The Chant of Savant

Friday 14 June 2013

Muungano: Tuache ulafi na ubinafsi tuwe na serikali moja


Hali ilivyo ni kwamba Tanzania iko msambweni kutokana na rasimu ya Katiba mpya kupendekeza ziwepo serikali tatu bila kujali mzigo anaoongezewa mlipa kodi maskini. Inashangaza kwenye nchi maskini na ombaomba kufikiri kuwa na serikali tatu. Kwa kumbukumbu yangu ni kwamba Tanganyika ilipoungana na Zanzibar na kuunda Tanzania, rais wa kwanza wa Zanzibar hayati mzee Abeid Aman Karume alitaka kuwepo serikali moja. Jambo hili lilikataliwa na rais wa kwanza wa Tanganyika hayati Mwl Julius Nyerere kwa madai kuwa ingeonekana kama Zanzibar imemezwa.
Ajabu sasa wanaoshupalia kuwapo kwa serikali tatu ni wazanzibari zaidi ya watanganyika. Kwanini imezwe Tanganyika isiwe issue ila iwe issue ikimezwa Zanzibar? Kimsingi kama ni kumezwa zinamezwa nchi zote mbili na kubakia nchi moja Tanzania.
Mie napendekeza tuungane kiukweli kwa kuwa na serikali moja na nchi moja ili kuimarisha muungano na kuwaondolea kero na mzigo wapiga kura.
Ni rahisi watu kupendekeza serikali tatu kwa sababu haziendeshiwa na pesa yao binafsi. Hata hivyo kuna gharama hapa. Kama tutapitisha serikali tatu basi pesa iliyokuwa ikiiendesha serikali ya Mapinduzi Zanzibar itumike kuendesha serikali ya Tanganyika ambayo haikuwepo kwa kitambo kirefu. Au vipi serikali mbili kila moja kwa namna yake bila kujali udogo au ukubwa zitoe pesa za kugharimia serikali ya muungano. Je hili ni rahisi? 
Kuogopa kumezwa ni woga na fikra ya kizamani. Mbona nchi ya Hawaii ambayo ni sawa na Zanzibar hailalamiki kumezwa na Marekani wala PEI  Kanada hailalamiki kumezwa?
Kuna haja ya kuepuka unafiki, ubinafsi na uchoyo na kuungana kwelikweli. Muungano ni kama ndoa ambayo huwaunganisha wawili na kuwa mwili mmoja. Muungano wa sasa ni sawa na mahusiano ya kinyumba ambapo kila mshiriki huwa na maisha yake independent of another.
Naomba kuwasilisha.

No comments: