The Chant of Savant

Sunday 24 April 2016

Chini ya Kikwete tulikuwa taifa la walevi


            Sina nia ya kumkandia rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye huwa sipendi kumuita dokta kwa vile hajasomea shahada ya uzamifu. Ila naweza kueleza kuwa chini ya utawala wake–kama ulivyoumbuliwa na aliyemrithi–ulikuwa wa kilevi kwa namna fulani. Hapa ninaposema ulevi lazima nieleweke. Simaanishi ulevi wa pombe bali kujisahau na kuwasahau wanyonge. Leo nitajaribu kudurusu namna sekta muhimu ya elimu ilivyokuwa imetelekezwa na tukashikilia–au kutoa vipaumbele kwa mambo ya kilevi tu–huku wanafunzi wakizidi kuumia. Leo nitajaribu kulinganisha baadhi ya huduma na watendaji na elimu na walimu.
            Hakuna tatizo linaloihangaisha serikali ya rais John Pombe Magufuli–kati ya mengi–kama la ukosefu wa madawati mashuleni hasa shule za msingi. Unashangaa kwa mfano kukuta hata short time guest houses zilizotamalaki nchini zina viti wakati mashule hayana viti. Hii maana yake ni kwamba biashara ya ngono wakati mwingine inaonekana kuwa na thamani kuliko elimu.
             Ukienda kwenye mabaa unakuta viti vimejaa hata vingine havina wa kuvikalia wakati watoto wa hao hao wanaokunywa wanakaa chini. Hata ukilinganisha wauza baa na walimu utagundua kuwa baadhi ya wauza baa wanaotesha vitambi wakati walimu wakikonda. Ukiangalia hata polisi ambao kazi yao inapaswa kuwasulubu na kuwakausha kama si kuwakondesha, wana vitambi ikilinganishwa na walimu waliokondeana.
            Ukitoka hapo waangalie wanasiasa ambao kimsingi ndiyo wanaotunga sheria. Wengi wanalipwa mabilioni wakati wataalamu wakikimbia nchi tokana na mishahara haba wakati wao si wataalamu wa chochote zaidi ya siasa.
            Kituko kingine japo kinasikitisha ni ukweli kuwa pombe inapatikana kila mahali nchini. Vitabu viko wapi? Hakuna. Tuna viwanda vya bia vingi wakati watunzi na wachapishaji wa vitabu wakizidi kudodeana kutokana na kutokuwa na mkakati wa serikali wa kutumia kazi zao kama ilivyokuwa awali.
            Sambamba na kupatikana pombe, hata kondomu zinapatikana lakini vitabu hakuna na kama vikipatikana vingine havikidhi viwango tokana na ubadhirifu bado vinatumika wakati vinavyokidhi viwango vikidoda kutokana na watunzi kutokuwa na mjomba kuwatetea. Watu wanaandika au kutunga vitabu vya ajabu na kuviweka kwenye mitaala wakati wakikataa vitabu vya maana.
            Wakati wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji walikuwa wakikwepa au kusamehewa kulipa kodi, watoto wetu waliongezewa ujinga badala ya maarifa tena kwa kutozwa kodi ya kulanguliwa. Tuna vyuo vingi vya hovyo kama St. Joseph ambacho hivi karibuni kilibainika kuwa bomu. Kama haitoshi, tuna academia za kitapeli ambazo zinakazania watoto waongee kiingereza lakini bila maarifa. Je kiingereza ndiyo elimu na maarifa au ni zaidi ya lugha?  Je Academia hizi zinakaguliwa vya kutosha kuona kama zinatoa maarifa yanayohitajika badala ya kusikiliza matakwa ya wazazi ambao wengi si wataalamu wanaoamini kuwa kujua kuongea kiingereza ndiyo kuelemika ili kuwatoa fedha?  Kiingereza ni muhimu hasa wakati huu wa utandawazi na tukizingatia kuwa kiingereza ni lugha kubwa kuliko yoyote duniani;na inatumika karibu duniani kote. Hata hivyo, tunapaswa kuwapa na ujuzi na maarifa watoto wetu. Mwandishi wa makala hii–pamoja na kusoma shule za “Kiswahili”–ameandika vitabu vingi vikiwemo vya kiada ambavyo vinafundishwa kwenye nchi zinazoongea kiingereza kama Afrika ya Kusini na Zimbabwe ambazo kiingereza ni kama  lugha yao ya kwanza–kuonyesha kuwa elimu si lugha bali maarifa.
            Chini ya Kikwete tulilewa na biashara hasa uchuuzi kiasi cha kuufanya kama jibu la kila tatizo. Hadi sasa walimu hawafundishi kwenye madarasa yao waliyoajiriwa kufundisha; badala yake wanafundisha kwenye madarasa ya tuisheni na hakuna anayestuka. Sisi tuliosoma miaka ya themanini hatukusoma tuisheni; lakini bado tuliweza kufanya vizuri tokana na kuwa na mfumo mzuri wa elimu. Chini ya ulevi wa kimfumo, leo tuna kila aina ya upuuzi unaiotwa elimu wakati ni upuuzi na ujinga. Nidhamu na motisha kwa wanafunzi imetoweka baada ya kushuhudia watu ima wakiimbia umma au kuuza mihadarati na kutajirika hata kama hawajui kusoma na kuandika. Watu wanafikiria kutunga mistari ili waukate wakisahau kuwa ni wachache wanaoweza kuukata ikilinganishwa na wengi wanaoukata kutokana na elimu zao.
            Uoza chini ya Kikwete ulikuwa mwingi tu hadi kukawa na dhana kuwa nchi ilikuwa ikijiendea tu bila mwelekeo wala kiongozi.
            Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli lazima aondoe hii kadhia kwa kuufumua na kuusuka mpya mfumo wetu wa utawala; kwani ni wa kilevi zaidi ya uchapakazi wala kutumia akili. Kituko, hata ikija kwenye siasa, tuna vyama hadi vya mfukoni vikijiita wa siasa wakati ni vya mission to town. Hapa hujagusia hata imani zetu ambapo tuna hata dini za ajabu ajabu zinazofanya miujiza ya kuwaibia wananachi wetu huku serikali ikiangalia tu.Tuna kila aina ya upuuzi kuanzia wa kufikiri hata kutenda. Kwa kuangalia haya yote kati ya mengi, unaweza kujenga hitimisho kuwa chini ya utawala wa Kikwete nchi ilikuwa imegeuzwa ya kilevi kiasi cha kufanya kila kitu kilevi wakati wale waliopaswa kutustua nao walikuwa wana ulevi wao kama kusafiri nje, kuombaomba, kushabikia upuuzi, kutegea, kutofanya kazi, kutofikiri bila kusahau kufuja na kuiba kana kwamba hakuna kesho. Nadhani hili ni somo kubwa kwa Magufuli.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: