Saturday, 1 October 2016

Mlevi kuomba kuwa mkurugenzi wa bandari

 
             Baada ya kushuhudia, ubabaishaji, ufisadi, ujinga na kila aina ya madudu bandarini alipotembelea Dokta Kanywaji, Mlevi napanga kuandika barua ya kuomba niwe mkubwa wa eneo hili nyeti ili nimsaidie rahis kunyoosha kaya ya walevi inayoliwa kilevi kama shamba la bibi. Kwa ambao hawakuwa wamelewa walivyoona kitimoto Dokta Kanywaji aliyowapa wababaishaji wetu pale bandarini watakumbuka jamaa walivyokuwa wakitoa majibu ya kitoto. Jamani, hata kudanganya hamjui? Halafu eti mnajiita wasomi wakati hamna hata chembe ya uzalendo! Yaani hawa waduwanzi kweli hawana maana. Yaani wanadanganya waziri mkubwa’ na wanaona kama haitoshi. Wanamdanganya hata dingi mwenyewe. Sijui atawafanya nini kwa walivyomuudhi ukiachia mbali kuibia kaya yetu kiasi hiki wakati walishaonywa? Wana bahati tena ya mtende. Kama ningekuwa mimi, licha ya kuzaba majuha vibao, ningeondoka nao waelekee Ukonga wakati wakingojea hatima yao.
            Napanga kuomba niwe mkubwa wa bandari ili kupunguza makali ya kaya yetu kuwa Kaya inakuwa kama ya mfukoni mwa majizi na walafi fulani.  Mie sitalea gendaeka wala kupokea kitu kidogo hata kikubwa kwa manufaa binafsi kama hawa waliotenda dhambi isiyopaswa kusamehewa ya kumdanganya dingi  mwenyewe. Kama nitateuliwa nitaunda kitengo cha ushushu cha kumulika kila kitengo bandarini. Watakaonidaganya ili nimdanganye dingi lazima nishauri wanyongwe haraka.
            Hakuna kitu kilinitisha kama kushuhudia mikompyuta imefungwa lakini haifanyi kazi yoyote ya kukagua mizigo. Hii maana yake ni kwamba magaidi wakiipata na wakaamua kuingia kayani mbona wataingia tena kwa ulaini? Nani anapenda kaya yetu iwekwe rehani kwa sababu ya upuuzi na uroho wa gendaeka wachache wasiotaka kubadilika?
            Lo! Nimechonga sana kiasi cha kusahau kueleza kwanini nina usongo na sifa za kuwa mkubwa wa bandari. Si juzi tukiwa tunakata ulabu akatokea mlevi mmoja akatutukana kinyumenyume akisema kuwa kaya yetu haina walevi bali majipu matupu kuanzia juu hadi chini. Kusema ule ukweli, kama siyo kunizuia huenda ningekuwa Ukonga nangoja kunyotolewa roho kwa kumnyotoa roho mlevi mwenzangu. Hata hivyo baada ya kutafakari niliona ukweli na kumpa ofa huyu jamaa aliyezibua akili yangu na kuamsha usongo wangu hadi nikaamua kugombea udingi wa bandarini.
            Baada ya kusukuti niliona nuru na ukweli kuwa kaya yetu sasa yaweza kuitwa kaya ya madudu. Hebu angalia trajectory ya dingi alipopita utagundua madudu matupu kama si majibu.
Uwanja wa ndege madudu matupu. Mitambo imeharibiwa ili kupitisha mibwimbwi. Sijui nao bado wanaendelea na mazoea yao hata baada ya kufichuliwa kama bandari? Bandari madudu kama mlivyoshuhudia wenyewe mibaba mizima ikiongea vitu vya kitoto vikidhani wote ni watoto kama yenyewe. Mmeua flow meters mnakuja na upuuzi. Mipakani madudu
Mita za kupima mafuta aka flow meters madudu. Wasimamizi madudu, mikompyuta madudu. Nai madudu madudu matupu kiasi cha kufikiri kuita kaya yetu kaya ya madudu kama siyo ya vidokozi, majambazi na mafwisadi.
            Hata hivyo silaumu sana. Kama ilifikia mahali hata bedroom ya kaya yaliyajaa madudu chini ya Njaa Kaya. Hawa wanaoendelea kuendekeza njaa, tamaa na ujanjaunjanja hawahitaji kutumbuliwa bali kuchomwa moto maana ni kansa tupu. Hata hivyo, tusiwalaumu wao tu. Nimepiga kelele hadi koo limevimba nikimtaka Dokta Kanywaji arejeshe maadili ya utumishi wa umma na taifa ambapo kila mlevi atapaswa kueleza alivyopata ukwasi wake. Hata hivyo, bila kurejesha katiba mpya haya yote yatawezekanaje zaidi ya kaya kuendelea kuwa ya madudu?
Tuonane wiki ijayo,
Mlevi-Uwanja wa Fisi
Tandale.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: