Wednesday, 19 October 2016

Kijiwe chamkumbuka mzee Mchonga

 
          Baada ya rais Joni Kanywaji Makufuli kunusuru mishiko kibao ambayo wanene wangekamua kwenda kujimwaya kule Simiyu, Kijiwe kilifunga safari hadi kule Mwitongo kumuona mama Merry ili kumpa taafu kwenye maadhimisho ya miaka 17 ya kifo cha mzee Mchonga wa Burito.
            Kapende ndiye anaanzisha mada. Anasema “wazee mnasemaje baada ya kuyoyoma miaka kumi na sabaa tangu mzee Nchonga arejeshe namba? Maana mie naona ni kama jana.”
            Mgoshi Machungi anamchomekea “kwani ujasikia wahenga waivoshema kuwa siku huwa hazigandi. Mimi namkumbuka huyu ngui hasa kipindi hiki tuipochagua dokta Joni Kanywaji Makufui ambaye si haba anajitahidi kujaibu kuvaa viatu vya dingi huyu. Uisikia aivozuia wanene kujiipa mamiioni kwenda Simiyu kutumbua na kuringishiana mashangingi?”
            Mipawa hangoji Mgoshi aendelee; anakatua mic “natamani mzee Nchonga angekuwa hai huenda angewalazimisha hawa wajivuni kurejesha katiba mpya waliyoiua kwa kuogopa ujambazi na madhambi yao wasiozee lupango. Sijui kwanini na dokta Kanywaji anasitasita kutuletea katiba mpya kana kwamba naye anapanga kubadili kibao baadaye.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “kaka hata mimi nashangaa anashindwa nini wakati ameonyesha nia ya kuirejesha kaya kwenye mstari. Kama atarejesha nchakato wa katiba mpya atakuwa ameweza kuvaa barabara viatu vya mzee Mchonga.”
            Mbwamwitu anachomekea kwa utani “bado ni mapema jamani. Mbona mbavu za mbwa za kaya walizogawana hajazirejesha au anafanya vitu kwa kuchagua atakavyo badala ya kutumia sharia utadhani kaya hii ni mali yake binafsi?”
            Msomi Mkatatamaa anatia daruga; na kusema “si kwamba dokta Kanywaji hajui umuhimu wa katiba mpya. Anajua fika. Sema anaogopa akirejesha itamnyina nafasi ya kutembeza undava kama ilivyo kwa sasa. Anajua fika kuwa katiba mpya ni kama upanga wa ncha mbili hasa kwa dingi kama yeye anayetumia tuturinga au vipi. Ona sasa mnavyoanza kutaka arejesha mbavu za mbwa za umma wakati naye alikuwa mnene wakati jinai hii ikiasisiwa na kutekelezwa. Nadhani vitu kama hivi ndivyo vitafanya katiba mpya iendelee kuuawa. Hili la kusema kuwa ana mpango wa kugeuka na kukwapua kama washenzi waliomtangulia silikubali. Jamaa ana usongo na kaya ingawa kaya haiwezi kujengwa kwa usongo wa mwanakaya mmoja.”
            Anapiga chafya na kuendelea “nadhani dokta Kanywaji anapaswa kumuenzi mzee Mchonga vilivyo. Japo na mzee Nchonga aliwatala kimituringa chini ya ujima wa chama kimoja, alikiri pale vyama vingi vilipoanzishwa kuwa lazima kila mmoja abadilike. Kitu kingine ambacho alifanya mzee Mchonga ni kuanzisha mfumo na sera vinavyoeleweka vya utawala. Kwa sasa sijui kaya yetu inatawaliwa na sera gani pamoja na usomi wangu.”
            Mpemba anampora Msomi mic; na kutambaa “yakhe unkumbusha kitu muhimu sana. Usemayo nkweli. Bila sera na nfumo twawezajikuta kubaya. Lazima hapa tunshauri jamaa atofautishe kati ya kauli mbiu na sera. Maana hata walontangulia walikuwa na vitu kama hivi. Mwakumbuka uwazi na ukweli ulioishia kuwa ufichi na urongo? Mwakumbuka maisha bora kwa wote yalotokezea kuwa mateso kwa wote bora sie wenye ulaji hatumo? Nikija kwa nzee Nchonga, nasema wazi. Huyu hakuwa ntu wa kawaida wala huwezimlinganisha na vinyankera walonfuatia. Dokta Kanywaji pekee ndo aonyesha lau kuelewa somo alofundisha mzee Nchonga. Walobaki wote mahabithi watupu.”
            Kanji anakamua mic “Ami veve sema kitu moja kuba sana. Mzee Chonga nasifu yeye. Alikuva disciplined. Hapana shukua mali ya chovu. Hapana toto yake hata moja nakuwa tajir ya kuibia mali ya umma. Hata bibi yake hapana naanzisha NGO. Chonga napenda yeye hata kama nakamata jumbani ha Hindi mingi sana.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu kinamna huku akiwa anaonyesha kama kuudhika. Sijui nani amemuudhi; anakula mic “hakuna walioniudhi kama wanaotaka kumlinganisha mzee Nchonga na mahabithi aliwaamini wakamuangusha. Kimsingi, Mchonga angekuwa hai angekuwa frustrated so much that he would remain at home kwa kuona aibu kwa alivyounga mkono majizi yakaja na kumuangusha. Hata hivyo, kama mzee Mchonga asingekufa kuna wengine urahis wangeusika kama wale marafiki zao waliowatosa. Unategemea upuuzi kama Njaa Kaya ungeweza kupelekwa ikuuu siyo? Saa nyingine hata dokta Kanywaji asingekuwa rahis. Hapa ndipo namsamehe mzee Nchonga kwa kosa la kuunga nkono vidhabi waliomgeuka na kumuangusha. Maana asingefanya kosa hili wale waliojenga mazingira ya dokta Kanywaji kujipenyeza wasingeingia ikulu na kujenga mazingira haya.”
            Msomi anarejea na kukamua mic “mheshimiwa Bwege naungana nawe. Umeogea jambo moja muhimu ambalo kitaalamu huita circumstantiality. Mzee Mchonga alivyotafsiri wakati ule wakati akiwakingia vifua vinyago vya mpapure na kuwakataa vilaza waliopenda sana kujichekesha kama vyangu. Hata hivyo, tokana na nia yake nzuri, fate iliamua kupitia kile ambacho huitwa divine intervention akapatikana dokta Kanywaji ambaye hata hivyo ana safari ndefu na ya hatari kama atajitwisha zigo pekee na akakataa kurejesha katiba mpya.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si Bombadier ikapita juu yetu tukatamani tungekuwa na  njuluku tungepanda kwenda zetu Mwitongo kimakwelini na si imani!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: