Thursday, 27 October 2016

Kijiwe chashanga Lukuvi alivyoshughulikia kashfa Moro


Image result for lukuvi morogoro
          Baada ya kuzinyaka kuwa waziri wa Ardhi Bill Lukuvi alivamia ofisi ya ardhi ya nkoa wa Moro na kugundua madudu na kuyaacha, Kijiwe kimeamua kumshangaa na kumjadili. Hii ni baada ya Msomi Mkatatamaa kuinyaka kwenye mitandao kulikorushwa video ya Lukuvi akishuhudia ufisadi wa wazi asichukue hatua wala kutoa karipio.
            Msomi anaamua kumwaga inshu akisema “mwenzenu nimepigwa na butwaa hasa nikizingatia usawa huu wa spidi ya “Hapa Job” ya Dokta Joni Kanywaji Makufuli,” anawasha kijisimu chake ambacho siyo Sumsung Note 7. Maana ingekuwa hiyo, kwa zinavyolipuka, kijiwe kizima kingetoka mkuku na kumuacha yeye na bomu lake.
            Baada ya kuwasha kisimu chake cha bei mbaya, si tuliona namna waziri alivyoingia kwenye ofisi ya ardhi na kukuta maelfu ya hati yakiwa yametekwa ili wahusika watoe chochote kitu ndipo wazipate. Hakuna kitu kiliacha hoi kijiwe kama afisa moja la kiume lililomdanganya waziri akashindwa kulinyaka na uongo wake. Alipoliuliza kwanini hati zilikuwa hazitumwi kwa walengwa, lilisema kuwa walikuwa wakiwapigia simu bila wao k uja kuchukua hati hizo. Ajabu waziri alipoliamru jizi hili kupiga simu kwa mmojawapo, lilimdanganya bila aibu kuwa halikuwa na namba ya simu. Bahati ya habithi huyu. Angekuwa bingwa wa takwimu dokta Kanywaji angehoji nini maana ya kusema kuwa walikuwa wamewapigia simu wahusika kwa simu zipi iwapo hili jinga halikuwa na namba za simu.
            Kushindwa kwa waziri kulibana fisadi hili uchwara kulituacha hoi kiasi cha kuhoji uwezo wa mhusika wa kufikiri na kukumbuka wakati uongo aliokuwa ameambiwa haukuwa umepitisha hata dakika kumi. Baada ya kuenjoy aibu hii ya kaya, tuliamua kuanza mjadala.
            Wa kwanza alikuwa Mgoshi Machungi aliyekula mic na kuzoza “Hivi huyu wazii ana tatizo gani jamani. Kwanini hakuiuiza hii jambazi la kaamu kwanini haikuwa na namba za simu wakati iisema kuwa iikuwa imewapigia wahusika simu?”
            Kabla ya kuendelea Mpemba ananchomekea “Yakhe hata mie nshangaa kwanini huyu waziri hakuuliza hilo swali. Yawezekana hawa jamaa wanjuana; vinginevo hapakuwa na sababu yoyote ya nsingi ya kutoliwajibisha hili jizi wallahi.”
            Msomi anakula mic “msimlaumu waziri. Kwa sasa jamaa wengi wanafanya kazi si kwa ujuzi wala utashi bali kuogopa dokta Kanywaji asiwatumbue. Hivyo, unaweza kukuta jamaa hapa alitaka apigwe picha na kurekodiwa video ili aonekana anachapa mzigo hata kama ni bila maarifa kama mlivyojionea.”
            Kapende anampoka Msomi mic “hata ukiangalia maangizo ya kishikaji aliyotoa waziri unahisi kuna tatizo. Kama si kulindana, basi wapo waliopewa madaraka ambayo hawana sifa wala uwezo nayo. Hata hivyo, kwa kiwango cha elimu cha watendaji wetu ambao wengi wao wameghushi, huwezi kujua japo simaanisha kuwa mhusika alighushi kama alivyowahi kudai Keinerugaba Msematrue.”
            Mipawa anakwanyua mic “hapa tusipindishe wala kuogopana. Hawa waweza kuwa waarabu wa Pemba ingawa Pemba hakuna waarabu bali wapemba mnaowachanganya na waarabu wakati wakienda arabuni wanaitwa abid au watumwa.”
            “Yakhe tuheshimiane ati. Wawezaje sema eti tukienda arabuni twaitwa watwana! Hebu niombe nsamaha kabla sijapiga ntu albadili mie.”
            Kanji anamchomekea Mpemba na kuokoa jahazi “Kwanini veve dugu yangu nachukia. Hata sisi hindi kama nakwenda Bombay hapana kubali kuwa sisi ni hindi. Hii kitu kawaida dugu yangu.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu baada ya kuona mada inaanza kupindishwa. Anaronga “Turejeeni kwenye mada waheshimiwani. Mie nadhani hapa hakuna tatizo tena dogo bali kubwa. Ukiangalia namna dokta Kanywaji ambavyo amekuwa akitumbua waovu kuanzia bandarini, TRA hadi Muhimbili, unashangaa na kujiuliza kama baadhi ya watendaji wake wanamuelewa. Kwa namna huyu jamaa tuliyetoka kumuangalia alivyovurunda, hakupaswa kuachwa ofisini na kupewa mwezi mzima ili azidi kuvurunda wakati vijana wanaotaka kazi na wenye sifa wapo kibao mitaani wakioza wakati majizi yakibungua kaya yetu. Nadhani kama mhusika atasoma kitu hiki atabadili uamuzi wake na kufanya kazi badala ya kutaka ujiko au vipi?”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kukamua mic “Jamani mmeona yule kaka alivyonona kwa fedha za rushwa kama anavyosema mheshimiwa waziri? Hakuna aliyeniacha hoi kama dada yangu ambaye ana dhamana ya kugawa hati kutoa macho kana kwamba hana ujuzi wala hajui kinachoendelea. Nadhani hawa jamaa wanapaswa kukamatwa na kuswekwa ndani na kuchunguzwa ili liwe somo kwa wengine ambao hawajaelewa kasi ya dokta Kanywaji ambaye siku zote namuonea huruma kutokana na kuzungukwa na gendaeka wasiojua anacholenga kufanya.”
            Mzee Maneno anakamua mic “kuna namna hawa jamaa wanavyofanya. Maana pamoja na habari hii kujaa kwenye mitandao hasa mabulogu, siioni kwenye magazeti yetu. Inakuwaje waziri anakwenda kwenye kufichua uoza huu haandamani na waandishi wa habari au wameatamia habari baada ya kurambishwa asali? Kama ni hivyo, kwanini waziri hakuwahoji waandishi alioandamana nao; na kama hakuandamana nao ni kwanini wakati hii ni kazi ya umma?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la Lukuvi! Acha twende kumhoji. Tulipotunakaribia kugonga kwenye dirisha si mataa yakaruhusu!
Chanzo: Tanzania Daima, Jumatano jana.

No comments: