Saturday, 22 October 2016

Maticha wanapoonyesha uanafunzi na waziri akaurudia!

 
            Nilitaka kuandika juu ya kadhia ya kule kwa kina Twambombo tununu ambapo wanafunzi maticha walimshushia kipigo cha mwizi mwanafunzi mmoja mtukutu kiasi cha kujivuka mipaka ya uticha wao na kuishia kumwagwa kwenye mitandao. Nilipoinyaka nilijua kuna tatizo hapa tena si la maticha wala mwanafunzi yule bali mfumo mzima hapa kayani. Sijui kama hawa maticha wanafunzi walikuwa wamesoma, wakasomeshwa na kuiva au ni yale ya voda faster aka mchina?
            Kosa limeishatendeka; hakuna namna ya kulifuta zaidi ya kushughulikia tatizo lakini si matawi. Japo nalonga kilevi, bado ninayo ilmu yangu tena ya ughaibuni. Mie sijaghushi kama ninaoona wakiadhirika kila kucha. Juzi si nilishangaa  nusu kuzimia tena kwenye nsiba baada ya wasfu wa kihiyo aka kilaza mmoja kusomwa. Tulimjua jamaa kama daktari. Lakini ajabu ya maajabu, kwenye wasfu wake hapakuonyesha hata kuwa na shahada moja! Hayo tuyaache;kwani kihiyo yule aliyewahi kuwa nstahiki alishajinyotokea roho japo tunahitaji kuwawinda vihiyo walioko hai na si kungoja mauti yaumbue.
             Tuejeree kwa maticha wanagezi. Je kosa walilotenda na adhabu waliyopewa ya kutimliwa ghafla chuoni ndiyo ndiyo adhabu yake kisheria au wahusika wametumia sheria ya mihemko na kuogopana ukiachia mbali kuwaridhisha walevi kuwa wana kasi ya kutosha? Je mdingi wa ilmu aliyetoa uamuzi huu wa kizimamoto alifanya vikao vyovyote ili kubaini tatizo ni nini, kupima na kujiridhisha kuwa hajavuka mstari au aliamua kwa jazba kwa kuangalia upande mmoja? Je uamuzi wake ni wa kitaaluma au kisiasa? Maana, hawa licha ya kuwa maticha wanagezi, bado wameishapoteza muda na njuluku zao na za kaya ukiachia mbali kuwa kaya inawahitaji kutokana na kuwa na wanafunzi wengi na maticha wachache? Je hili ndilo jibu la tatizo au ni jip utu?
            Kimsingi, hapa nadhani kuna haja ya kutumia busara badala ya jazba.  Nadhani hapa tunajifunza kuwa mfumo wetu wa elimu una matatizo katika maandalizi ya wanafunzi na maticha wetu kiasi cha wengine kutokuwa na nidhamu huku wengine nao kutokuwa wavumilivu wala kujua kanuni, mbinu na sheria za kushughulikia kadhia kama hii ya kwa akina Twambombo.
Umeambiwa wale ni wanafunzi na uanafunzi huruhusu sehemu ya kosa kama njia ya kujifunza.                  
                Hakuna kilichowashangaza walevi kama hii kasi ya kuadhibu matokeo ya mapungufu ya kimfumo. Kwa ushauri nadhani tunapaswa kuchunguza mapungufu kwenye maandalizi ya maticha wetu na namna ya kuwaweka sawa wanafunzi. Sisi tuliosoma zama za mzee Mchonga, halikuwa jambo linalofikirika acha kutenda eti mwanafunzi amkate kibao ticha. How do you do that? Nadhani tunapaswa kubaini mapungufu katika mfumo wetu na kuurekebisha badala ya kuadhibiana kihasirahasira na kihasarahasara.
             Japo nasema kwa nguvu ya vile vifaa ninavyoweka kw asana, naweza kusema tena kwa kinywa kipana kuwa kama hawa vijana yaani maticha wanagezi wangekuwa wamefundishwa saikolojia ya elimu na mahusiano, nadhani wasingefanya walichofanya. Walichofanya ni ushahidi kuwa hawakuandaliwa na wakaiva kitaaluma.
            Ukiangalia upande wa pili, hata wanafunzi wetu nao wanaandaliwa vibaya hasa ikizingatiwa kuwa kuna uhaba wa shule za umma. Sitegemei kama kwenye shule ya serikali au ya seminari tulizosoma sisi hali ingeweza kufikia hapa kabla ya utawala haujagundua na kuchukua hatua mapema kuiepuka. Inapofikia mwanafunzi akamchapa kofi mwalimu, ujue kuna uzembe kwenye mfumo. Anapata wapi hii jeuri kama siyo kulelewa muda mrefu? Inapofikia ticha akaacha kutumia kiboko akatumia fimbo, karate au ngumi, ujue kuna mapungufu yaliyoachwa muda mrefu.  Ticha aliyesoma akaiva kisaikolojia hana jazba wala haraka. Unaweza kumkosea akajifanya kama haoni ila siku akikupata, anahakikisha anafuata taratibu zote na mwisho wa siku unakuwa umepoteza kila kitu. Hata hivyo, tuache utani, kitoto kinakuchapa kibao halafu ukipe maua siyo!
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: