The Chant of Savant

Monday 24 October 2016

Namuonea huruma Magufuli

        
          Akisema amejitoa sadaka kwa ajili ya watanzania, wapo wanaouliza: “Kwani yeye ni Yesu” utadhani Yesu alikuwa mtanzania! Sijui wanataka awatoe wao sadaka kama ilivyokuwa kabla?       Sukari ikiadimika wapo wanaomlaumu rais John Pombe Magufuli wakisema ameondoa vibali. Akiruhusu sukari mbovu iingizwe hao hao wanaohoji: “Kwanini amesahau viwanda vyetu au amehongwa aviue?” Wakati mwingine unashindwa kuelewa nini jema kwa wanadamu. Je mhusika anapaswa kufanya nini zaidi ya kuwapuuzia na kutekeleza yale anayoamini yataleta ufanisi baadaye hata kama ni baada ya kuumia kidogo? Nadhani anachofanya Magufuli ni kuikamua nchi jipu; lazima iumie ili ifurahi baada ya kupona.
Akitumia madaraka yake wanasema eti ni dikteta huku wakilaumu serikali iliyopita iliyoacha kuyatumia ikaishia kuitwa goigoi. Akiacha kuzurura ughaibuni wengine wanasema anahujumu nchi kidiplomasia wakati hao hao ndiyo waliombatiza jinal la Vasco da Gama rais aliyepita.
            Wapo–tena wanaweza kuwa wengi tu–wanaoona urais ni kazi rahisi kiasi cha kuurahisisha urais na kupata fursa ya rahisi kumlaumu rais Magufuli–baada ya kuja na namna mpya ya kufanya mambo kiasi cha kuwaudhi na kuwastua wengi ukiachia mbali kuhatarisha ulaji wao wa dezo waliozoea bila kujua una mwisho. Hawa walioamua–kwa makusudi mazima kurahisisha urais–baada ya kuzoea urais legelege uliopita–badala ya kumkosoa, kumshauri hata kumkumbusha rais, wameamua kuziba macho na masikio hata akili zao ilmradi wajiridhishe kwa kulaumu tu. Wanaojua ugumu wa dhamana aliyotwishwa, licha ya kumuonea huruma rais Magufuli hasa kutokana na hatua za maksudi alizochukua, hujitahidi kumshauri pale anapoonekana kufanya ndivyo sivyo. Tumkosoe anapokosea na si kumhukumu wala kumlaumu, kumkatisha tamaa bila kuvuta subira na kuona matokeo ya anayopanga na kufanya. Tumuongoze badala ya kuwa wepesi wa kushutumu. Yeye hajui kila kitu; na amesema hivyo mara nyingi akiomba tumsaidie na kumuombea. Isitoshe, anayofanya si kwa manufaa binafsi kama waliomtangulia ambao walitanguliza familia zao na matumbo yao kiasi cha nchi kuoza kama ilivyo sasa.
            Kwanini tunamuonea huruma? Amerithi nchi iliyovurugwa vibaya sana tena kwa muda mrefu tu. Tazama anavyopangua safu kwa umahiri na ujasiri unaohitaji moyo wa mwendawazimu. Ni wangapi wameishawapangua ambao waliteuliwa kutokana na ima kutoa rushwa iwe ijulikanayo au vinginevyo au kwa vile walikuwa karibu na wakubwa wa zama zile? Unadhani wanafurahi hawa pamoja na kutokuwa na stahiki wala udhu wa kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma wakifanya yale waliyozoea?
            Kitu kingine kinachofanya nimuonee huruma Magufuli ni ile hali ya kutokuwapo mfumo unaoeleweka, jambo ambalo anapaswa kulifanyia kazi. Hapa ndipo umuhumu wa kurejea Rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyokuwa imependekezwa na wananchi chini ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba. Hata hivyo, Magufuli anawezaje kuliongelea hili wakati chama bado kiko mikononi mwa wale wale walioikataa na kuiua kutokana na uovu na upogo wao? Watamkwamisha; kwa vile bado wana mamlaka tena makubwa chamani. Hivyo, tumpe muda. Najua mengi anayasoma kama siyo kusomewa au kuyasikia toka kwa washauri wake. Nina imani naye. Siku atakapopata nyenzo zote, hakuna shaka. Katiba mpya itapatikana ili imsaidie katika vita yake na kumwepusha kuonekana kama anatafuta sifa au kuwa muungu mtu jambo ambalo ni kumuonea.
            Kinachofurahisha na kuweka tumaini na ushindi ni ukweli kuwa Magufuli si mwoga, si muongo. Si mpenda sifa kama wabaya wake wanavyotaka kumuelezea. Alionyesha asivyopenda sifa pale alipoombwa aliite Daraja la Kigamboni jina lake; lakini akakataa na kupendekezwa liitwe Nyerere.
                        Kitu kingine kinachofanya nimuonee huruma ni ile hali ya kuwa mkweli. Magufuli huongea ya moyoni bila hata kujali madhara yake.  Hata ukimuangalia usoni wakati akisema ayasemayo unaona aina fulani ya ukweli na si ujanja ujanja na unafiki wala ujuaji. Ni kutokana na ukweli huu, Magufuli haogopi lawama pale anapochukua maamuzi anayoamini ni sahihi na ni kwa ajili ya maslahi ya taifa.
            Sifa nyingine inayomfanya awapiku wengi waliomtangulia ni ile hali ya kutotaka wala kupenda makuu. Si mbaguzi wala shufaa. Hata kwenye harakati zake anasisitiza utanzania kuliko itikadi za kisiasa. Rejea amri ya kutaka meya wa Dar es Salaam apatikane bila kujali anatoka chama gani wala kuangalia kama CCM itashinda au kushindwa. Hili limewaudhi na kuwastua wengi ndani ya CCM kiasi cha kumchongea hata kwa mwenyekiti wa chama. Hata hivyo, kuonyesha alivyo mkweli, Magufuli alipotakiwa kujieleza, alisema wazi kuwa CCM ilipoteza jimbo la Dar kwa sababu ya wanafiki wa ndani ya chama. Hivyo, haikuwa vibaya kwa CCM na wanafiki wake kuonja adha ya unafiki wao. Tabu ya watu waliozoea unafiki ni kwamba usipokuwa mnafiki wanakuchukia; kwa vile unawaambia yale wasiyotaka kusikia.
            Tuhitimishe. Jambo jingine ni kwamba Magufuli anaonyesha kuwa na dira. Nakumbuka maneno ya Profesa Issa Shivji aliyesema wazi kuwa Magufuli anaonyesha kujua analofanya kuliko waliomtangulia ukimuondoa marehemu baba wa taifa mwl Julius Nyerere. Shivji si mkurupukaji wala mtu mpenda sifa wala anayeweza kutumiwa kirahisi ingawa bado ni binadamu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili jana.

No comments: