Monday, 18 April 2016

Akina Kilango wasipangiwe kazi nyingine


            Hivi karibuni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, John Pombe Magufuli, aliwaacha wengi hoi pale alipomtumbua jipu aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anna Kilango Malecela baada ya kumpelekea taarifa zisizo za kweli. Bila kusita wala kuficha, rais aliamua kutengua uteuzi wake jambo ambalo limewafurahisha wengi licha ya kuwa onyo kwa wengine. Wengi walishangaa; hasa ikizingatiwa kuwa Malecela alikuwa ana siku 30 tu kwenye nafasi hiyo. Kitendo hiki–licha ya kumstua mhanga–kitakuwa kiliwastua wengi na kuwa kama onyo kuwa hapa hakuna mchezo unapovurunda. Nashauri rais akaze Kamba na kumulika si kuhusu wafanyakazi hewa bali masuala mengine kama vile usafi, uchapakazi, ufuataji sheria (maana tangu aanze kung’ata, mawaziri wake wamekuwa wakifanya kazi ya zimamoto ili kumfurahisha badala ya kufuata sheria) uadilifu, ufanisi na mengine mengi yanayoendana na uongozi. Namshauri rais ajenge uongozi badala ya utawala. Maana wakuu wengi wa mikoa na wilaya walikuwa wanajiona kuwa watawala zaidi ya viongozi wakati jukumu lao ni kuongoza na si kutawala. Wapo waliofikia kujiona ni marais kwa vile wameteuliwa na rais. Ukale huu unapaswa kukomeshwa. Hapa ndipo mtihani kwa rais Magufuli uliopo. Kwani mara nyingi, amekuwa akisisitiza umuhimu na ulazima wa kuwatumikia wananchi na siyo kuwatumia kama ilivyokuwa imezoeleka wakati wa utawala wa kiza uliofikia hata kufuta magazeti yaliyouambia ukweli.
            Hata hivyo, tuseme wazi; pamoja na rais kufanya maamuzi mazuri na haraka na kwa wakati, ametuacha hoi kiasi cha kuhisi kama anajipinga kama siyo kuanza kutuchanganya na kujichanganya. Kwani, akitengua uteuzi wake, alikaririwa akisema kuwa Malecela atapangiwa kazi nyingine! Kazi gani nyingine na ipi wakati ameishavuruga wazi tena ndani ya muda mfupi? Anampangia kazi nyingine ili aende huko nako kuvurunda akitaraji kupangiwa kazi nyingine? Kuendelea kuwapangia kazi nyingine wavurundaji baada ya kuvurunda nyingine ni kuotesha majipu mapya tena sugu ambayo yatalisumbua taifa. Mbona wezi wa bandarini hawakupangiwa kazi nyingine zaidi ya kufikisha mahakamani. Hata kumpelekea taarifa za uongo rais ni kosa la jinai. Kwani, kufanya hivyo, kunaweza kuvuruga mipango ya taifa na kusababisha hasara na usumbufu kwa wananchi. Kosa jingine walilotenda akina Kilango ni kutaka kubariki wizi wa fedha za umma kwa kuficha wafanyakazi hewa. Ina maana rais asingestuka na kutuma wachunguzi wake, wafanyakazi misukule waliokuwa wamefichwa na akina Kilango wangeendelea kulipwa mishahara kinyume cha sheria jambo ambalo ni wizi tu wa kawaida.
             Hoja nyingine ni kwamba kama rais alikuwa na haja ya kuendelea kumwajiri au kumteua mhusika basi angempa onyo kuliko kumfukuza kwa mkono wa kulia na kumrejesha kwa mkono wa kushoto. Huku ni kujipiga mtama kiutawala. Tanzania si maskini wa nguvu kazi. Wapo wenge walio tayari na wanaoweza kuchukua nafasi hiyo na hiyo nyingine anayotaka kupewa mtu aliyefeli wazi. Kwani, lazima yeye? Kupangiana kazi nyingine kunatokana na tabia chafu za kikale ya kuhamisha watu wanapovuruga sehemu itamgharimu rais; na itamwonyesha kama mwenye hangover ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo kimsingi, ndilo chimbuko la uoza na ufisadi vinavyomsumbua rais. Tanzania ina watu wengi wasio na kazi tena wenye taaluma na uzoefu tu ambao hawatokani na familia za kikubwa au vigogo wa chama. Hivyo, tungeshauri akina Malecela waachwe nje wakaonje joto ya jiwe ili liwe somo kwa wengine. Kwanini mtu ahangaike wakati akijua kuwa akivuruga atapangiwa kazi nyingine?  Mbona baadhi ya wabovu waliotimliwa Ikulu hata kabla ya rais kuingia hawakupangiwa kazi au kuna watu na viatu?
            Tumhamasishe rais abadili kila kitu hasa mfumo na utaratibu wa kizamani. Mambo ya kupangiana kazi nyingine ni ya kizamani. Kufanya hivyo ni kujichanganya na kujidanganya. Unaweza kuwaonea huruma baadhi ya watu chini ya mashikamano ya chama au ukaribu.  Mwisho wa siku, watakuangusha na kukuacha ukisononeka kwa aibu. Tanzania ni kubwa. Pia ina watu wengi tena wenye sifa kedekede. Kama msumemo kata mbele na nyuma bila kujali nani ataumia kama astahili.  Haki ni haki daima; huvunja hata milima. Lazima tufike mahali tukubali kubadilika kabla hatujabadilishwa na mahitajio ya wakati. Kwa wanaojua maana ya demokrasia na uongozi unaotegemea utashi wa watawaliwa, Malecela hakupaswa kufikiriwa kuteuliwa; achilia mbali kuteuliwa. Je wako wangapi kwenye wateule wa Magufuli walioshindwa kwenye kura za maoni lakini wakazawadiwa vyeo kama sehemu ya kupeana ulaji? Je hili si jipu tena sugu na linalonuka? Tafadhali rais Magufuli, usigeuke nyuma ukageuka jiwe–tena jiwe lenyewe la chumvi–kama mke wa Luti. Tufikie mahali tuweke uzalendo mbele tukijua na kuamini kuwa Tanzania ni zaidi ya kundi dogo la watu wanaojuana, kulindana na kufadhiliana.
              Hata kwa Malecela kuteuliwa ilikuwa ni makosa ingawa hatulengi kukosoa mamlaka ya rais kufanya hivyo. Kwanini kuteua watu walioshindwa kwenye kura za maoni jambo ambalo linaonyesha ni namna gani umma–tena wa watu wa kwao–uliwakataa baada ya kushindwa kuhudumia vilivyo kwenye vipindi vyao vya ubunge?
            Tufunge hoja kwa kumtaka rais asiposimbuke na kondoo mmoja aliyejipoteza wakati kuna kondoo wengi wasio na hatia.
Chanzo:Mwanahalisi

No comments: