Wednesday, 13 April 2016

Kijiwe kutuma mjumbe Panama


            Baada ya kampuni ya uwakili ya Fonseca ya nchini Panama kuwaanika wezi wenye maulaji, kijiwe kinataka kumtuma Msomi Mkatatamaa kwenda kule kubaini na kutaka FONSECA ifichue na majina ya majambawazi ya Kibongo yaliyoficha njuluku kule.  Hoja hii imeletwa na Mgosi Machungi akishangaa kwanini wezi wetu hawakutajwa kwenye expose iliyotolewa hivi karibuni.
            Baada ya kuamkua, Mgosi anaamua kuanzisha mada, “Wagoshi, leo nina bonge ya inshu juu ya ufichaji njuuku kue Panama Canai. Mmesoma oodha ya vigogo wa Kiafiika waioficha njuuku kue Panama?”
            Kabla ya kuendelea, Msomi anaamua kutia guu, “Orodha ninayo hapa,” anachomoa jarida moja kubwa la kimataifa la masuala ya njuluku na kuliweka kwenye benchi kila mtu aone. Mchunguliaji analidaka huku kila mmoja akitoa mimacho kuambua kilichomo kwenye jarida hili.
            Mipawa anakula mic, “Pamoja na kukaribisha ufichuaji wa majambazi yanayojificha nyuma ya vyeo, taarifa hii imenikera sana.”
            Kabla ya kuendelea, Kapende anauliza, “Eti hii taarifa adhimu imekukera? Au mwenzetu nawe umeficha mshiko au jamaa zako?”
            Mipawa anajibu, “Siyo hivyo ndugu yangu. Mie nipate wapi mshiko wa kuficha Panama na ukapa na ukata huu ndugu yangu? Kilichonikera ni taarifa hii kutokuwa na majina ya mafwisadi wetu walioficha njuluku kule. Ni hilo tu. Vinginevyo naiunga mkono taarifa yote.”
            Msomi anakatua mic, “Mheshimiwa Mipawa huna haja ya kuchukia. Kwani mambo bado. Huu ni mwanzo tu. Majina ya majambazi yako yatakuwamo–huenda kwenye orodha nyingine itakayotoka–ambayo nimeishahakikishiwa kuwa inaandaliwa.”
            Baada ya Msomi kusema hivyo, kila mmoja anamtazama mwenzake kwa mshangao. Kama amegundua ambavyo wanakijiwe wameshangaa na kudhani hizi ni Kamba, anakula mic tena, “Najua ninaposema nafuatilia, wapo watakaotia shaka wasijue kuwa hawa wanasheria wawili wenye kampuni ya Fonseca yaani, Jürgen Mossack na Ramón Fonseca, nimewafundisha sheria nilipokuwa nafundisha kwenye chuo kikuu cha Yale kule kwa Joji Kichaka. Hivyo, ninamanisha ninachosema.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakamua mic, “Kaka Msomi iwe hivyo. Nangoja kuona orodha hii ili nijihakikishie kama wote wapo au ni danganya toto ya kutaka kupewa mshiko tena ili kuwafichia wengine madhambi yao. Maana haiwezekani kaya nyingi za Afrika zitajwe bila Danganyika kuwemo angalau mmoja.”
            Kapende hajivungi. Anakwanyua mic, “Hata mimi kusema ule ukweli, orodha hii haijanikuna. Bila kuwataja akina Rugemalayer, Rizi, Ana Tamaa, Ana Kajuamlo Tiba na majambazi wengine sitaiamini.”
            Msomi anarejea, “Inawezekana wezi wetu hawafichi kule hasa ikizingatiwa kuwa maficho ya njuluku si Panama tu. Nani alijua kuwa visiwa vya Jersey ni maficho kabla ya ujambazi wa mzee wa Vijsenti na Roast Tamu kugunduliwa? Kuna sehemu nyingi zinakofichwa njuluku kuanzia Dubai, Mauritius, Isle of Man, Cayman, Bahamas, London, Paris na kwingineko. Hivyo jamani vuteni subira watapatikana.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu, “Mie watajwe wasitajwe hainisumbui. Nijuacho ni kwamba wapo wezi wetu. Hata hivyo, tunapaswa kujiuliza. Hata wakitajwa tutawafanya nini zaidi ya kupiga kelele na kunyamaza? Wako wapi waliotajwa na Uswisi hata mjengo ukapiga kelele na kuwagopa?”
            “Mambo iko badilika dugu yangu. Hii dokta kanyaji kama napata jina ya hii naficha juluku Panama takamata yeye kama nakamata Hasi Tilya na miji mingine. Hapana fanya chezo na dokta Kufuli veve,” anajibu Kanji.
            Mheshimiwa Bwege haridhiki. Anatia guu tena, “Hapa hakuna cha kufuli wala funguo. Kama unaona kufuli lako laweza kuwafunga majambazi wetu, jiulize kwanini halijashughulikia Escrew na kubadili mikataba ya kijambazi ya uchukuaji katika madini na nishati kayani? Kama unaona kufuli–sijui funguo–mbona amegwaya kuzitaka mamlaka za Uswizi ambazo zilionyesha utayari kurejesha njuluku zetu kufanya hivyo?”
            Mpemba anaamua kula mic, “Wallahi hapa Mhishiwa Bwege wankuna japo wankata. Nami nshangaa sana. Kama kweli huyu Makufuli amaanisha asemacho, kwanini asikamate lau wevi wa Kagoda waniojulikana hata kwa kunguru? Mbona hajaingilia kati kwenye wizi wa UDAA ambao uko wazi kabisa?”
            Msomi anakula tena mic, “Najua–kwa sasa wengi wanahangaishwa na kutaka kujua majina ya wezi wetu–yapo mambo mengi makubwa yatatokea. Kama Makufuli atakuwa makini na kutaka taarifa za mabenki mengi kayani yaliyokuwa yakiibia sirikali na kuikopesha njuluku hiyo hiyo yaliyoiibia, tutasikia mengi. Nyie tegeni masikio mtasikia na kuona mengi hata ambayo hamkutegemea. Mnadhani hii njuluku inatoroshwa na nani kama si baadhi ya mabenki na Bureau de change zilizotapakaa kayani kama uyoga?”
            Mpemba anakatua mic tena, “Usemayo Msomi ya kweli. Nshangaa sana kuona bureau de change nyingi zenye kutia shaka zikiachwa ziendelee kutorosha njuluku zetu wallahi.”
            Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si simu ya Msomi ikalia. Kumbe ni Fonseca walikuwa wakimpa maendeleo ya kinachoendelea kule Panama.
Msomi anapokea simu na kusema, “Thanks brother, I am in the process of coming over to check more names.
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili 13, 2016.

No comments: