa lazima kila mtu ale jasho lake. Ili
kumridhisha bi mkubwa, nilimwambia kuwa kama katiba mpya isingefuta ubunge
msukule bin underwear aka viti maalumu,ningempachika pale.
Nne, ili
kuhakikisha nashinda, nitaanza kutangaza sifa zangu kaya nzima. Nina mpango wa
kupeleka picha zangu wa wataalamu wa picha ili wafanya photoshopping niweze
kuonekana kijana kuliko nilivyo. Kuanzia juzi napaka piko kuficha
mvi. Pia naitwa mzee kijana.
Tano,
nitahamasisha walevi wote kaya nzima wanipigie kampeni ya baa kwa baa.
Sitaruhusu upuuzi wa kitanda kwa kitanda ili wasiambukizane miwaya kama wale
wachovu waliokuwa wakitumia kampeni hii ya kimalaya. Wala sitaruhusu mambo ya
mafiga matatu maana asili yake nayo ni uchangu.
Kwa
waliofuatilia mikakati yangu siku zilizopita wanakumbuka nilivyotangaza neema
kwa waandishi wa habari. Nawashauri kuanzia sasa wanipigie kampeni nishinde
kitsunami na kuondosha kadhia ya kutekwa na kunyofolewa kucha na kutobolewa
macho. Nawashauri wanoe kalamu ila wasitegemee kuteuliwa ukuu wa wilaya na mkoa.
Wanipigie kampeni wakijua kuwa nia yangu si kulipana fadhila bali kukomboa kaya
toka kwenye mikono michafu. This time around the kaya won’t go to the dogs
anymore. Believe ye me everybody.
Kwa wasiojua
chama changu kitukufu ni kwamba sera yangu kuu ni kuhakikisha kila mtu anapata
uwezo wa kuweka mahanjumati na pilau mezani huku akishushia na ulabu. Nani
asiyependa ulabu iwapo tunaambiwa hata peponi utakuwapo? Kwanini tusianza
kuuramba ulabu kabla ya hata ya kufariki na kuingia huko peponi? Kwa maana
nyingine ni kwamba sera yangu ni kuwaingiza walevi peponi kabla ya kurejesha
namba. Mnaonaje sera hii walengwa?
Tano, ili
kupata kura ya kula, nina mkakati wa kufanya kile wazungu huita miracles.
Nitawambia baadaye hiyo miujiza.
Sita,
nitafutilia mbali mikoa na wilaya vilivyoanzishwa kisiasa na kutengenezeana
ulaji kichovu na kifisadi.
Saba,
nitahakikisha naweka sera ya kuzuia watumishi wa serikali kuwa na nyumba ndogo;
zinamaliza pesa ya kaya bila sababu. Pia ni mwiko kwa mtu kuiba wala kuficha
pesa nje ya kaya.
Saba, ili
kuepusha mzigo kwa walevi, sitakuwa nikifanya ziara ughaibuni mara kwa mara.
Nane,
nitasafiri ughaibuni mara nne kwa mwaka.
Tisa, nitakuwa
nikiandamana na watu wachache ambao majina yao hayatafanywa siri kama ilivyo.
Kumi,
tumekubaliana na bi mkubwa kuwa hataruhusiwa kudandia safari zangu unless
otherwise.
Kumi na moja
nimemshauri bi mkubwa atumie muda wake mwingi kujitafutia elimu badala ya
kufikiri juu ya NGO za kufanyia biashara ikulu. Maana elimu yake ni ya UPE na
alikuwa mwalimu wa chekechea.
Kumi na mbili
nawataarifu wapiga kura na mashabiki wangu kuwa sitajiingiza kwenye biashara
yoyote. Sitanyakuwa kiwanda wala mgodi wala sihitaji kuwekewa kinga kwenye
katiba.
Kumi na tatu,
nitabadili katiba na kutamka wazi kuwa rais akiiba,kufanya biashara ikulu au
kushiriki ufisadi anyongwe.
Kumi na nne,
natangaza kuwa hata nitakapokuwa nikisafiri kwenda uwanja wa ndege au
matembezini sitahitaji misiruru ya magari na wala body guards. Vya nini iwapo
sina mpango wa kumuibia mtu wala kuridhi tabia za kikoloni kama wengine?
Kumi na tano,
nina mipango gunia. Mengine nitawaeleza siku za baadaye.
Kumi na sita,
nawashauri wote mniamini na kunipa kula ili mpate kula. Hata nikiwaingiza mkenge
mvumilie na wala msilalamike.
Kumi na saba,
kula la heri.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Juni 8, 2013.
2 comments:
kila la kheri..ila hizo ahadi naona kama zimezidi zipo 19 si kumi na saba....
Da Yacinta shukrani sana. Unajua tena. Ukiandika umetoka kuuweka lazima mambo mengine yajiweke. Ahadi zisikutie hofu. Mbona Njaa Kaya alitoa ahadi milioni bila kutekeleza hata moja na bado anapeta. We nitafutie kura ya kula nami nile dezo kama Njaa Kaya na jamaa zake au vipi?
Post a Comment