Friday, 22 April 2016

Makonda asimhadae rais na dunia


            Akitoa salamu za mkoa wa Dar Es Salaam hapo Aprili 19, Mkuu wa mkoa, Paul Makonda, aliwaacha wengi hoi alipojitahidi kujifagilia na kulinda kitumbua chake. Alisema kuwa tangu ateuliwe kuwa mkuu wa mkoa, vijana wengi wamejenga imani na matumaini makubwa kwa rais John Pombe Magufuli. Yeye ni mkuu wa mkoa wa Dar. Je amezunguka lini nchi nzima kuongea na kupata mawazo ya vijana wengi na wengi kiasi na wa wapi kama si uongo (uingi ni dhana tegemezi). Huwezi kujenga hitimisho la jumla kama hili ukaheshimika au kuaminika kisomi. Je Makonda aliongelea vijana wapi kati ya wale wanaofaidi matunda ya taifa na wale wasio na wa kuwakingia kifua kama alivyofanyiwa na rais mstaafu Jakaya Kikwete baada ya kutuhumiwa kumdhalilisha mzee Joseph Warioba? Je anaongelea vijana wapi kati ya wale wa CCM na wa upinzani au wa vijijini na mijini?
            Kuna haja ya maafisa wa umma kujiamini na kuacha kujikomba na kujidhalilisha ili wasitimliwe kwenye ulaji wao. Makonda aliwaacha wengi–hasa wale waliomwangalia usoni na kusikiliza na kuchambua alichosema–wakati akitoa madai haya ya ajabu kidogo. Alisema eti vijana wamekuwa wakimuuliza kama rais Magufuli huwa anacheka. Ajabu kwenye mstari huo huo Makonda alisema kuwa Magufuli hutumbua majipu akiwa anacheka! Sasa kama anafanya kazi ya kuumiza kama vile akicheka, vijina hao (wa kubuni bila shaka) walitaka kicheko gani wakati ni rahisi kwa Magufuli kucheka hata kama anafanya kazi ya kuhuzunisha? Nadhani alichofanya bila kujua ni kumjenga Magufuli kama mtu mkatili anayeweza kucheka mahali anapopaswa kununua hata kulia. Hadithi za Makonda zinanikumbusha nilipokuwa kidato cha pili. Wengi wa marafiki zangu nami tulizoea kujitambulisha kwa vijana wa form one kama form fours wakati tulikuwa form two tu.
            Tunachojifunza hapa si sababu ya kuongopa bali ile hali ya baadhi ya watu kujidhalilisha kwa kila njia hata za uongo bila kujua kuwa kuna watu wenye akili (tena wasomi na wachambuzi) wanaowasikiliza ukiachia mbali wanaowalenga nao kuwa na akili. Hii maana yake ni kwamba watu wa namna hii (wasiojiamini) wana kila uwezekano wa kuwachusha hata kuwakera wale waliowaamini madaraka wasijue udhaifu wao. Watu wa namna hii ni rahisi kufanya makosa tena ya kijinga tu. Japo suala la kama rais anacheka au ananuna au vinginevyo si muhimu, kwa mlengwa mwenye kuwa makini linaonyesha ni namna gani mteule wake anavyomuona au kutaka wa kuweza kudanganywa na maneno matamu hata kama ni ya uongo. Sidhani kama Magufuli alifurahia sifa kama hii isiyo na msingi. Sijui kucheka au kununa kwa rais ni tatizo ambalo linawakabili hao vijana waliomtuma Makonda. Nadhani–kama kweli–wangekuwapo vijana wa kumtuma Makonda kwa rais, basi wangemtuma aulize ni kwanini anawapa vyeo wazee na walioshindwa kwenye uchaguzi wakati vijana wapo na hawana ajira na mahitaji mengine ya msingi.
            Si mara ya kwanza kwa safu hii kuandika juu ya Makonda. Tunajitahidi kumfuatilia ili kuona mwisho wake utakuwa vipi hasa ikizingatiwa kuwa uibukaji wake una wingu zito ambalo–hata kama wenye mamlaka ya kuteua hawakuliona au kulipuuzia–kuna siku litajidhihiri na ukweli kudhihirika bila uficho wala kuwa na dirisha na kuuzuia au kuubadili,
            Sioni kama kuna sababu ya kudanganya au kugeuzana mabwege wakati lengo (kama kweli ni hilo) la kuwa kwenye ofisi za umma ni kuutumikia na si kuutumia umma. Sidhani kama rais anahitaji vibwagizo hata visivyoingia akilini kama ilivyokuwa kwa Naibu waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Chato Dkt. Medard Kalemani hapo tarehe 29 Machi akiwa Chato tena mbele ya rais akisema kuwa atatundika umeme hata kwenye matoroli na juu ya miti. Hii haingii akilini; na wala haimfurahishi unayemlenga. Ukitaka kujua inasikika na kutafsirika vipi, vaa viatu vya unayemlenga. Hizi ni siasa za kujikomba na za kibabaishaji. Nani anataka sifa za kipuuzi?
Hii inanikumbusha mwanasiasa mmoja wa Kenya ambaye hakujua Kiswahili vizuri. Katika kumfurahisha rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi, alistukia (tena kwa bahati mbaya ya kutojua Kiswahili) akisema, “Piga makofi Daniel arap Moi” badala ya mpigie makofi.
            Kisa hiki cha Moi hakina tofauti na hiki cha Makonda cha kujumlisha (generalization) vijana wote kuwa wamefurahia kuteuliwa kwake. Sijui kama vijana kama watoto wa akina Mzee Joseph Warioba aliyemnyanyasa wamefurahia uteuzi huu ambao kimsingi umetokana na kadhia hii. Ni bahati mbaya kuwa Makonda na wale waliomuumba na kumteua hawataki kugusia kashfa ya kumdhalilisha Mzee Warioba. Sidhani kama vijana wasio na tabia ya kujikomba wanafurahia uteuzi wa Makonda. Kimsingi, Makonda, sawa na wateule wengine, wanapaswa kuwa wakweli kuwa uteuzi wao umewafurahisha wana familia na marafiki zao lakini si vijana wote wa Tanzania au Dar Es Salaam. Sijui kama vijana wa Ubungo ambao mbunge wao aliwekwa ndani kwa kuwatetea walipokuwa wakihujumiwa na waajiri wao wana furaha anayosema Makonda. Ni bahati mbaya kuwa waliomuumba na kumteua Makonda hawakutaka kuliona hili kama lilivyo. Badala yake wameingiza ushabiki wa kisiasa na kuweka historia mbaya kwa vizazi vijavyo. Wakati mwingine najiuliza mtu wa kuteuliwa na mtu mmoja kupewa madaraka na jeuri ya kumweka ndani mwakilishi wa umma wakati anawakilisha tumbo lake na yule aliyemteua tofauti na mbunge anayewakilisha wananchi kwa malaki. Tunamkomoa na kumdanganya nani na kwanini na kwa faida gani na ya nani wakati cheo ni dhamana tena ya muda tu?
Chanzo: Mwanahalisi. 

No comments: