Sunday, 9 October 2016

Je watanzania tunaelewa tunachofanya na tunachotaka?


            Kashfa mbili za hivi karibuni zimenifanya nifikiri upya kuhusiana na mikakati madhubuti anayofanya rais John Pombe Magufuli.  Kashfa hizi–yaani ile ya bandarini ambapo mita za kupimia mafuta hazijafungwa pamoja na wahusika kuhakikisha zingefungwa na ile ya watendaji wa Halmashauri ya mji wa Bukoba kutaka kuiba fedha ya waathirika wa tetemeko–zimenikatisha tamaa japo zimenifikirisha.
            Kwa hali ilivyo ambapo kila mtu anataka kutumia ofisi ya umma kujitajirisha hata kama ni kuwa kuwauza watanzania, nashindwa kuelewa kama watanzania wanamuelewa vizuri rais Magufuli na harakati za kuwakomboa anazofanya. Inasikitisha na kukatisha tamaa; ingawa hatumshauri rais na watendaji wake wenye mapenzi mema na taifa kukata tamaa. Kilichojitokeza kwenye kashfa hizi mbili ni ushahidi kuwa watu wetu walio wengi hawajakubali kubadilika hadi wabadilishwe kwa nguvu. Na si hao tu. Hata ukiongea na watu wa kawaida mitaani waliozoea vya dezo vitokanavyo na mabaki ya chumo la mafisadi, wanamlalamikia Magufuli kwa kufanya maisha yao yawe magumu baada ya kukosa mabaki waliyozoea kutupiwa na kupwakia.
             Tokana na tishio hili, tunatoa baadhi ya maangalizo ili kuweza kupambana na kadhia hii inahyotishia kulifuta taifa la Tanzania toka kwenye uso wa dunia.
            Mosi, tunashauri rais na serikali yake aufumue na kuusuka mpya mfumo mzima wa uendeshaji wa taifa letu. Watu walishazoeshwa kuishi kihalifu bila kujua kuwa kuna maisha nje ya uhalifu. Hatuwezi kuendelea kuwa taifa la wahalifu, majambazi, wauza unga, vidokozi, wavivu, wababaishaji na wachumia tumbo. Hivyo, rais lazima aelekeze nguvu zake kwenye kuweka mfumo unaoweza kujitegemea kupambanana maovu badala ya kumtegemea mtu mmoja au kikundi cha watu. Wenzetu kwenye nchi zilizoendelea wamefanya hili. Hawategemei usongo au uzalendo wa rais au watu wake wa karibu bali mfumo wenye kanuni zinazoweza kujiendesha hata kama nchi itakuwa ikiongozwa na chizi.
            Pili, hakuna njia ya kuufumua na kuufuma mfumo wa uendeshaji taifa letu unaoweza kufanikiwa bila kuwa na sheria na mamlaka yanayousadia katika kujiendesha. Hapa ndipo hitajio la kurejesha rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyoandikwa na tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba linapokuwa halikwepeki wala kuahirishwa. Kama kweli rais Magufuli amedhamiria kuiondoa Tanzania kwenye mikono ya uhalifu na ujambazi, atapaswa kupingana na msimamo wa chama chake wa kuua katiba mpya ambao ulitokana na viongozi waliokuwa madarakani wakati ule kuchelea kufikishwa mahakamani kwa uovu waliotenda.
            Tatu, tunamshauri rais Magufuli abadili msimamo wake wa kuwalinda viongozi wastaafu wanaotuhumiwa kuifikisha nchi yetu hapa ilipo ima kwa uzembe au uovu wao wa kujitajirisha wao na jamaa zao haraka kwa kuwaumiza watu wetu. Hili si kuzua. Wanajulikana hata makosa waliyotenda yanajulikana karibia kwa watanzania wote.
            Nne, tumekuwa tukipigia kelele sheria ya maadili ya utumishi wa umma bila kupata majibu. Bila kuwa na sheria ya maadili kwa utumishi wa umma rais anachofanya ni kujichosha kwa kutwanga maji kwenye kinu akitegemea kupata unga. Hatafanikiwa zaidi ya mikakati yake kuishia kuwa mbio za sakafuni ambazo mwisho wake unajulikana.
            Tano, badala ya rais kupoteza muda na nguvu nyingi kupambana kama mtu binafsi, aelekeze nguvu zake kwenye kuujenga mfumo endelevu na wa uhakika usiotegemea mtu au kundi la watu. Kwa mfano, iundwe sheria ya kumtaka kila mtanzania si kutangaza mali zake tu bali kueleza namna alivyozipata. Kila binadamu anayo na anajua historia ya maisha yake. Matajiri wote tulio nao nchini walazimishwe kueleze historia za utajiri wao tena kwa maandishi yatakayotunzwa na kuhakikiwa kisheria ili kuangalia kama kuna namna ya uovu na uhujumu waliotendea taifa. Hatuwezi kuendelea na mfumo huu wa kijambazi bado tukajidanganya kuwa sisi ni kisiwa na taifa la amani. Amani haiwezi kuwepo bila haki kwa wote. Watanzania walio wengi hasa wale maskini wana hasira na serikali kutokana na kutumika kama koleo la kuchotea utajiri kwa wachache wakati wengi wakiendelea kuumia. Rais amesikika mara nyingi akisema kuwa anawapigania watanzania maskini. Je hili ni kweli wakati anaendelea kuwalinda wale waliosababisha huu umaskini anaodai kupambana nao? Huwezi ukapambana na umaskini sambamba na kuwalinda waliousababisha tokana na usimamizi wao mbaya wa mali na fedha za umma. Hapa ndipo hitajio la hata kusimamisha marupurupu na mafao ya viongozi wastaafu walioboronga linapokuwa haliepukiki kama kweli tunadhamiria kurejesha taifa letu kwenye mstari. Kuendelea kufanya hivyo si sawa na kutwanga maji tu bali kujenga daraja kuzuia maji wakati ukishuhudia yakijipitia bila kikwazo. Hii ni sawa na kutumia pakacha kuteka maji. Utaishia kuloa tu; na jua likipiga utakauka na kuchomwa moto tu.
            Sita, tufanye kile ambacho wenzetu wameishafanya. Hivi karibuni kule nchini Brazil, rais Dilma Rousseff, alifukuzwa madarakani tena kwa si kwa makosa binafsi bali kushindwa kueleza ukweli kwa umma. Nchini Israel waziri mkuu wa zamani, Ehud Olmet alihukumiwa kwenda jela baada ya kugudulika kuwa alitumia madaraka yake vibaya. Nchini Georgia waziri mkuu wa zamani Ivane Merabishvili alihukumiwa miaka mitano jela kwa makosa ya jinai.
            Kituko ni kwamba wakati wenzetu wakiwafukuza hata kuwafunga viongozi wao waliotenda uovu sisi tunawahukumu mawaziri wetu vifungo vya nje tena vya muda mfupi. Namna hii hatuwezi kurejesha Tanzania kwenye mstari. Ningekuwa Magufuli hata kesi za akina Basil Mramba na Daniel Yona zingerejerewa upya na kutoa adhabu zinazostahili. Sijui kama watanzania tunajua tunachoka.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

No comments: