Wednesday, 20 April 2016

Kijiwe chatongoa Nkapa Foundation


            Hivi karibuni bwana nkubwa bingwa wa kuzodoa wenzie Ben Tunituni Makapi alikuwa na harambee ya kuchangia kampuni yake iitwayo Makapi Foundation. Kwa vile huyu bwana aliwahi kuwika kuliko hata jogoo kiasi cha kuogopewa akiwa kwenye ulaji–kabla ya kugeuka zilipendwa hasa alipobainika kufanyia biashara patakatifu pa patakatifu–wanakijiwe walipenda kwenda kumdeku alivyo mpole na tegemezi sasa.
            Kapende ndiye anayeanzisha mada, “Nadhani wote mnajua kuwa kesho ni siku ya harambee ya kunchangia Mr Ben na kampuni yake ya Makapi Foundation.”
            Kabla ya kuendelea, Mijjinga anauliza, “Sisi ulaji na biashara ya wanene tena waliotuchuuza kwa wachukuaji waliowapa jina zuri la wawekaji vinatuhusu nini?”
            Kabla ya kuendelea Mipawa anakatua mic, “Mie inanihusu sana hasa nikikumbuka nyodo za jamaa. Mie nitakwenda–licha ya kutoa mchango wa kahawa–kuona jamaa alivyolainika kiasi cha kutegemea magacholi na wengeni wenye kutia shaka kumchangia kile ambacho hakupaswa kuomba kwa vile alikuwa akikimilki. Ama kweli cheo ni dhamana,” anamalizia huku akiangua kicheko.
            Mgosi Machungi anakamua mic, “Hawa anaochangia njuuku huyu jamaa mwenye nazo wamekosa pa kuziweka. Huenda kuna kitu wananunua. Kama anataka njuuku si angeenda kwenye benki na kuchukua kwenye akaunti ya Kiwia Coaa mine na kuchota atakavyo?”
            Mheshimiwa Bwege anaramba mic, “Usinikumbushe Kiwila na uwekezaji wa kijambazi ndugu yangu. Nadhani jamaa anatukoga. Ana shida gani ya njuluku wakati akienda pale MM bank anachota njuluku toka kwenye akaunti ya Fursa Sawa kwa Yote? Ama kweli waroho hawatosheki. Pamoja na kufanya biashara akiwa kukuu yeye na nkewe, vigegemezi na vivyele bado anaendelea na biashara hata ya kubomu! Ajabu, wakati Makondakonda akiwafukuza ombaomba wa mitaani, anawagwaya hawa wanene wa maofisini. Hivi harambee siyo uombaomba hata kama unafanywa na wanene?”
            Kabla ya mheshimiwa Bwege kuendelea, Mbwamwitu anamchomeka, “Mmesahau kuwa jamaa alitubinafsisha na akajibinafsisha mwenyewe? Huoni anavyochangiwa na wale aliotubinafsisha kwao asijue naye amajibinafsisha?”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, “Najua wengi wanashangaa ni kwanini kuhudhuria changishafedha ya mjivuni. Mie naliangalia hili tofauti. Lazima twende kujenga urafiki na kujua jinsi mambo yanavyokwenda halafu tumripoti kwa Dokta Kanywaji atumbuliwe jipu. Bila kwenda pale kuona nani ametoa nini na kiasi gani kujua kama analipa au kukwepa kodi au kushiriki kwenye kashfa na ufisadi mwingine, hatuwezi kuwajua na kuwashughulikia. Lazima twenda pale na kujua ni wafanyabiashara wangapi wanamfadhili ili tujue kama wana udhu au la.”
            Kabla ya kuendelea, Mpemba anakula mic, “Yakhe hapa wanstua kweli. Lazima nienda jua kama hii kampuni yajamaa yafanyiwa ukaguzi wa mahesabu. Pia nitataka kujua kama ile ya nkewe ya Fursa sawa kwa wote kama nayo yakaguliwa ati. Hapa lazima twende jifunza yale tusojua ili tuyajuapo tuyafanzie kazi ya kutumbua majiipu.”
            Kanji aliyekuwa akiangalia tu anakula mic, “Mimi ona wile hii kitu juri sana. Kama kuba nastaafu nanza biasara na nasaidia sikini iko jambo juri sana. Pia napata fursa juana na fanyabiashara ile nasaidia vakati iko darakani nayo isaidie yeye na yeye isaidie vananchi.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe hakubaliani na mshikaji wake Kanji. Anakula mic, “Nadhani mnene yeyote akitaka kuwasaidia wananchi aanzishe sera nzuri na si za kuwachuuza halafu anakuja kuunda kampuni ya ulaji binafsi kwa kisingizio cha kuwasaidia. Kama alishindwa kuwasaidia alipokuwa anaongoza lisirikali ataweza kwa vijisenti hivi vya kusimangiwa anavyopewa na wanaomsanifu au uvuvi wa kufikiri?”
            Maneno ya Sofi yanamkuna Msomi kiasi cha kumuangalia kwa mshangao huku akimpoka mic, “Da Sofi siku hizi umegeuka mwanamapinduzi wa kupigiwa mfano. Kwa mtu aliyekusikiliza miaka iliyopita akaondoka, akishiriki vikao leo anaweza kushangaa kuwa huyu anayeongea huenda ni pacha wako. Usemayo ni kweli. Kama gendaeka alishindwa kuwasaidia hao anaodai anataka kuwasaidia leo amepata wapi huo upendo kama siyo kuwatumia kutafutia ulaji kama alivyokuwa akifanya bi mkubwa wake na yule wa mrithi wake? Nadhani tungefanya kila iwezekanavyo tumfikishie taarifa Dokta Kanywaji ili aamuru makampuni uchwara kama haya yakaguriwe na kutumbuliwa. Hamkuona alivyomkataza bi mkubwa kufanya biashara hii ya NGO?”
Mijjinga naye anaamua kurejea, “Nadhani tukubaliane. Jamaa baada ya kuachia ulaji, ameamua kujifunza toka kwa wenzake wa kaya zilizoendelea ambao huanzisha Foundations ili kuendelea kuwatumika umma. Hata hivyo, alishahau kitu kimoja muhimu kuwa wenzake hufanya hivyo kuendeleza mazuri waliyofanya tofauti na hawa wetu wanaotafuta sehemu ya kuendelea kulia na kupatia umaarufu. Kusema ukweli sioni cha mno wala cha maana Dungong Ben anacho kwa walevi ambao–kama wengi walivyokwishasema–aliwachuuza tokana na ujinga na uvivu wake wa kufikiria hadi kumpa ujiko Dokta Kanywaji. Hivi mzee Ruxa, Ben na Jake wangefanya vizuri unadhani Dokta Kanywaji angekuwa big deal kama alivyo sasa? Naona tukubaliane. Twende kule kumzomea hakuna cha nini wala nini na kumwambia dogo Makondakonda naye amtimue au vipi? Lazima tukate mzizi wa fitina. Umeona ambavyo Dokta Kanywaji wala hakuhangaika kwenda kule?
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la Ben. Acha tulikimbize ili kulimwagia kahawa ya moto!
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: