The Chant of Savant

Friday 22 April 2016

Uliwahi kufurahi kutangaza kifo?


Naona yule anatikisa kichwa akidhani mibangi na ulabu vimeanza kunitia kichaa. Si kichaa wala roho mbaya au kuwanga vinavyonisumbua kufurahia kutangaza kifo au vifo vya gendaeka. Nina sababu tena zenye siha na mashiko. Hivi uliwahi kujiuliza kama hawa gendaeka wanaoibia kaya yetu kana kwamba ndiyo mwisho wa dunia  waliwahi kufikiri kuwa kuna bwana death? Nauliza hivi kutokana na ninavyowaza na kuyaangalia maisha hasa uhai kama msomi, fyatu na mja mwenye adabu.
Baada ya kugundua kuwa kaya yetu–kwa miongo zaidi ya mitatu–ilitawaliwa na kuliwa na gendaeka tuliofanya kosa kuwaamini madaraka tukidhani ni wenzetu, niliamua kujiuliza kama ingekuwa ni mimi ningefanyaje. Jibu nililopata ni kwamba nisingefisidi wala kuibia kaya kwa vile kuna siku nitarejesha namba tena niondoke mtupu kama nilivyokuja. Hivyo, wanaodhani niandikacho ni mibangi na uchizi nadhani hapa tutaelewana.
Siku rais Braack Obamiza alipotangaza kifo cha Osami bin Laden, hakuwa na chembe ya huzuni hasa ikizingatiwa; huyu jamaa alikuwa ameishasababisha vifo vya jamaa wengi wasio na hatia tokana na wendawazimu wake. Hivyo nami ninaposikia fisadi mmoja amerejesha namba huwa nafurahi kama sina akili nzuri. Kwanini? Simple; ufisadi umeishaua walevi wangapi tokana na kusikinishwa na wanahizaya hawa? Mie wakirejesha namba nafanya sherehe kama ilivyotokea niliposikia kuwa jambazi moja lililokwapua mabilioni kwenye Belly of Tembo (BoT) liitwalo Matusi Liyumbayumba lilirejesha namba. Hakuna siku nilikogeka kama siku Dadi Balaliii, yule jambazi, aliyewezesha ujambazi wa EPA aliporejesha namba kama kweli amerejesha namba.
Hivyo, leo ninapoandika waraka huu ili kuwafikirisha wanaofikiri kwa masaburi wasijue kuna kesho, nina furaha. Hata hivyo, nina huzuni hasa mafisi na mafisadi yaliyotumiwa na wanene zaidi yanaporejesha namba; kwani huwa furaha kwa mabwana zao ambao mara nyingi–ima huwadedisha ili kuficha chafu yao–au kuomba wafe ili siri zao ziwe salama. Unadhani baada ya fisadi hili jambazi kufa juzi wale waliolitumia lilipokamatwa na simu lupango likitaka kuwasiliana na munene hawajafurahi?  Najua wengi wananiona kama mwanga kufurahia msiba wa gendaeka. Nifanye nini iwapo nayo yanafurahia mateso na vifo vya walevi yanayosababisha tokana na kutoidurusu kesho na maisha ya waja? Hata liliporejesha namba lile jambazi la kigabacholi lililokuwa likimwita first lady wa mzee Ruxa shem, nilisherehekea kwa kuvuta mibangi na kunywa kama sina akili nzuri.
Siku mijambazi ya Kagoda, EPA, Escrow na mingine ikirejesha namba lazima nisherehekee; kwani namba ya wauaji itakuwa imepungua kinamna. Guess what. Nimefikia hatua hii–ambayo wasionijua vizuri wanaweza kusema ni kuwanga au kukata tamaa–baada ya kugundua kuwa sheria zetu za hovyo na za kikale huyasaidia majambazi kama haya hata kutoozea lupango. Kwa vile wenye madaraka tena ya kuazima ya hapa duniani wanakula na majambazi na kuyakingia vifua kama alivyofanya Njaa Kaya kwa jamaa wa mihadarati, ufisadi, ufichaji njuluku ughaibuni, mafisadi na majambazi, bwana God ameamua kutulipia wanyonge tunaonyongwa kwa umaskini wa kutengenezwa na hawa wajalaana audhubillahi mina sheitwaan rajiim.
Hebu tuwe serious kidogo. Hivi ukisikia mijambazi kama vile Jimmy Rugemalayer, Singasinga, Roast Tamu na mingine imenyotoka roho utafurahi kiasi gani? Hebu nieleze; ukisikia mijambazi kama hii iliyoibuliwa juzi kwenye kituo cha mabasi yaendayo mikoani imenyotoka roho utafanyaje zaidi ya kumshukuru Subhana? Adui yako muombee kifo siyo njaa maana anaweza kuwa na uchache akala na kunenepeana wakati wahanga wake wakiteketea.
Je ni walevi wangapi wanajazwa ujinga na umaskini kutokana na ufisadi ulioua mifumo yetu? Je ni wangapi wanapoteza maisha kutokana na kutopata huduma wakati wakubwa wanaopaswa kusimamia haki wanakwenda kutibiwa hata mafua Ulaya na India? Hebu fikiria. Kama fyatu kama mimi naudhiwa na ujambazi unaoendelea kayani hivi, hao wenye akili timamu tena waathirika wasio na bangi na ulabu wa kuwatuliza wana hasira kiasi gani? Uzuri ni kwamba kul nafsi zalikatu maut yaani kila nafsi itaonja mauti. Naongea kishehe kidogo kuonyesha kuwa mimi si Maimuna ati.
Mlevi nina uga madhubuti adhimu na adimu wa kutolea hasira zangu ambao kwa kitaalamu huitwa venting. Je ni wahanga wangapi hawana pa kutolea hasira zaidi ya wanyonge zao kama vile bi wakubwa zao mambo yanapoharibika? Je hawa mafwisadi wameishavunja ndoa ngapi ukiachia mbali kusababisha vibaka kuchomwa moto baada ya kusikinishwa? Laiti wachovu wa kaya hii wangekuwa na akili na usongo kama vyangu, wasingehangaika kuwachoma moto vibaka–ambao hata hivyo siwatetei–badala ya kuchoma mibaka? Au wanangoja mkono wa Bwana God tu utende haki?
Leo sichongi sana. Nina furaha ajuaye Bwana God. Anapokufa fisadi mimi kwangu sherehe. Ngoja nikitoe nikapate misokoto na ulabu kusherehekea maamuzi ya haki na sahihi ya Bwana God kwa wachovu na walevi. Nina furaha kutangaza kifo cha fisadi nonihino kilichotokea kule kwa wazito na habari ziwafikie wahanga wote ili washerehekee.
Chanzo: Nipashe.

No comments: