The Chant of Savant

Monday 18 April 2016

Wageni wanaokwepa kodi wafukuzwe nchini


Unaweza kusema Tanzania ni nchi ya ajabu sana. Pamoja na kugeuzwa–hata kuitwa shamba la bibi–bado inaendelea kuvumilia uhujumu uchumi wa ajabu huku watu wake wakiendelea kuwa maskini. Taarifa za wageni kukwepa kodi hata kutorosha fedha na nyara za taifa zinaanza kuzoeleka. Ndani ya mwaka mmoja, yameripotiwa matukio ya wafanyabiashara wa kichina ima kutorosha fedha, kukwepa kodi au kutoa Ankara zenye kuonyesha fedha pungufu tofauti na waliyopokea. Inashangaza sana jinsi watuhumiwa wanavyoendekezwa. Kosa la kukwepa kodi ni kubwa hata katika mataifa tunayoona yameendelea ambayo ustawi wake umetokana na kukusanya mapato na kuadhibu vikali wanaokwepa kodi.
Nchi za magharibi zina makosa makubwa ambayo mtu akiyatenda anapoteza haki ya kugombea uongozi. Mojawapo ya makosa haya ni kukwepa kulipa kodi, kuficha mapato, kushindwa kutangaza mapato, ushiriki ugaidi na mengine mengi. Haya ni makosa yasiyo na mjadala wala msamaha anapoyatenda mtu. Kinachoshangaza, inakuwaje Tanzania haiigi mfano toka nchi hizi ambazo nyingi huifadhili. Haiwezekani taifa likaruhusu wamachinga toka nje kuja kufanya biashara na shughuli ambazo watu wetu wanaweza kuzifanya. Kuendelea na mchezo huu–licha ya kuwa motisha kwa wageni wahalifu kujazana nchini–ni ushahidi kuwa hatuko makini. Hata hawa wanufaika wa upungufu huu licha ya kutuibia, wanatudharau na kutuona kama hamnazo. Mswahili akikwepa kulipa kodi, kutorosha fedha au nyara huko uchina, atafia gerezani kama siyo kunyongwa. Kama taifa–tufikie mahali–tufanye vitu kama watu wenye akili na si mataahira na wapumbavu wasio na akili wala wasioweza kujifunza toka kwa wengine. Hivi inahitaji shahada ya sheria au biashara kujua kuwa wageni hawapaswi kufanya shughuli au biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa? Je hili nalo linangoja wafadhili walisemee ndipo tustuke na kuchukua hatua? Si uzushi. Ongezeko la wamachinga toka nje hasa Uchina, Uturuki na India ni ushahidi kuwa mfumo wetu ni wa hovyo na wa kijinga unaopaswa kubadilishwa haraka. Tunatoa changamoto kwa rais John Magufuli kuliangalia hii kwa upana na makini sana ili kuepuka kuendelea kuwa maskini kwa kujitakia kutokana na mfumo na sheria mbovu. Pia kuna haja ya kuwalaumu wananchi wetu wanaoshirikiana na wageni kuibia taifa lao halafu hili likishatokea hao hao wanaanza kulalamika wakati nao ni sehemu ya jinai hata kama si wote.
Kwa vile wageni si watu wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi, adhabu inayowatosha na kuwafaa ni kuwatoza faini kubwa, kutaifisha mali zao na kuwafunga kisha kuwafukuza nchini. Pia serikali isimamie sheria zinazotamka wazi uwekezaji ni nini badala ya kuwaacha wageni kuja kuchukua kazi zetu huku watu wetu–hasa vijana–wakiendelea kusota kwa kukosa kazi na kipato. Sijui kama machinga wetu wanaweza kwenda Uchina na kufanya shughuli za kimachinga na mamlaka za kule zikawanyamazia tu.
Wakati wa Tanzania kugeuzwa shamba la bibi au kichwa cha mwendawazimu umekwisha. Watanzania lazima tustuke na kuamka na kuacha kushirikiana na wageni eti kwa vile wanatuhonga mabaki ya chumo la wizi wanalotuibia. Unashangaa namna wageni wanavyokuja nchini–wengine hata kinyume cha sheria–na kupangishwa nyumba, kupewa leseni za kufanya biashara ya kimachinga. Unashangaa zaidi kuona wizara ya Mambo ya Ndani ikiendelea kuwatumia polisi wake kuwasumbua wananchi wakati wageni na wakimbizi haramu wa kiuchumi wakizagaa nchini. Lazima tuwe makini kwa kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na kitambulisho cha uraia, anwani ya kudumu na kuhakikisha mfumo wetu unakuwa wa kompyuta ambapo kila mtu atakuwa na namba maalumu ya utambulisho yaani Social Insurance Number (SIN) au namba yoyote itakayoamriwa na mamlaka ili kuwatambua na kuwahudumia watu wake. Nikitolea mfano hapa Kanada, huwa serikali haitumii fedha nyingi kulinda mipaka yake. Badala yake, serikali ya hapa imetoa namba kwa raia na wakazi wa hapa na kuziweka kwenye mtandao wa kompyuta. Kila unapokuwa nchini Kanada, ukitaka kupata huduma kama ya kupanga nyumba, kupata leseni ya udereva, kujiandikisha au kuandikisha mwanao shuleni, kupewa huduma hospitali, huwa unaulizwa namba yako na hadhi yako ya kuwa Kanada. Bila kuwa na namba ya utambulisho–licha ya kutoweza kupata taarifa–utalipotiwa polisi na kuchukuliwa hatua mara moja. Sisi tunashindwa nini kuiga hili. Ajabu, badala yake watu wetu wanaigizi mambo ya kipuuzi kama kutoga masikio, kuvaa milegezo na upuuzi mwingine. Wakanada hawamwamini yoyote hasa mgeni; na huwezi kuishi hapa au kufanya biashara au shughuli yoyote chini ya meza. Mfumo huu–licha ya kuhakikisha usalama wa nchi–unasaidia kupunguza kutumia fedha nyingi mipakani ukiachia mbali kukatisha tamaa wageni kuingia nchini.
Bila kubadili sheria na mfumo wetu, tutaibiwa sana hasa wakati huu wa utandawazi na kukua kwa teknolojia ambayo wahalifu huitumia kufanya uhalifu.
Tumalizie kwa kuitaka serikali ibadili na kutunga sheria zenye mashiko na meno ili kupambana na wakimbizi wa kiuchumi wanaoibia taifa letu huku watu wetu wakiendelea kuwa maskini bila sababu za msingi.
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili 17, 2016.

No comments: